Mbeya City katika picha tofauti
Timu hiyo, imefanikiwa kuzikomalia klabu kongwe za Simba na Yanga pamoja na Azam FC inayoundwa na baadhi ya wachezaji wenye uzoefu na wenye hamasa kubwa.
MBEYA City ni kati ya timu tishio iliyoleta changamoto ya ushindani katika msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na ubora wa kikosi chao kinachoundwa na wachezaji wengi vijana.
Timu hiyo, imefanikiwa kuzikomalia klabu kongwe za Simba na Yanga pamoja na Azam FC inayoundwa na baadhi ya wachezaji wenye uzoefu na wenye hamasa kubwa.
Mbeya City tangu imepanda daraja na kucheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu imefanya vitu vya tofauti kama Mwanaspoti inavyobainisha katika mahojiano na Mwenyekiti wa timu hiyo, Mussa Mapunda.
“Tulichagua jezi za rangi ya zambarau na nyeupe kutokana na hofu ya kuingiliana na rangi za vyama vya siasa na klabu za Simba na Yanga, timu yetu haiingiliani na chama chochote cha siasa na haina uhusiano wa karibu na Simba, Yanga,nembo yetu ina rangi ya njano inayowakilisha manispaa yetu.
“Sisi jezi zetu tunazinunua kutoka China, wapo mawakala wetu, ni raia wa Tanzania waishio China ambao tumefikia makubaliano mazuri, tunawatumia kwa ajili ya kutununulia na kututumia.
“Jezi zetu orijino shingoni na kifuani zina nembo ya manispaa yetu ya rangi ya njano, ukiiona jezi haina alama hizo basi ujue hiyo si origino, ni zile zizonauzwa sana mitaani.
“Jezi zetu origino tunaziuza Shilingi 15,000 kwa bei ya rejareja na si chini ya hapo, wapo baadhi ya wauzaji ambao wenyewe wanauza jezi kwa bei ya shilingi 25,000, hiyo si halali.
“Tumepanga kubadili muonekano wa jezi zetu ili zitofautiane kati ya wachezaji na mashabiki, tupo kwenye hatua za mwisho za kulileta kontena letu litakalokuwa na jezi, bendera, kofia, skafu, soksi na bipsi zetu.
“Hivi sasa tunatafuta mawakala mbalimbali nchini baada ya kukamilisha mpango huo wa kontena letu watakaosimama mauzo ya jezi, zinapatikana kwenye matawi yetu yote hapa nchini ikiwemo hapa Mbeya na kwa Dar es Salaam zinapatikana kwenye tawi letu la Ubungo Terminal, Ubungo.
“Mwanzoni jezi tulikuwa tunauza Shilingi 5000 mara baada ya kupanda daraja kabla ya kuzipandisha na kuziuza kiasi hicho cha fedha, lengo lilikuwa ni kuwahamasisha watu waipende Mbeya City. Matawi yetu yapo 11 mengi yapo hapa Mbeya maeneo ya Mwanjelwa, Tunduma, Tukuyu, Mwakaleli, Kyela na Ubungo Terminal lililopo, Dar es Salaam.
“Wakazi wa Mbeya waishio Zambia ndiyo walioomba tufungue tawi lingine huko lakini tukakataa kwa sababu ni nje ya nchi.”
Kuhusu uwanja anasema; “Tupo kwenye mikakati ya kujenga uwanja na hosteli kubwa kama kituo cha michezo, tutakachokitumia kukuza na kuendeleza vijana kwa kuanzia umri wa miaka 14-20.“Pia uwanja huo tutautumia kwa ajili ya kucheza mechi zote za ligi kuu, shamba hilo lipo Mbeya maeneo ya Iwambi lenye ekari 15 ambalo lipo chini yetu. Timu yetu inagharamiwa kila kitu na manispaa yetu kwa kuanzia kambi, usafiri, chakula, malazi na posho za timu nzima.
Wajitoa kwenye siasa
“Sisi timu yetu haifungamani na chama chochote kile cha siasa, kila mmoja anaruhusiwa kuipa sapoti timu yetu katika kuipa mafanikio. Siku ya mechi mji mzima wa Mbeya watu wanasitisha shughuli zote za kazi na barabara zote zinafungwa, watu wote wanakwenda kuishagilia timu yao.
Malengo yao ni nini? “Ni kuhakikisha timu yetu inashika tatu bora katika msimamo wa Ligi Kuu, mweleko wetu huo ni mzuri, kinachotakiwa ni kuungana kwa pamoja kuanzia viongozi na mashabiki ili tufanikishe malengo yetu.”
Kumbe wanamamiliki timu ya Netiboli: “Tofauti na timu yetu ya soka, pia tunamiliki timu ya netiboli inayoshiriki Ligi Kuu ambayo katika msimu uliopita ilifanikiwa kushika nafasi ya nne katika msimamo, ilikuwa ikijulikana kwa jina la Amambe Halmashauri.”
Chimbuko la Mbeya City: “Hii timu tuliinunua kutoka Arusha na ilikuwa ikiitwa Rhino Rangers, kikubwa tulichokifanya ni kununua hati yao ya umiliki na kuileta Mbeya. Tuliinunua timu rasmi mwaka 2011 na malengo yetu yalikuwa ni kupanda daraja ili tushiriki Ligi Kuu, kiukweli katika hilo tukafanikiwa kupanda 2012.
“Hizo ndiyo ndoto tulizoziweka ambazo tunashukuru tumefanikiwa, 2011 tuliinunua timu na 2012 tukashiriki Ligi Daraja la Kwanza kabla ya kupanda Ligi Kuu 2013 tukiwa kituo cha Morogoro,”anasema Mapunda na kusisitiza kwamba wanataka nafasi mbili za juu mwisho wa msimu
No comments:
Post a Comment