Picha nikielelezo cha stori yenyewe sio shabiki
Kuna hayawani mmoja alikwenda kuharibu ukweni bila kuelewa. Kakutana na Baba mkwe, akaanza kumsifia mshenga wake kwa jinsi alivyofanikisha ndoa yake. Alianzia pale alivyompa mshenga rupia za kumlainisha mtoto wa watu, kisha rupia za kuondolea udhia kwa wakwe.
Bwege huyo alimalizia kwa kumsifu mshenga kwa kujaliwa uwezo wa hali ya juu wa kupangilia na kutoa maneno (art of talking) ya kumrubuni baba mkwe.
Baba akaona Lah! Hawa wamempata binti yangu kwa staili ya mahindi ya njano! Wengi mlikuwa wadogo wakati huo. Baba zetu walikuwa na akili sana. Sisi tulipokuwa na njaa walikwenda hotelini kuchukua “chakula cha mbwa”. Lakini hakikuwa cha mbwa, bali kilikuwa ni cha walaji wa hotelini. Alichotewa chakula kilichobaki katika sufuria moja kati ya nne zilizopikwa siku hiyo, basi tukakiita “chakula cha mbwa
”.
Basi mzee mwenye akili aliwatazama wanawe waliofunga mikanda hadi wakatishia kuvikata viuno vyao. Akafikiriiiii, akaona hana jinsi ila kuomba msaada. Mmoja kati ya rafiki zake wenye uwezo alilima mahindi ya njano. Njano kabisa; mdogo wangu shabiki wa Simba aliyagomea. (Chukua tahadhari, hadithi hii ni tafsiri yangu tu, sikuwa shuhuda wa haya.
Mzee akamwendea yule mkulima. Akamwambia: “Sisi tunakula ugali mweupe. Nyinyi mnakula wa njano?” Huyu rafiki kwa kutotaka kujishusha hadhi akaruka: “Aaaah! Hebu nitake radhi. Haya mahindi ni kwa ajili ya ng’ombe wangu tu.” Mzee wetu akamwambia “kumbe ndiyo maana ng’ombe wako wana afya njema hivi? Nipatie na mimi nikawape wa kwangu.” Akapata tani kwa tani, nasi tukanusurika kufa kwa njaa. Turudi kwa baba mkwe. Alikumbuka jinsi alivyoelimishwa juu ya utunzaji wa familia. Halafu akakiri kimoyomoyo kuwa watoto wa mjini wamemtia changa la macho. Alipigwa hekaya za Karubandika hadi akamtoa bintiye akaolewe na tapeli. Kwa kweli alichukia sana, akasema “sina radhi na ndoa hii”. Naye binti akasema “na mimi siko radhi kuendelea na ndoa aliyoiharamisha baba.”
Hawa wajinga walilaumiana sana. Yaani mume (hapa tumwite tapeli) na mshenga (yeye tutamwita dalali). Dalali akasema “wewe umenikosea kwa kunitia sifa za kijinga” na mwenzie akalalamika kwa nini hakuelezwa kuwa anaingizwa kwenye familia inayojielewa (extended). Yote kwa yote ikawa imekula kwao.
Si siku nyingi sana zilizopita nilitazama kipindi TV cha Mikasi (oooh sorry ulimi hauna uti wa mgongo, ni kipindi cha Mkasi). Mgeni wa siku hiyo alikuwa Manju wa Muziki nchini, Massoud Massoud. Alisikitishwa sana na baadhi ya waandaaji au waendesha vipindi ambao hutumia muda mrefu kuwatangaza wadhamini badala ya kutangaza walichokusudia kwa siku hiyo.
Ingawaje yeye (Manju) aliainisha kuwa matangazo huenda ikawa ni sera ya kituo cha utangazaji, mimi bado naona mapungufu mengine hata ndani ya sera hizo. Huenda nikawa na tatizo na wote: watangazaji na hata wamiliki. Mmiliki wa kituo ana uwezo wa kukubali au kukataa kurusha kipindi kutokana na maudhui yaliyo katika kipindi hicho, ndiyo maana kipindi kikitukana anahojiwa Mhariri.
Bila shaka kila mmoja anaelewa kuwa yapo matangazo yenye mfumo wa vipindi. Mtu anatengeneza kipindi na kukilipia kiende hewani. Lakini haina maana mtangazaji wa kipindi hicho kupata nafasi ya kutumia muda mrefu kurudiarudia majina ya wapambe. Anaanzwa mkewe aliyempikia chai, dereva aliyempa lifti hadi jirani anayemtazama wakati huo.
Kisha anakumbukwa mshkaji aliyemnunulia bia jana, mchizi aliyemnyoa pale saluni, nyumba ndogo inayotarajiwa kutembelewa usiku na mambo kemkem yasiyo na tija kwa watazamaji. Bila kumsahau Massawe aliyempigia kiwi na yule aliyemfagilia wakati anasubiri viatu ving’are.
Hapo mama ntilie anayetarajia kumkopesha chakula ataacha kudai kufagiliwa? Ana wangapi waliomfanikisha yeye kuwapo pale siku hiyo? Kwanza Mungu, baba na mama yake, mkunga wa Hospitali aliyozaliwa, walimu wake wa chekechea, msingi na sekondari… Ajabu mambo haya hujitokeza hapa kwetu tu.
Ipo filamu iliyowahi kuutikisa ulimwengu ikiitwa Apocalypto. Iliandaliwa na Mel Gibson chini ya watendaji ambao sina uhakika wa idadi yao. Naamini iwapo Mel angekamata kipaza na kuanza kumtaja mmojammoja, kusingelikuwa na muda wa kuonesha japo utangulizi wa filamu hiyo.
Kwa bahati nzuri wao wanakuachia utazame uhondo kamili wa kilichotengenezwa, kisha unaletewa orodha ndefu kabisa ya maandishi kuonyesha kila aliyeshiriki kufanikisha kazi hiyo, yaani haki shiriki (hadi aliyebeba waya). Utagundua kuwa maandishi ni mengi kuliko matajo, za kwetu matajo ni mengi kuliko maandishi.
Ni lazima tujue kuwa mapenzi na ulevi vina uzito sawa. Shabiki mmoja wa Msondo alikiri hadharani kuuza koti lake la harusi ili asikose onyesho la bendi hiyo. Namfahamu pia shabiki wa Simba aliyetembea uchi huku akimwaga machozi baada ya timu yake kuchapwa na Stella pale Uwanja wa Taifa. Hivyo hata mashabiki wa vipindi wanapata taabu sana wanapokutana na vipindi vibovu. Kama mtu anaweza kunywa pombe hadi kufa, na kijana kupenda hadi akajinyonga, basi shabiki wa kipindi ni vivyo hivyo yanaweza kumkuta.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment