ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 28, 2014

MADINI YA TANZANITE YANGA'RA BANGKOK


Baadhi ya madini ya Tanzanite ambayo yanapatikana katika mabanda mbalimbali katika maonesho ya 53 ya Kimataifa ya Bangkok Gems and Jewelry Fair.
 Mfanyabiashara  wa madini na Afisa Masoko wa Kampuni ya Tom Gems Tanzania, akimwonesha mgeni aliyefika katika banda la Tanzania kuona madini ghafi ya Tanzanite  yanayozalishwa Tanzania pekee. Wageni wengi wamefika katika banda hilo kuona Tanzanite halisi kutoka Tanzania. 
 Mwenyekiti wa Madini ya Viwandani Bw. Kassim Iddi Pazi, akimwonesha mgeni madini ya Ruby. Kutokana na maelezo ya Bw. Pazi, ameeleza kuwa, madini hayo yametoka katika maeneo ya Winza Dodoma na Matombo Morogoro.
Mfanyabiashara wa Madini kutoka Kampuni ya Tom Gems Bw.Benjamin Mtalemwa akimwonesha mgeni madini mbalimbali alipotembelea banda la Tanzania. Wanaoshuhudia kutoka kulia ni Mthamini wa Madini kutoka Wizara ya Nishati na Madini Bw. Edward Rweymamu, Wa pili kulia ni Afisa Madini kutoka Shirika la Madini Tanzania (STAMICO). Bw. Peter Maha, na  wa kwanza kulia  ni Afisa toka Wizarani Bibi. Margareth Muhony.
====================

Na Asteria Muhozya, Bangkok

Madini ya Tanzanite yamekuwa kivutio kikubwa katika maonesho ya 53 ya Kimataifa ya‘’Bangkok Gems and Jewelry Fair’’, yanayoendelea katika eneo la kibiashara la ‘Impact Challenger’, jijini Bangkok.

Madini ya Tanzanite yanayozalishwa nchini Tanzania pekee duniani, yamekuwa kivutio  kikubwa kwa wageni wanaotembelea maonesho hayo ikiwemo  wauzaji, wanunuzi na wafanyabiashara ambao wamefika  katika banda la Tanzania kutaka kuona Tanzanite halisi kutoka Tanzania.

Aidha, pamoja na kwamba madini ya Tanzanite yanazalishwa na  Tanzania pekee, lakini katika maonesho hayo ya Bangkok, madini hayo yanapatikana kwa kiasi kikubwa katika mabanda  ya washiriki kutoka nchi mbalimbali  duniani jambo ambalo linaonesha namna madini hayo yalivyo na muhimu katika sekta za kibiashara na kiuchumi.

Akizungumzia suala la uwepo  wa madini ya Tanzanite kwa kiasi kikubwa katika soko la kimataifa, na katika maonesho hayo, Kamishna Msaidizi wa Madini , Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Hamis Komba, ameeleza kuwa,  uwepo wa Tanzanite katika soko la kimataifa unaashiria mahitaji makubwa ya madini hayo duniani na umuhimu wake katika kuchangia  ukuaji wa uchumi wa Tanzania, na nchi nyinginezo ikiwemo thamani yake katika soko la kimataifa na upekee wake.

Aidha, , aliongeza kuwa, hiyo ni changamoto katika uthibiti wa madini hayo katika soko la kimataifa kutokana  na uwiano wa takwimu  za kiasi cha madini kinachotoka kwa kufuata taratibu za usafirishaji madini hayo nje ya nchi na uwingi halisi unaoonekana  katika soko la Kimataifa.

“Uwiano wa takwimu za uzalishaji Tanzania na idadi halisi ya madini iliyopo katika maonesho ya  kimataifa ni tofauti. Hii ni changamoto katika udhibiti wa madini haya” Amesema Kamishna Komba.

Hivyo, ameongeza kuwa, Serikali inalifanyia kazi suala hili kwa lengo la kufanikisha usimamizi na biashara endelevu ya madini ya Vito na usonara. 

Mbali na madini ya Tanzanite  kuwa kivutio, katika banda la Tanzania, vinyago vinavyotengenezwa kutokana  na mawe aina  ya  Zoisite, Basalt, Limestone, Travertine, Granite na White marbale yanayopatikana Tanzania  ambayo  yametengenezwa mapambo mbalimbali ya majumbani yamekuwa kivutio kikubwa katika maonesho hayo kwa wageni waliotembelea banda la Tanzania kutoka nchi za Ulaya na Asia, akiwemo pia Rais  wa Shirikisho la wafanyabiashara wa vito na usonara Bw. Somchai Phornchindarak, ambaye pia alitembelea Banda la Tanzania na kuonesha kuvutiwa na kushangazwa na mapambo hayo.

Akizungumzia kuhusu ushiriki wake katika maonesho hayo, Mratibu wa kituo cha Tanzania Geomological Center, Bw. Musa Shanyangi, amesema kuwa, maonesho hayo yamekuwa ya manufaa katika soko la madini ya mawe kutokana na wageni wengi kuonesha kuvutiwa nayo.

Shanyangi, ameongeza kuwa, tayari  kituo hicho kimeanza kufanya ukarabati wa miundombinu na kuandaa mitaala  ya kufundishia , hivyo chuo kitaanza kutoa mafunzo ya uchongaji wa vinyago, ukataji wa  madini ya vito, uchongaji wa mawe, mafunzo ya utambuzi wa madini ikiwemo pia maabara itakayotumiwa kwa ajili ya shughuli hizo.

Hivyo, amewataka vijana wa kitanzania kuitumia fursa hiyo kupata mafunzo hayo ili waweze  kuingia katika sekta ya madini kwa kuwa itawasiadia kujiajiri, kuinua vipato vyao na kuchangia katika ukuaji wa uchumi. Aidha, amewataka wadau katika sekta ya madini kuona umuhimu wa kuongeza thamani ya madini.

“ Maonenesho hayo, yamekuwa na manufaa kwa Tanzania,  kituo chetu kimepata fursa ya kufaa kwa  bidhaa za mawe, kwasababu nimejaribu kuzunguka katika mabanda mengi sana sijaona bidhaa kama hizi. Hiyo ni fursa kwetu na kwa vijana wa Tanzania katika soko hili.  Amesema Shanyangi. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Madini ya Viwanda Tanzania (FEMATA), Bw. Kassim Iddi Pazi  akielezea ushiriki wake katika maonesho hayo na soko la madini kimataifa ameeleza kuwa, maonesho hayo yamefungua fursa kubwa ya biashara kutokana na kupata oda nyingi za madini mbalimbali yakiwemo madini ya ruby na zoisite.
Ameongeza kuwa, wamegundua mambo mengi ya muhimu yatakayowasaidia wachimbaji katika sekta hiyo  na hasa madini ya viwandani.

“Hakuna kitu muhimu kama kushiriki maonesho. Ruby yetu ni bora na imependwa sana hapa. Wengi walijua Ruby inatoka Bama lakini uwepo wetu umewafanya kujua Ruby safi inatoka Tanzania. Namshukuru Sana Mhe. Rais na Wizara kwa kutuwekea mazingira mazuri katika sekta hii na kutuwezesha kushiriki maonesho haya”. Amesema, Pazi.

Aidha, ameongeza kuwa, kama viongozi wa shirikisho hilo, wanao wajibu wa kuwasaidia wachimbaji wengine kupata taarifa mbalimbali kuhusu sekta hiyo kutokana na uzoefu walioupata na hivyo amewataka  kufanya kazi na Serikali kwa ushirikiano.

Tanzania inashiriki kwa mara ya kwanza maonesho hayo ya 53 ya Kimataifa ya ‘Bangkok Gems and Jewelry Fair, ambapo mwaka  2013  ilishiriki kama nchi mwalikwa ambapo kiongozi wa ujumbe wa Tanzania alikuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati Mhe. Stephen Masele

1 comment:

Anonymous said...

Wakati kukiwa na taarifa kuwa madini ya Tanzanite yako karibu kutoweka nchini, je kuna mwenye statistics kuonyesha nchi imefadika vipi na mawe haya adimu.