ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 6, 2014

Tunapendwa, ni kweli, lakini kwa nini tunapendwa hivyo? -

Na Jenerali Ulimwengu
SASA ningependa kuangaza masuala ambayo naamini yanahitaji marekebisho au masahihisho, kwa sababu naamini kwamba yalikosewa huko nyuma, na kwa sababu mbalimbali tumeendelea kukosea katika kuyashughulikia.

Ni kweli kwamba, kama alivyosema mwandishi mmoja aliyejitambulisha kama balozi mstaafu – hakutaja jina lake –Tanzania inasifika sana nje ya nchi na wakuu wa nchi yetu hualikwa mara kwa mara, na wakuu wa nchi nyingine wamekuwa wakitembelea nchi yetu kwa namna ya kushangaza kidogo.

Kinachogomba hapa ni kujua ni kwa nini tunapendwa hivyo? Mtu yeyote ambaye anajua nini kinaendelea katika nchi yetu atajua kwamba tumekuwa na malumbano ya ndani ya nchi kuhusu matumizi ya rasilimali za nchi hii. Baadhi ya wachambuzi wakidai kwamba rasilimali hizi zinawanufaisha zaidi wageni kuliko wananchi. Malumbano haya bado yanaendelea leo hii.

Kwamba wakuu wa nchi za kibeberu wanatupenda si jambo la kushangaza kwa sababu hali hiyo inarandana na utetezi na ulinzi wa maslahi yao. Ni jambo la kawaida kwa mmiliki wa shamba kulitembelea mara kwa mara, ili kuhakikisha kwamba maslahi yake yanaangaliwa vyema na kujenga uhusiano wa karibu na waangalizi wa siku hadi siku wa maslahi yake.

Hakuna asiyejua kwamba hadi leo bado tuna shaka kuhusu jinsi rasilimali za nchi rasilimali za nchi hii zilivyotolewa kwa wageni kwa kudharau kabisa maslahi ya wananchi. Kipindi cha awamu ya tatu, chini ya Rais Benjamin Mkapa, kilikuwa ni kipindi kichungu sana kwa wananchi walioshuhudia mali zao zikigawiwa kama vitu visivyokuwa na thamani kwa maelezo ya kustaajabisha.

Wale tuliodiriki kudai maelezo tuliambiwa tuna uvivu wa kufikiri, tuna wivu na maneno, na maneno kama hayo. Kilikuwa ni kipindi cha ubeberu wa kiuchumi kujiimarisha nchini mwetu chini ya injili za uliberali mamboleo iliyohubiriwa na watawala wetu. Hadi leo ni injili hiyo inayoendesha uhusiano wetu na wakubwa wa dunia. Sisi, pamoja na nchi yetu, ni shamba, na mwenye shamba anajulikana, na anatupenda sana, na anapenda sana kututembelea na kutualika tumtembelee kila mara!

Nilieleza mwanzoni kabisa wa mfululizo wa ngwe hii ya safu hii kwamba diplomasia ni mwendelezo wa siasa za ndani katika medani ya nje, na kwamba kinachotendeka katika diplomasia ni mwangwi wa kile kinachotendeka nyumbani. Iwapo nchini tunagawa mali za wananchi hovyo hovyo kwa mabepari wa dunia, kwa nini wasitupende? Kwa nini wasitualike mara kwa mara? Kwa nini wasije kututembelea, tena wawili wawili au watatu watatu, kama alivyosema ‘balozi mstaafu’ katika makala yake wiki iliyopita katika gazeti hili?

Hali hii inanikumbusha Malcom X na maelezo yake kuhusu ‘house nigger’ na ‘field nigger’ kwa maana ya mtumwa wa nyumbani na yule wa kondeni. Mtumwa wa nyumbani anampenda sana bwana kwa sababu anamlisha mabaki ya vitu vitamu; mtumwa wa kondeni anamchukia bwana kwa sababu bwana huyu anamfanyisha kazi ya ngwamba na anamlisha vyakula vya mifugo.

Inaonyesha jinsi tulivyodidimia katika kujiheshimu kwamba sasa tunajitathmini kwa kuhesabu ni mara ngapi tumegongwa mabegani na kuambiwa ‘nyiye ni watoto wazuri.’ Ndiyo, watakuja sana; ndiyo watatualika sana, lakini hayo yote ni kwa maslahi yao.

Tofauti na anavyoelekea kusema ‘balozi mstaafu’ mimi sijasema kwamba Rais Kikwete anasafiri mno; hilo halinihusu. Lakini siikubali mantiki ya kukubali kila mwaliko. Mialiko iko kila siku, kutoka kila kona, lakini ni muhimu kuteua ni ipi unakwenda na ni ipi unaweza kuwakilishwa. La sivyo rais, au waziri, anaweza kujikuta anahudhuria vikao vya ‘maofisa waandamizi.’

Tunaweza kujirekebisha, lakini si kwa kurekebisha diplomasia. Kumbuka nilichosema, kwamba diplomasia ni mwangi wa siasa za ndani. Uonevu, dhuluma na ulaghai katika siasa za ndani huzaa mambo yanayofanana na hayo katika siasa za nje.

Nitoe mfano mdogo utakaoeleweka moja kwa moja: Mwangalizi wa uchaguzi katika nchi ya nje hawezi kusema kwamba uchaguzi haukuwa huru na wa haki iwapo mambo aliyoyashuhudia ni kama yale yanayofanywa na serikali anayoiwakilisha.

Kwa hiyo tukitaka kurekebisha sera zetu za nje hatuna budi kurekebisha sera za ndani kwanza, kwa sababu huo ndio msingi; kilichoko nje ni mwangwi tu. Kadri tutakavyoweza kutetea kwa dhati kabisa maslahi ya watu wetu katika masuala ya kiuchumi ndani ya nchi yetu ndivyo tutakavyoweza kuyatetea katika medani ya kimataifa.

Hili ndilo jambo linalomtatiza kila anayejaribu, kama ‘balozi mstaafu’ kueleza diplomasia kama jambo linalojisimamia na kujitegemea lenyewe. Hakuna kitu kama hicho. Haki nyumbani, haki katika diplomasia; uhuni nyumbani, uhuni katika diplomasia. Hiyo ndiyo sheria.

Tukumbushane: Sisi tunataka kuwasha mwenge…. Umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini…. Ukiishi ndani ya kiza huwezi kuwasha mwenge wa kumulika nje ya mipaka yako. Huwezi kula nyama ya binadamu nyumbani kisha ukahubiri ulaji wa mboga za majani (veg) nje.

Hili ndilo fundisho analohitaji ‘balozi mstaafu’ na wengine wanaoshawishika kuamini kwamba tunaweza kuwa na diplomasia ya kiuchumi iliyotenganishwa na siasa za kiuchumi ndani ya nchi. Kinachofanyika ndani ya nchi kitapata mwangwi wake katika siasa za nje, yaani diplomasia.

Kama anavyosema ‘balozi mstaafu’ mimi si mwanadiplomasia, na wala sijawahi kuwa. Pia mimi si kuku, na kwa hivyo hiyo siwezi kutaga yai. Hata hivyo, nikipewa yai viza nitatambua kwamba halifai kuliwa.
Raia Mwema

No comments: