Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mkuu wa Misheni ya Kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa katika DRC ( MONUSCO) Bw. Martin Kobler akiwasilisha mbele ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Usalama katika eneo la Mashariki ya Kongo na jukumu linalofanywa na MONUSCO katika utekelezaji wa mamlaka yake.
Na Mwandishi Maalum
Baraza Kuu la Usalama
la Umoja wa Mataifa, limeambiwa, kuna taarifa
za uhakika na zisizo na shaka
kuwa kundi la waasi la M23
limeanza kujiunda na kujipanga upya.
Hayo yameelezwa siku
ya jumatatu na Bw. Martin Kobler, Mwakilishi
wa Katibu Mkuu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mkuu wa Misheni ya
Kulinda Amani katika DRC, ( MONUSCO).
Alikuwa akiwasilisha
mbele ya Baraza Kuu la Usalama la
Umoja wa Mataifa, taarifa ya Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa kuhusu Misheni ya
Kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa katika DRC ( MONUSCO).
“Tunazo taarifa za uhakika kabisa kwamba kundi
hili la M23 baada ya kusambaratishwa vibaya mwezi Novemba mwaka jana, sasa
limeanza kujiunda na kujipanga upya” akasema Bw. Kobler
Na kuongeza, “ Ninapenda
kutumia nafasi hii, kuitaka Serikali ya DRC kuanza kutekeleza makubaliano ya Nairobi. Na kwa nchi za Uganda na Rwanda
kutoruhusu ardhi yao kutumiwa na kundi la M23 iwe ni kujipanga upya au kwa mafunzo ya aina yoyote ”.
Mbali ya Mkuu wa MONUSCO kutoa taarifa yake kwa Baraza
hilo, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu katika eneo la Maziwa Makuu, Bi. Mary
Robinson naye aliwasilisha taarifa yake.
Mkuu huyo wa Misheni
ya MONUSCO alieleza bayana kwamba makundi ya waasi katika Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo bado ni tishio kubwa katika mchakato mzima wa
utafutaji wa Amani ya kudumu katika DRC na hususani katika eneo la Mashariki ya
nchi hiyo.
“Uwepo wa Brigedi
Maalum ( FIB) na matumizi ya ndege zisizoendeshwa na binadamu ( UAVs), makundi yote ya waasi yanajua
wazi kwamba, sasa tuna nia na uwezo wa
kutumia nguvu kubwa wakati wowote”. Akasisitiza Mkuu huyo wa MONUSCO.
Katika taarifa yake kwa Baraza Kuu la Usalama, Bw. Kobler , alielezea
kwa kina hali ya usalama ilivyo
nchini DRC na kazi kubwa inayofanywa
na MONUSCO katika kuyakabili makundi ya
waasi na vilevile kutoa ulinzi kwa raia.
Bw. Kobler alibainisha zaidi kwa kusema kuwa,“
Katika wiki zijazo, tutakuwa tumekamilisha
mapitio ya mkao wa kijeshi katika
eneo lote la Mashariki ya Kongo. Baada
ya kukamilisha kazi hiyo tutakuwa
na urahisi wa kwenda mahali popote na
wakati wowote tunapohitajika,
kukabiliana na tishio la aina yoyote na
kutoa ulinzi kwa raia “
Naye Bi. Mary Robinson, Mjumbe Maalum wa Katibu
Mkuu katika eneo la Maziwa Makuu, akizungumza kwa njia ya video
tele-conferencing kutokea Kishansa DRC, ameliambia Baraza Kuu la Usalama, kwamba wakati umefika sasa kwa nchi
zile zilizotia saini Mpango Mpana wa Umoja wa Mataifa kuhusu Siasa, Usalama na Maendeleo katika DRC na Maziwa
Makuu kuanza kutekeleza maamuzi magumu.
Akasema juhudi za
kutafuta Amani na usalama katika
DRC zipo katika kipindi muhimu hivi sasa na kutoa wito kwa viongozi
waliosaini mpango huo kuanza kutelekeza ahadi zao ili hatimaye Amani iweze
kupatikana.
Bi. Robinson ambaye kesho ( Jumanne) atahudhuria mkutano wa Wakuu
wa Nchi za Maziwa Makuu ( ICGLR)utakaofanyika nchini Rwanda alieleza pia kwamba,
mazingira ya utulivu yaliyokuwapo
baada ya kusambaratishwa kundi la M23
yamepotea na kwamba eneo hilo sasa lipo
katika kipindi cha kurejea kwa
machafuko.
Akasema
utulivu huo umetoweka hasa baada
ya kutokea kwa mashambulizi yaliyofanywa
na kundi la waasi la Alliend Democratic Forces ( ADF) katika
eneo la Mashariki ya DRC.
Aidha kuendelea kwa hali ya machafuko katika Jamhuri ya
Afrika ya Kati na kuibuka kwa
mapigano katika Sudan ya Kusini,pia
kumechangia kuwepo mdororo huo wa kiusalama mashariki ya DRC.
Na kwa sababu hiyo
anasema, utekelezaji wa mpango mpana wa
kisiasa bado unabaki kuwa suluhu pekee
ya upatikanaji wa Amani ya kudumu, usalama, ushirikiano na
maendeleo katika eneo la Maziwa Makuu.

No comments:
Post a Comment