Hatimaye washabiki wa Manchester United wamepata kitu cha kushangilia na kujifariji kwa usajili wa Juan Mata kutoka Chelsea baada ya kuanza msimu kwa majanga mfululizo.
United walio chini ya David Moyes kutokana na kustaafu kwa Sir Alex Ferguson wanatakiwa kutetea ubingwa wao na ni jambo linaloonekana kuwa gumu.
Washabiki wamekuwa wakilia kutokana na vipigo kutoka kwa timu kubwa na ndogo na kwa namna ya pekee kwenye dimba la Old Trafford ambako haikuwa kawaida kufungwa.
Hata matumaini ya kupata uwakilishi wa Ligi ya Mabingwa yalianza kupotea lakini kwa kumsajili kiungo huyo mchezeshaji kwa pauni milioni 37.1, Man U wanaweza kuwa na matumaini ya kupanda kutoka nafasi ya saba wanayoshika kwenye msimamo wa ligi.
Kwa upande mwingine, Chelsea wameuza mmoja wa wachezaji wazuri zaidi Ulaya kutokana na kocha Jose Mourinho kutompa nafasi kwenye kikosi cha kwanza kwa kutoendana na aina ya soka anayoitaka.
Mata binafsi amefaidika maana alishaanza kuchanganyikiwa kwa kukosa kucheza mara kwa mara, na katika umri wake wa miaka 25 tu lilikuwa pigo. Kadhalika Mourinho alikuwa ametishia kutomuuza.
Huku Kombe la Dunia likikaribia nchini Brazil mwaka huu, mchezaji huyu wa kimataifa wa Spain alikuwa katika hatari ya kukosekana huko.
Lakini akiwa Man U bila shaka ataanza mechi nyingi akiwa fiti na hiyo ni faida kwa timu hiyo na pia kwa timu ya taifa ya Hispania kwani kijana wao atapata mazoezi ya kutosha.
Mata ni aina ya wachezaji ambao Moyes anawapenda kwa kuangalia tangu aanze kufundisha Preston na baadaye Everton – ni wachezaji wanaojituma hasa na wenye ubunifu uwanjani.
Akiingia United ataongeza nguvu hasa kutokana na kuumia kwa washambuliaji Robin van Persie na Wayne Rooney ambao wakipona watafanya kazi pamoja kwa kushirikiana na kinda Adnan Januzaj.
Mata ni mmoja wa wachezaji wanaotengeneza pasi nzuri za kufunga kwa hiyo atawasaidia United ambao wameshuka kutoka kufunga mabao 2.26 kwa mechi msimu uliopita hadi bao 1.64 msimu huu.
Moyes anaweza kufanikisha ndoto zake United baada ya usajili uliopita kufanikiwa kumsajili Marouane Fellaini pekee na ambaye bado hajasaidia sana timu na amekuwa pia majeruhi.
Je, kuingia kwa Mata kunaweza kumsababisha Rooney aliyebakisha miezi 18 kwenye mkataba wake kuondoka, na labda kujiunga na Chelsea ambao Mourinho amepata kumtaka? Ni vigumu lakini si kitu kisichowezekana.
Bado safari ni ndefu na Moyes anaendelea kujifunza mengi hapo Old Trafford ambapo viatu vya Fergie vinaonekana kuwa vikubwa kwake, walau kwa muda huu.
Chelsea wamefaidika kwa kupata mamilioni hayo ya pauni kwa sababu Mata alikuwa anakaa benchi tu tangu Mourinho aingie na labda watazitumia kumpata mchezaji mwingine kwa ajili ya mashindano ya ndani na ya kimataifa kama ambavyo wamekuwa wakimuwinda Mmisri Mohammed Salah anayekipiga Basel ya Uswisi.
Arsene Wenger wa Arsena tayari amesema si haki kumuuza Mata na anataka dirisha dogo la usajili lisiwepo kabisa, akisema Mata ameshachezea Chelsea na dhidi ya United na Arsenal ambapo amekuwa mwiba pia kwa The Gunners.
Kuja kwa Mata kunaweza kumwathiri Shinji Kagawa aliyesajiliwa na Fergie kutoka
Borussia Dortmund kwa pauni milioni 12 mwaka juzi akiwa na lengo la kuimarisha safu ya ushambuliaji.
Bado Moyes haonekani kuwa na imani sana na Kagawa na labda ataanza kumpumzisha zaidi kama si kumuuza au kumbadilisha na Marco Reus au Ilkay Gundogan. Bosi wa Dortmund, Jurgen Klopp bado anamhusudu Kagawa kwa hiyo huenda akamtaka arudi.
Credit: Tanzania Sports
No comments:
Post a Comment