Mbwia unga anaitwa teja, kwa maana hiyo na wewe ambaye mapenzi yatakuingia kama bangi, jina linalokufaa ni teja wa mapenzi. Kwa maana kuwa yatakupumbaza nawe utapumbazika, siku ya kuachwa ndiyo utalia kwa kusaga meno. Usisahau kuhusu wale waliojiua!
Zingatia kuwa mapenzi yatakufanya uwe shujaa, mwenye furaha, matumaini, tena utaonekana mtu bora sana pale yanapokuendea chanya, kinyume chake utachekwa, utakosa furaha na matumaini, tena utaonekana wa ovyo kabisa.
Je, ni sahihi kwako kuonekana wa ovyo? Uchekwe na kugeuzwa mfano wa vijiweni wa watu walioangukia pua katika mapenzi? Bila shaka hutaki hayo yakutokee, kwa hiyo msingi utakaokubeba ni ndoto zenu. Jiulize, wewe na yeye mna ndoto wa kuwa pamoja?
Jiulize tena, wewe unaamini kwamba maisha yapo ndani yake na yeye anaamini wewe ndiye maisha yake? Ni mpenzi wa shida na raha au ni wa msimu wa mavuno pekee? Na majibu hayo utayapataje? Ipo kanuni muhimu kwa maisha yako ya kila siku.
TUMIA NA UIHESHIMU KANUNI HII
Ukipenda unaweza kuiita kanuni kiongozi, kwa maana kwamba ukiitumia katika maisha yako yote, itakusaidia kuvuka salama kwenye mazingira tofautitofauti. Inaitwa Tilia Shaka Kila Kitu (Doubt Everything)
Kama mapenzi hayatakuchukua kama madawa ya kulevya yanavyomlewesha teja, utaweza kuiheshimu kanuni hii. Kwamba hutakiwi kupenda tu, badala yake unatakiwa kuzipatia majibu pande zote kuzunguka mapenzi yenu.
Unatakiwa utilie shaka kila kitu ambacho mwenzi wako anacho. Vilevile wewe mwenyewe jitilie wasiwasi. Unatakiwa uwe na uhakika usio na chembe ya shaka kuhusu mapenzi yake juu yako. Nawe inakufaa ujiridhishe.
Isije ikatokea unamuona anakufaa leo kwa sababu hujaona wengine. Uchaguaji wa mwenzi wa maisha unakutaka ufikiri mara nyingi kabla ya kuamua. Kama jibu linafanana mara zote basi nenda mbele, ikiwa yanatofautiana hapo pia ni pa kutilia shaka.
Kama ni mwanaume jiulize, mwanamke wako unampenda akiwa kijana kabisa, mrembo, tena msichana mbichi, je akishakuwa ndani ukimzoea itakuwaje? Akishazaa utaendelea kuwa na mapenzi juu yake?
Mapenzi yenye sura ya maisha hayabadiliki baada ya kuoana na kuishi pamoja ndani ya nyumba, kwa kisingizio cha kuzoeana. Mapenzi sahihi hayapungui baada ya kuzaa. Badala yake hukua na kuchanua kwa maana hatua hizo ni kutimia kwa ndoto.
Ukiona mwenzi wako amepunguza mapenzi kwa sababu mpo karibukaribu muda mwingi, huyo ana walakini. Jitambue kwamba hukuwa wa ndoto zake. Ndiyo maana nasisitiza utilie shaka kila kitu chake mpaka utakapojiridhisha.
Itaendelea wiki ijayo...
GPL
No comments:
Post a Comment