Baadhi
ya madini ya Tanzanite ambayo yanapatikana katika mabanda mbalimbali
katika maonesho ya 53 ya Kimataifa ya Bangkok Gems and Jewelry Fair.
Mfanyabiashara wa
madini na Afisa Masoko wa Kampuni ya Tom Gems Tanzania, akimwonesha
mgeni aliyefika katika banda la Tanzania kuona madini ghafi ya Tanzanite yanayozalishwa Tanzania pekee. Wageni wengi wamefika katika banda hilo kuona Tanzanite halisi kutoka Tanzania.
Mwenyekiti
wa Madini ya Viwandani Bw. Kassim Iddi Pazi, akimwonesha mgeni madini
ya Ruby. Kutokana na maelezo ya Bw. Pazi, ameeleza kuwa, madini hayo
yametoka katika maeneo ya Winza Dodoma na Matombo Morogoro.
Mfanyabiashara
wa Madini kutoka Kampuni ya Tom Gems Bw.Benjamin Mtalemwa akimwonesha
mgeni madini mbalimbali alipotembelea banda la Tanzania. Wanaoshuhudia
kutoka kulia ni Mthamini wa Madini kutoka Wizara ya Nishati na Madini
Bw. Edward Rweymamu, Wa pili kulia ni Afisa Madini kutoka Shirika la
Madini Tanzania (STAMICO). Bw. Peter Maha, na wa kwanza kulia ni Afisa
toka Wizarani Bibi. Margareth Muhony.
====================
Na Asteria Muhozya, Bangkok
Madini
ya Tanzanite yamekuwa kivutio kikubwa katika maonesho ya 53 ya
Kimataifa ya‘’Bangkok Gems and Jewelry Fair’’, yanayoendelea katika eneo
la kibiashara la ‘Impact Challenger’, jijini Bangkok.
Madini
ya Tanzanite yanayozalishwa nchini Tanzania pekee duniani, yamekuwa
kivutio kikubwa kwa wageni wanaotembelea maonesho hayo ikiwemo
wauzaji, wanunuzi na wafanyabiashara ambao wamefika katika banda la
Tanzania kutaka kuona Tanzanite halisi kutoka Tanzania.
Aidha,
pamoja na kwamba madini ya Tanzanite yanazalishwa na Tanzania pekee,
lakini katika maonesho hayo ya Bangkok, madini hayo yanapatikana kwa
kiasi kikubwa katika mabanda ya washiriki kutoka nchi mbalimbali
duniani jambo ambalo linaonesha namna madini hayo yalivyo na muhimu
katika sekta za kibiashara na kiuchumi.
Akizungumzia
suala la uwepo wa madini ya Tanzanite kwa kiasi kikubwa katika soko la
kimataifa, na katika maonesho hayo, Kamishna Msaidizi wa Madini ,
Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Hamis Komba, ameeleza kuwa, uwepo
wa Tanzanite katika soko la kimataifa unaashiria mahitaji makubwa ya
madini hayo duniani na umuhimu wake katika kuchangia ukuaji wa uchumi
wa Tanzania, na nchi nyinginezo ikiwemo thamani yake katika soko la
kimataifa na upekee wake.
Aidha, ,
aliongeza kuwa, hiyo ni changamoto katika uthibiti wa madini hayo
katika soko la kimataifa kutokana na uwiano wa takwimu za kiasi cha
madini kinachotoka kwa kufuata taratibu za usafirishaji madini hayo nje
ya nchi na uwingi halisi unaoonekana katika soko la Kimataifa.
“Uwiano
wa takwimu za uzalishaji Tanzania na idadi halisi ya madini iliyopo
katika maonesho ya kimataifa ni tofauti. Hii ni changamoto katika
udhibiti wa madini haya” Amesema Kamishna Komba.
Hivyo,
ameongeza kuwa, Serikali inalifanyia kazi suala hili kwa lengo la
kufanikisha usimamizi na biashara endelevu ya madini ya Vito na usonara.
Mbali
na madini ya Tanzanite kuwa kivutio, katika banda la Tanzania, vinyago
vinavyotengenezwa kutokana na mawe aina ya Zoisite, Basalt,
Limestone, Travertine, Granite na White marbale yanayopatikana Tanzania
ambayo yametengenezwa mapambo mbalimbali ya majumbani yamekuwa kivutio
kikubwa katika maonesho hayo kwa wageni waliotembelea banda la Tanzania
kutoka nchi za Ulaya na Asia, akiwemo pia Rais wa Shirikisho la
wafanyabiashara wa vito na usonara Bw. Somchai Phornchindarak, ambaye
pia alitembelea Banda la Tanzania na kuonesha kuvutiwa na kushangazwa na
mapambo hayo.
Akizungumzia
kuhusu ushiriki wake katika maonesho hayo, Mratibu wa kituo cha
Tanzania Geomological Center, Bw. Musa Shanyangi, amesema kuwa, maonesho
hayo yamekuwa ya manufaa katika soko la madini ya mawe kutokana na
wageni wengi kuonesha kuvutiwa nayo.
Shanyangi, ameongeza
kuwa, tayari kituo hicho kimeanza kufanya ukarabati wa miundombinu na
kuandaa mitaala ya kufundishia , hivyo chuo kitaanza kutoa mafunzo ya
uchongaji wa vinyago, ukataji wa madini ya vito, uchongaji wa mawe,
mafunzo ya utambuzi wa madini ikiwemo pia maabara itakayotumiwa kwa
ajili ya shughuli hizo.
Hivyo,
amewataka vijana wa kitanzania kuitumia fursa hiyo kupata mafunzo hayo
ili waweze kuingia katika sekta ya madini kwa kuwa itawasiadia
kujiajiri, kuinua vipato vyao na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.
Aidha, amewataka wadau katika sekta ya madini kuona umuhimu wa kuongeza
thamani ya madini.
“
Maonenesho hayo, yamekuwa na manufaa kwa Tanzania, kituo chetu
kimepata fursa ya kufaa kwa bidhaa za mawe, kwasababu nimejaribu
kuzunguka katika mabanda mengi sana sijaona bidhaa kama hizi. Hiyo ni
fursa kwetu na kwa vijana wa Tanzania katika soko hili. Amesema
Shanyangi.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Madini ya Viwanda Tanzania (FEMATA), Bw.
Kassim Iddi Pazi akielezea ushiriki wake katika maonesho hayo na soko
la madini kimataifa ameeleza kuwa, maonesho hayo yamefungua fursa kubwa
ya biashara kutokana na kupata oda nyingi za madini mbalimbali yakiwemo madini ya ruby na zoisite.
Ameongeza kuwa, wamegundua mambo mengi ya muhimu yatakayowasaidia wachimbaji katika sekta hiyo na hasa madini ya viwandani.
“Hakuna
kitu muhimu kama kushiriki maonesho. Ruby yetu ni bora na imependwa
sana hapa. Wengi walijua Ruby inatoka Bama lakini uwepo wetu umewafanya
kujua Ruby safi inatoka Tanzania. Namshukuru Sana Mhe. Rais na Wizara
kwa kutuwekea mazingira mazuri katika sekta hii na kutuwezesha kushiriki
maonesho haya”. Amesema, Pazi.
Aidha,
ameongeza kuwa, kama viongozi wa shirikisho hilo, wanao wajibu wa
kuwasaidia wachimbaji wengine kupata taarifa mbalimbali kuhusu sekta
hiyo kutokana na uzoefu walioupata na hivyo amewataka kufanya kazi na
Serikali kwa ushirikiano.
1 comment:
Wakati kukiwa na taarifa kuwa madini ya Tanzanite yako karibu kutoweka nchini, je kuna mwenye statistics kuonyesha nchi imefadika vipi na mawe haya adimu.
Post a Comment