ANGALIA LIVE NEWS
Thursday, February 27, 2014
UHUSIANO ULIOPO UNA MANUFAA MAISHANI MWAKO?
ILI jambo lolote liwe na maana ni lazima liwe na manufaa. Hakuna mtu anayeweza kufanya jambo ambalo halina faida kwake. Marafiki, kwa bahati mbaya sana, wapo ambao wanakuwa kwenye uhusiano bila ya kuwa na mipango yoyote ya maana.
Ndugu zangu, huwezi kukwepa mapenzi katika maisha, lakini jiulize, upo kwa sababu gani na huyo mwenzi wako? Umempenda au unataka kupoteza muda?
Anayefanya mambo bila kutazama faida na hasara zake siyo makini na anaweza kufanya mambo mengi kwa hasara au madhara kutokana na kosa hilo.
Hebu tujiulize; nani anaweza kuishi bila kupendwa? Yuko wapi anayeweza kuishi bila kuwa na familia? Hiyo familia itapatikana vipi kama hapatakuwa na uhusiano? Ni uhusiano gani unaweza kudumu bila mapenzi ya kweli? Naamini hakuna.
Marafiki zangu, naamini naeleweka vizuri sana ninaposema mapenzi yamechukua sehemu kubwa ya maisha yetu. Hiyo ni sababu inayotosha kabisa kuchambua mada hii; unanufaika na nini kwenye uhusiano wako?
Tafadhali sana, ikiwa unahitaji kuwa mpya, kujijua ulivyo na kuishi kwa malengo, fuatilia kwa makini mada hii itakubadilisha.
ANGALIA MAFANIKIO
Sijui kama kuna ambaye hafahamu kwamba anatakiwa kuwa na maendeleo maishani mwake, naamini hakuna na kama wapo ni wachache sana ambao naweza kusema akili zao zinawatosha wenyewe! Maisha ni maendeleo!
Vijana wengi wanapomaliza masomo akili zao huzielekeza katika kutafuta ajira, baadhi yao hawafikirii baada ya kupata ajira hizo wanatakiwa kufanya nini. Hili ni tatizo linalowasumbua vijana wengi wa sasa.
Hebu jiulize, umepata mafanikio gani tangu umekuwa katika ulimwengu wa uhusiano? Kama ni kazi unafanya au pengine umejiajiri mwenyewe ni sawa, lakini kuna kipi cha maana ulichofanya?
Kama hujapata mafanikio ni kwa nini? Hapa sasa ndipo ninapohusisha moja kwa moja na mapenzi. Inawezekana kabisa mapenzi yakawa chanzo cha wewe kukosa mafanikio katika maisha yako.
Si ajabu mtindo wako wa maisha katika mapenzi ni mbaya ndiyo maana hufanikiwi. Vipo vitu vya kujifunza hapa kabla ya kwenda mbele zaidi. Tuendelee kujifunza.
UFUJALI WA FEDHA
Yapo mambo mengi ambayo yanahitaji fedha na yamemaliza fedha za vijana wengi bila kujua na kujikuta kila siku wapo palepale. Kwa mfano kuhonga.
Unapokosa msimamo katika mapenzi au tabia za kubadilisha wapenzi kila mara, lazima utaangukia kwenye kuhonga. Vijana wengi wamekuwa na tabia ya kushawishi wapenzi kwa fedha!
Hili ni tatizo kubwa na inawezekana kabisa kwamba ni chanzo cha wewe kutokuwa na mafanikio yoyote katika maisha yako. Kuhonga huko hakuishii hapo, kuna pesa ya kulipia gesti.
Nyumba za kufikia wageni hutumiwa na wengi kwa ajili ya kukutana faragha na wapenzi wao. Wapo wanaopenda za bei ya juu, kati na za kawaida.
Hebu jiulize, kwa mwezi huwa unaingia gesti mara ngapi? Mpaka sasa umeshatumia kiasi gani kwa kulipia nyumba hizo za wageni? Je, hizo fedha ulizolipia gesti zinaweza kununua matofali mangapi?
Rafiki zangu, inawezekana usione kama unatumia fedha nyingi kwa matumizi yasiyo na lazima, lakini ukitulia na kuangalia hesabu utagundua kuwa unajirudisha nyuma taratibu.
Kumbuka mapenzi ya uzinzi mara nyingi huwa yametawaliwa na anasa za kila aina. Pombe huwa kiunganishi kikubwa kwa wapenzi wa aina hii. Hebu jiulize kwa dhati kabisa ya moyo wako, umetumia fedha kiasi gani kwa matumizi ya pombe wewe na mpenzi wako?
Kama nilivyotangulia kusema awali kwamba mapenzi ya ngono yamejaa anasa, wapenzi hao huwa hawatembei kwa miguu au kupanda daladala hata kama hakuna ulazima wa kutumia gari. Sehemu yoyote hutumia teksi au gari binafsi! Je, unatumia mafuta kiasi gani au kulipia teksi?
Kumbuka hapo hujazungumzia usafiri; labda una gari yako, lazima utamfuata na pengine kumrudisha kwao. Usipofanya hivyo utamlipia teksi ili imlete na kumrudisha.
Jaribu kuchanganya gharama zote kwa umakini mkubwa halafu gawanya kwa mwezi, wiki na hatimaye siku kisha utagundua unatumia kiasi gani katika mapenzi.
Tafakari, mpaka hapo mapenzi yatakuwa yamekutia hasara kubwa kwa kiasi gani? Wakati unafanya starehe zote hizo, nyumba unayoishi ni ya kupanga na haina hali nzuri, inawezekana kabisa hata kodi ya pango unalipa kwa wasiwasi.
Je, kwa mtindo huo utaendelea? Somo bado ni pana sana, wiki ijayo nitakuwa hapa kwa mwendelezo wake, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano, anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment