ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 24, 2014

Uhuru Marathon 2014 kuzinduliwa kijijini Butiama


Mratibu wa Mbio za Uhuru Marathon, Innocent Melleck akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo wakati akizungumzia maandalizi ya uzinduzi wa Mbio hizo kwa Mwaka 2014,ambapo mwaka huu Mbio hizo zitazinduliwa kwenye Kijiji cha Butiama,Mkoani Mara.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Selemani Nyambui akinzungumza kwenye Mkutano huo.

MBIO za Uhuru (Uhuru Marathon) zinatarajiwa kuzinduliwa rasmi katika kijiji cha Butiama mkoani Mara, Agosti mwaka huu, huku lengo kubwa likiwa ni kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mratibu wa Uhuru Marathon, Innocent Melleck alisema, wameamua kuzindulia Butiama ili kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye katika uhai wake alipigania mno mambo hayo.

“Tukumbuke Mwalimu Nyerere alipigania mno amani, umoja na mshikamano miongoni mwetu, pia ndiye muasisi wa Taifa hili, hivyo tuliona bora tukazindulie Butiama ili kumuenzi.”

Alisema, mara baada ya uzinduzi huo wanatarajia kuzunguka nchi nzima kuanzia ngazi ya wilaya, ili kuzitambulisha mbio hizo na kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa amani, umoja na mshikamano miongoni mwetu.

Melleck alisema, kiini cha kuanza kampeni ya kuzindua mbio hizo mapema imekuja, kwani zenyewe zimebeba ujumbe wa amani, umoja na mshikamano, hivyo ni vyema kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kutunza na kuenzi mambo hayo.

“Amani ya nchi yetu katika siku za hivi karibuni inaonekana kwenda vibaya hasa kutokana na baadhi ya vyama vya siasa kufanya siasa kwa visasi badala ya kujenga hoja kukabiliana na changamoto za kisiasa, hivyo ni jukumu letu kuilinda,” alisema.

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Selemani Nyambui alisema, kuanza maandalizi mapema kwa mbio hizo ni faraja kwao na watahakikisha wanakabiliana na changamoto zote ili ziweze kufana.

Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Desemba 8, mwaka huu na kwa mara ya kwanza zilifanyika mwishoni mwa mwaka jana na kushirikisha wanariadha kutoka nchi mbalimbali.

No comments: