ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 7, 2014

Uandikishaji Darasa la Kwanza utata mtupu

Dar/Moro/Mbeya. Msimu wa uandikishaji watoto wanaoanza darasa la kwanza, umeanza, huku kukiwa na malalamiko lukuki hasa kutokana na michango inayotozwa kwa watoto wanaokwenda kuanza darasa la kwanza.
Itakumbukwa, Novemba 7, 2012, Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu, Majaliwa Kassim Majaliwa alisema bungeni mjini Dodoma kuwa ni kosa kwa walimu wakuu kutoza fedha kwa watoto wanaoanza darasa la kwanza na atakayefanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Majaliwa alikuwa akibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, alisema kama ni michango ni ile iliyokubaliwa na wazazi wenyewe, Kamati za Shule lakini pia na kupata baraka za mamlaka husika za elimu katika Halmashauri au Wilaya.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Serikali, inaonekana kupigwa kumbo huku wazazi wakishangaa michango hiyo, ambayo mingine haieleweki na mingine ilikubalika kupitia kamati za shule.
Tozo la kujiandikisha:
Wazazi wa watoto waliokwenda kujiandikisha katika Shule ya Msingi Kivule wameulalamikia uongozi wa shule hiyo kuwachagisha kiasi cha Sh40,000 kwa ajili ya watoto wanaojiunga darasa la kwanza jambo lililosababisha watoto kushindwa kujiunga.
Malalamiko kama hayo ambayo yako kwenye shule mbalimbali, pia yaliibuka katika Shule ya Msingi Mtoni, Dar es Salaam kwa wazazi kulalamikia kutozwa Sh33,500 wakati mjini Morogoro katika Shule ya Msingi Kambarage iliyopo Kata ya Chamwino katika Manispaa ya Morogoro michango ilifikia Sh50,000 kwa kila mzazi.
Katika Shule ya Msingi Kivule, Dar es Salaam, wazazi wameulalamikia uongozi kukataa kuwaandikisha watoto na wazazi kulazimishwa kutoa Sh40,000 ndipo watoto wao waandikishwe kuanza darasa la kwanza mwaka huu.
Mwandishi wa habari hizi alipomtafuta Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Wilson Muhemba, alikana madai hayo na kusema anachoelewa yeye ni mchango wa Sh15,000 kwa ajili ya kujenga madarasa ya shule mpya ambayo ilipitishwa kwenye kikao cha wazazi.
Mmoja wa wazazi aliyejitambulisha; Rozi Mwing’a alisema alifika shuleni hapo kwa ajili ya kuwaandikisha watoto wake wawili aliambiwa atoe mchango wa Sh40,000 kwa kila mtoto hivyo imesababishia kushindwa kuwaandikisha watoto hao.
Alisema wanachangia michango wa ujenzi wa shule Sh15,000, mchango wa fulana Sh6,000, mchango wa mafunzo ya awali Sh6,000, nembo Sh1,000 na ulinzi ni Sh5,000.
Mwing’a alisema mchango mwingine wa fomu Sh5,000, kupima uzito Sh1,000, picha za pasipoti Sh3000 na mchango wa madaftari saba Sh1,500.
“Tumeshangazwa kuona tunachangishwa Sh15,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa wakati madarasa yameshajengwa, mimi naona huu ni mradi wa walimu na kamati na bodi ya shule,” alisema Mwing’a.
Mzazi mwingine, Silvester Chacha alisema hiyo michango wanayochangishwa hawakuwahi kukaa kikao chochote kwa watoto watakaojiunga darasa la kwanza.
Alisema mwanaye amerudishwa nyumbani hadi hapo atakapopata kiasi cha Sh 25,000 ili kufikia kiwango cha kiasi walichopanga walimu hao.
Walimu wajitetea kwa michango:
Mwalimu Mkuu Msaidizi Muhemba alisema yeye anachojua ni mchango wa ujenzi wa shule mpya na vyoo ambayo ni Sh15,000 iliyopitishwa kwenye kikao cha wazazi walichokaa mwishoni mwa mwaka jana.
“Hiyo michango mingine mimi siifahamu wala mchanganuo wake siuelewi hivyo anayeelewa ni mwalimu mkuu wa shule.
“Inaonekana hawa wazazi wameunganisha na michango ya kununulia fulana na hela ya mafunzo ya awali ambayo tulikubaliana na wazazi ni hiari Sh6,000, mchango wa nembo ya shati, madaftari na hela ya picha ambazo hizo ni lazima watoe wazazi hawakutakiwa kuchanganya na Sh15,000 ya jengo ambayo ilikubaliwa na wazazi wenyewe.”
Alisema na suala la watoto kurudishwa haijawahi kutokea katika shule hiyo. Kama mzazi hana fedha ya kumwandikisha anaruhusiwa kumwandikisha lakini baadaye analipa fedha hizo kwa utaratibu utakaowekwa.
Kwa upande mwingine, wazazi waliofika kuandikisha watoto kwa ajili ya kuanza daraza la kwanza katika Shule ya Msingi Mtoni wamelalamikia kutozwa Sh33,500 lakini Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Omar Kitwana amekataa kutoa ufafanuzi kuhusu mchanganuo wa fedha hizo.
Mmoja wa wazazi hao, Subira Ali alisema wameambiwa ada ya kuandikisha mtoto kuanza darasa la kwanza ni Sh33,500. Tumeambiwa fedha hizi ni kwa ajili ya madawati, lebo, fulana na mlinzi, kwa umaskini huu tunashindwa kuandikisha watoto ili kusoma elimu ya msingi,” alisema Subira aliyeondoka na mtoto, June Hassan bila ya kumwandikisha.
Mwalimu Kitwana mbali na kukataa kutoa ufafanuzi wa zoezi la uandikishaji, pia alikataa wanafunzi walioanza darasa la kwanza wasipigwe picha.

Katika Shule ya Msingi ya Bokoramu ya Temeke, wazazi wanaandikisha watoto kwa Sh35,000 ili kuanza darasa la kwanza.
“Nimetoka kulipia ada hiyo ya usajili, lakini inasikitisha kwamba licha ya fedha nyingi ambazo wazazi wamekuwa wakitoa lakini watoto wamekuwa wakisoma wakiwa wamekaa sakafuni,” alisema.
Alitaka Serikali kuweka viwango vya ada ya uandikishaji vinavyofanana tofauti na ilivyo sasa kila shule kutoza kiwango chake kwa kisingizio cha Kamati za Shule na Wazazi.
Wakati wazazi wakilalamikia hayo, baadhi ya Wakuu wa Shule za Msingi, wametoa ufafanuzi wa madai yanayotolewa na wazazi kuhusu malipo ya michango ya shule kwa watoto wao wakati wa kujiandikisha wakisema agizo hilo ni la Serikali.
Akizungumza jana na mwandishi wa gazeti hili, mmoja kati ya wakuu hao ambaye aliomba kutotajwa jina na shule anayofundisha kwa madai ya usalama wa ajira yake, alisema mwaka jana Wizara ya Elimu ilitoa agizo hilo kwa Halmashauri zote nchini.
“Kwa hapa Dar es Salaam, kila shule iliitisha vikao na wazazi, mimi kwa hapa shuleni kwangu tuliainisha mahitaji kadhaa yanayotakiwa kuchangiwa na mzazi na jumla ya mahitaji yote ilifikia gharama ya sh 16,000 kwa mahitaji ya sare ya shule (fulana), kulipia mitihani, mchango wa dawati na uji,” alisema na kuongeza:
“Baada ya hapo tukawashirikisha wazazi kwenye vikao vyetu mbalimbali na kukubaliana ila wanaolalamika ama ni wageni au hawakufika kwenye mikutano ya kuweka utaratibu wa maendeleo ya shule na hawaelewi kama kuna makubaliano ambayo hufanyika kwenye vikao vya wazazi.”
Aidha, aliongeza kuwa gharama hizo hazichukuliwi kama malipo ya ada kwa mwanafunzi anayesajiliwa kujiunga na darasa la kwanza. “Kwa hivyo ni suala la uelewa tu kwa wazazi na wala hakuna utapeli unaofanyika,” alisema mkuu huyo.
Serikali Dar yatoa ufafanuzi:
Akitoa ufafanuzi mbele ya wazazi hao, Ofisa Taaluma Mkoa wa Dar es Salaam, Kiduma Mageni alisema hakuna shule yoyote inayoruhusiwa kutoza pesa kama malipo ya kusajili mwanafunzi anayeingia darasa la kwanza.
Mageni alisema pamoja na kuwepo kwa makubaliano ya michango hiyo, bado haiwezi kuwa kikwazo kwa mwanafunzi asipate haki ya kuandikishwa kuanza shule.
“Ni marufuku na hairuhusiwi michango hiyo. Kwanza ni lazima mtoto aandikishwe kisha iangaliwe namna ya mzazi kumudu gharama hizo kwani uwezo wa wazazi unatofautiani
M wingine hata Sh10,000 tu hana kuilipa kwa mwaka halafu umpe michango ya Sh30,000 au zaidi atawezaje,” alisema Mageni kwa kauli ya kuchukizwa.
Mjini Morogoro, wazazi wenye watoto wanaoanza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kambarage iliyopo Kata ya Chamwino katika Manispaa ya Morogoro jana walipigana ngumi na bakora kutokana na kubishania ulipwaji wa mchango wa Sh50,000 kwa kila mzazi.
Vurumai hiyo ilitokea mbele ya Mbunge wa Morogoro Mjini, Abdullah Aziz Abood aliyekuwa katika ziara ya kutembelea shule za msingi na sekondari katika jimbo lake ili kujionea uandikishaji wa watoto unavyofanyika.
Wazazi wa watoto ambao walikuwa hawajalipa mchango huo, walikuwa wamejikusanya shuleni hapo.
Mmoja wa wazazi, Hamad Hassan alikiri wazazi kukubaliana michango hiyo kutokana na kikao cha Novemba mwaka jana.
Imeandikwa na Raymond Kaminyonge, Pamela Chilongola, Dar, Lilian Lucas, Moro na Mussa Mwangoka, Mbeya.
Mwananchi

No comments: