ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 28, 2014

USILAZIMISHE MSICHANA WA KAZI AWE MKE MWENZIO

Haya haya kama kawa kama dawa tumekutana tena kwenye kona yangu mimi Anaa Orijinali wengine magumashi. Sitakuwa muungwana kutowajulia hali wapenzi wa kona hii mi’ Naa mzima wa afya njema kama ilivyo ada tumekutana tena siku ya Jumatano ambayo najua mliisubiri kwa hamu.

Leo nilitaka tukumbushane jambo moja muhimu ambalo huenda tumejisahau na kushindwa kuelewa tunatengeneza bomu ndani.

Nilitaka tukumbushane majukumu ya ndani ya nyumba ya msichana wa kazi ni yapi na mipaka yake ni ipi. Ni kweli wengine tumekuwa bize na kazi za kuajiriwa au kujiajiri lakini tunasahau kuna majukumu mengine ya nyumbani na hutakiwi msichana wa kazi kuyafanya.

Wengi tumekuwa tukijisahau na kuamini jukumu lako muhimu katika nyumba yako ni kukidhi hamu za mumeo na kusahau kuna mambo ambayo msichana wa kazi anatakiwa kutoyagusa kabisa bali wewe mwenyewe.

Suala la kutandika kitanda chako, usafi wa chumba chako, kumuandalia mumeo chakula au maji ya kuoga si la msichana wa kazi bali lako. Nataka kuwaeleza kitu kimoja wapenzi wangu. Mahaba ndani ya nyumba hayaongezwi na kitanda tu bali kuna vitu vingi ambavyo mwanaume huvikosa sehemu nyingine na kupatikana nyumbani tu. Nataka kukueleza kitu kimoja kitanda peke yake hakilei nyumba.

Kama sukari ya mwili hata kina dada poa wanatoa lakini mahaba ya kumjali mumeo ni ndani tu. Mahaba hayo yanapatikana katika sehemu nyingi kama kumpokea mumeo akitoka kazini. Kuoga na kula pamoja, vitu hivi ndivyo unatakiwa kumfanyia mumeo si msichana wa kazi.

Lakini siku hizi katika vitu nilivyovisema ni kimoja tu hakifanyi msichana wa kazi cha kuoga pamoja lakini vyote msichana wa kazi anavifanya. Kama msichana wa kazi atamsubiri mumeo amejifunga upande wa khanga na Mungu kamjalia maumbile tata lazima akamilishe mzunguko kwa kufanya mambo yote ya kushea mume na kuoga pamoja wewe unabakia mke jina. Mke anayemhudumia mumeo ni msichana wa kazi.

Sisemi mtafute wasichana wa kazi wasio na sifa bali kumpangia majukumu kuhakikisha haingiii upande wa pili. Ni kosa kumpa msichana wa kazi majukumu yako kwa kisingizio upo bize, kwa kufanya hivyo unakuwa unalazimisha msichana wa kazi kuwa mke mwenzio tena mwenye heshima ndani ya nyumba kuliko wewe. Unamjali mumeo kitandani, pengine kutokana na uchovu bila kukugusa wewe huna hamu naye. Kama ndo kishaanzisha uhusiano na msichana wa kazi basi kila siku anajinafasi.

Mwisho wa siku talaka inakuita hujui tatizo kwa kuamini kitanda pekee kinalea ndoa.
Mfanye mumeo rafiki, kuwa karibu yake muda wote mpokee akirudi kazini kama nawe mfanyakazi basi hakikisha maji ya kuoga unamuandalia, ogeni pamoja ili kuyafanya macho yafaidi umbile lako na kujenga hisia ili mkifika ‘uwanjani’ hamu iwe juu, lazima chakula kitakuwa kitamu kwa sababu ukiwa na hamu lazima atakiona kitamu.

Siku za mapumziko itumie kumuandalia mumeo chakula ili aone tofauti ya msichana wa kazi na mkewe, utamu wa chakula nao unaongeza mahaba na kumfanya mumeo atamani kurudi nyumbani kula chakula cha mkewe. Msichana wa kazi maeneo yake ni kufanya usafi wa nyumba mwisho nje ya chumba chako harusiwi kuingia chumbani kwako.

Chakula kula na mumeo, bafuni oga naye hata kama umeoga, kila kinachomuhusu mumeo kifanye wewe. Kumuachia msichana wa kazi ni kulazimisha awe mke mwenza na mwisho talaka hiyoo. Kama anajua kupika anamtengea chakula na kusubiri atoe vyombo.

Amtengee maji ya kuoga mumeo akishawishika kamgeuza nyumba ndogo wewe hapo una nini? Amka shoga kijua ndicho hiki.

Yangu nimeyatoa kazi kwako, ni mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu.

GPL

1 comment:

Anonymous said...

Ushauri mzuri. Nadhani kinachofuata ni kuwaeleza jinsi ya kuorganize maisha yao ili wafanye baadhi ya vitu ulivyoshauri. Kwa mfano hili la kutandika kitanda nadhani ni vyema utandike mara baada ya kuamka ili utandikaji usiingiliane na matayarisho yako ya kwenda kazini. Tayarisha nguo unayotaka kuvaa asubuhi usiku uli usianze kurusha nguo kitandani nk.
Ni kazi ngumu kwa sababu huwa tumechoka sana jioni turudipo vibaruani lakini jitahidini ndugu zangu.

Msaidizi wa shangingi mstaafu.