MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amelishushia tuhuma nzito Baraza la Mawaziri, baada ya kudai baadhi ya mawaziri walioteuliwa hawana elimu ya kutosha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Profesa Lipumba alisema mmoja wa mawaziri hao ni Waziri wa Fedha, Saada Mkuya. Alisema chama chake, kina wasiwasi na elimu ya Waziri Mkuya, kutokana na wasifu wake kutoonyesha vyuo alivyosoma wakati wa kupata shahada ya kwanza na ya pili katika masuala ya biashara.
Alisema katika tovuti ya Bunge, wasifu wa waziri huyo umeonyesha sehemu aliyosoma elimu ya sekondari na kuhitimu kidato cha sita.
Alisema katika tovuti hiyo, haionyeshi chuo alichosoma shahada ya kwanza ya biashara, ingawa inaonyesha masomo aliyochukua jambo ambalo linatia mashaka uhalali wake kuongoza wizara hiyo nyeti.
“Ukiingia kwenye tovuti ya Bunge, utaona wasifu wake kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha sita na shule alizosoma, lakini kuanzia elimu ya shahada imeonyesha masomo aliyochukua na kupata shahada ya kwanza ya biashara, haionyeshi vyuo, jambo ambalo linatia mashaka,” alisema Lipumba.
Alisema nafasi aliyopewa inahitaji kiongozi mwenye upeo wa hali ya juu, kuweza kupambanua mambo yanayohusu uchumi wa nchi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kifedha za ndani na nje ya nchi.
“Napata wasiwasi kama Rais Jakaya Kikwete, aliangalia wasifu wa waziri wake kwa sababu asingeweza kumchagua kushika nafasi kubwa kama hii, wakati vyeti vyake vina mashaka,” aliongeza.
Alisema kitendo cha kumuweka mtu mwenye vyeti vya mashaka, kunaweza kusababisha nchi kuyumba kiuchumi, kuongezeka kwa deni la taifa, kwa sababu uamuzi wake unatokana na ufahamu wake.
Alisema kutokana na hali hiyo, uamuzi wa Serikali wa kuwaondoa mawaziri mizigo hautafanikiwa kwa sababu waziri huyo anaweza kuongeza mzigo mwingine kwa nchi.
“Mawaziri mizigo, wanaisababishia Serikali kuwa na viongozi mizigo, hivyo basi tunapaswa kuwa makini kwa kupinga kuongozwa na viongozi mizigo, kwa sababu wanaweza kutuletea matatizo,” alibainisha.
Akitolea mfano katika kipindi ambacho Waziri wa Fedha anapaswa kuwa makini na matumizi ya fedha za Serikali, ni pamoja na kuwepo kwa mchakato wa uboreshaji wa daftari la wapiga kura, mchakato wa Bunge maalumu la Katiba, vitambulisho vya uraia na mambo mengine ambayo kwa kiasi kikubwa yanahitaji fedha.
Alisema kutokana na hali hiyo, waziri huyo anapaswa kusimamia matumizi ya fedha katika shughuli mbalimbali zikiwemo za halmashauri na safari za Rais, ambapo katika kipindi hiki cha robo mwaka, safari zake za nje zimemaliza bajeti yake ya mwaka mzima.
Alisema kutokana na hali hiyo, Rais Kikwete alipaswa kumchagua mtu makini mwenye sifa stahiki kukalia nafasi hiyo, ili aweze kutimiza majukumu yake kwa kufuata taratibu za kisheria.
Alisema chama hicho hakina mashaka na uteuzi wake, lakini wana mashaka na chuo alichosoma na kupata shahada ya kwanza na ya pili.
WAZIRI AJIBU
Akizungumza na MTANZANIA Jumatatu kuhusu madai hayo, Waziri Mkuya alisema elimu yake wala haina mashaka, kwani alisoma kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Lumumba mjini Zanzibar.
Baada ya hapo, alijiunga na masomo ya diploma ya Biashara katika Chuo cha Stamford cha Malaysia, ambapo pia alichukua diploma nyingine ya biashara nchini Uingereza. Alisema mbali na masomo hayo, pia amesoma shahada ya pili ya biashara katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na kuhitimu mwaka 2009.
“Nimehitimu Shahada ya Uzamili ya Utawala na Biashara (MBA) ya Chuo Kikuu cha WATT kilichopo Edinburgh, Scotland. “Kwa sasa nachukua Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Utawala wa Biashara Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, tawi la Dar es Salaam,” alisema Mkuya.
Source: Mtanzania JUMATATU, JANUARI 27, 2014
5 comments:
Asante sana mh. Lipumba. Inaonyesha wazi jinsi Raisi wa nchi anavyokurupuka na kutokusoma au kupokea uhalali wa elimu ya mtu muhimu kama huyo wa kuiongoza wizara nyeti ya fedha. Hatutafika mbali huu ni ukipuaji wa nchi yetu wenyewe. Nchi inakoelekea ni kubaya lakini tunalifumbia macho! je? ni viongozi wangapi na wabunge wanadhiriki kukubali uteuzi huo hata kama alikuwa naibu lakini wasifu wake unadanganya toto! Hili ni suala zito linalosimamia fedha za nchi na mabenki lukuki! Acha waendelee kuimega hadi nukta ya mwisho!! TUMEKWISH.
asante simba wetu professor lipumba wewe kweli ni mtetizi wa wanyonge tanzania na tena ni msomi wa uchumi na unayejua mahesabu vizuri saana big up man tungekuwa na watu wenye vichwa kama ishirini kama wewe tanzania yetu ingekuwa njema sana lakini wapi arjojooooooo ndombole kila leo
Mkianza uchambuzi huo mbona mtakamata wengi katika hilo baraza
Hao ndio Vihio ahsante Limpumba hana elimu huyo ndio hivyo tena kupeana madaraka tu dakika za lala salama hivo kwa Kikwete
Its true kitu Lipumba anachosema, na wote tunaona hilo, Mimi nadhani hawa mawaziri au mawaziri wote kwa ujumla walikua wapendekezwe na raisi lakini walitakiwa wote wapelekwe bungeni na experiences zao zichunguzwe vizuri pamoja na vyeti vyao waliokua navyo pia vichunguzwe, kuna mawaziri wengi Tanzania unasikia ni Dr. lakini wapi alipata hizo nyazifa za u Doctor? hazijulikani, mtu anatoka kua na diploma in 6-12 month amekua Dr au ana masters zisizoeleweka, au hata bado anasoma, nashindwa kuelewa. watu wanabuma vyeti, hawana elimu ya kutosha wala experience ya kuambatanisha nyazifa zoa, waziri wa fedha, ni jukumu kubwa sana la taifa,Kiini cha uchumi wa Tanzania , personally nadhani sio kitu chakupeana kiholela,
Also kuna watu wengi tu wamesoma Tanzania lakini kama Raisi, au chama hakikuungi mkono, you pretty much do not have any chance.
For example, kama mnafahamu marehemu Siraju Juma Kaboyonga( mungu amlaze mahali pema) he was one of the smartest economist mtanzanian , i could not understand a person like him with experience and education he had, could have not make it to be a governor wa bank ya Tanzania au economic adviser wa president or something, lakini vichwa mchungu kibao wanakua na huge post ambazo hawawezi hat kuexplain what is an inflation.
Bongo yetu, Kikwete anatupiga mchanga wa macho, siku zinaenda..
Post a Comment