ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 28, 2014

Mbowe apaisha homa serikali 3

Helkopta iliyobeba viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ikitua katika uwanja wa mikutano wa Uhuru mjini Bukoba kwa ajili ya kuhutubia mkutano wa hadhara.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema iwapo kutakuwa na uchakachuaji wa rasimu ya Katiba mpya na kuondoa mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya mfumo wa serikali tatu, chama hicho hakitakubali na hatua madhubuti zitachukuliwa.

Mbowe aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa hadhara wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa Biharamulo mkoani Kagera na Chato, mkoani Geita.

Alisema katika Bunge Maalum la Katiba, vyama vya upinzani na wengine wanaounga mkono mfumo wa serikali tatu katika Bunge hilo ni wachache, lakini hawatakuwa tayari kukubali wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao ni wengi wakijaribu kuvuruga.

“ Kama noma na iwe noma, Chadema haitakubali wabunge wa CCM kupindisha na kukataa kupitisha serikali tatu, tuko tayari kwa lolote iwe kupigana ngumi na mieleka kuhakikisha kinaeleweka kuhusu serikali tatu,” alisisitiza Mbowe.

Alisema wananchi wengi wameonyesha kutaka serikali tatu, lakini wachache ambao ni CCM wanapinga na kwamba Chadema haitawaangusha wananchi bali itawatetea kuhakikisha wanachokitaka kinafanikiwa.

Mbowe alisema Katiba ni uhai wa Watanzania, hivyo ni bora siasa zikawekwa kando na kutanguliza uhai wa wananchi.

Mbowe alisema katiba za vyama zipo kwa ajili ya vyama vyenyewe, lakini Katiba ya nchi ni kwa ajili ya Watanzania wote, hivyo inapaswa kuheshimiwa.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa kama wanataka nchi itamalaki, ni vyema wakaheshimu maoni ya wananchi wengi ya kuwapo kwa serikali tatu.

Alisema Chadema inataka Katiba inayotengenezwa sasa iondoe makovu ya muda mrefu ambayo yaliwaumiza Watanzania.

Kwa mujibu wa Mbowe, zipo taarifa kuwa CCM wameanza kukaa vikao vya kukataa rasimu ya Katiba kwa sababu hawataki serikali tatu zilizopendekezwa na kwenye rasimu hiyo na kusisitiza kwamba jambo hilo halitakubalika bali watapambana ili njama hiyo isifanikiwe.

Mbowe anaendelea na ziara yake na leo anatarajia kufanya mikutano mbalimbali mkoani Iringa.

SLAA: VIJANA JIANDIKISHENI
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, akizungumza jana mjini iringa, aliwataka vijana kuhakikisha wanajiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura.

Akiwahutubia wananchi katika viwanja vya Mwembetogwa, Dk. Slaa pia aliwataka vijana nchini kuachana na propaganda ambazo hazina maana yoyote kwao.

Sambamba na hilo, aliwatahadharisha Watanzania kuwa kwa sasa nchi inaingia kwenye deni la Sh. trilioni 25 huku wananchi wakililipa taratibu bila wao kujua na kuhoji kuwa deni hilo limetokana na nini.

Alisema mwishowe wananchi ndiyo watakaoumia kwa kukatwa kupitia kodi.

LISSU ALIA NA WASALITI
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Chadema ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, akiwahutubia wakazi wa mjini Dodoma katika viwanja vya Barafu jana, alisema hawataacha kuwashughulikia wale wote watakaobainika kukihujumu chama hicho.

Naye Mwenyekiti cha Baraza la Vijana la Chadema Taifa (Bavicha), John Heche, ambaye aliambatana na Lissu katika ziara hiyo, alisema ni lazima daftari la kudumu la wapigakura lirekebishwe kwani hadi sasa kwa mujibu wa sensa ya baraza hilo, takribani vijana milioni 5.5 nchini kote hawajajiandikisha kwenye daftari hilo.

Imeandikwa na Elizabeth Zaya, Biharamulo; Agusta Njoji, Dodoma na George Tarimo, Iringa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: