Mh. Nyalandu akiojiwa na vyomba vya habari
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akizindua moja kati ya magari zaidi ya 20 aina ya Toyota Land Cruiser ambayo yametolewa na wizara hiyo kwa ajili ya kukabiliana na ujangili katika baadhi ya hifadhi za taifa nchini. Hatua hiyo ni mpango wa serikali kutekeleza kwa vitendo mapambano dhidi ya ujangili. Picha zingine Nyalandu akiwa kwenye matukio tofauti wakati wa uzinduzi huo uliofanyika wizara hapo jana.
SERIKALI imeendelea na dhamira yake ya kuhakikisha inatokomeza vitendo vya ujangili wa wanyama na nyara zao baada ya 'kushusha' bunduki 500 aina ya AK 47, imeelezwa.
Mbali ya hilo, imeligawanya pori la akiba la Selous lenye ukubwa wa kilomita za mraba 55,000 kwa kuzipandisha hadhi kanda nane ili ziweze kujitegemea kiuendeshaji.
Hayo yalisema jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, wakati akikabidhi magari maalumu yatakayosaidia kukabiliana na ujangili kwenye hifadhi na mapori ya akiba nchini.
Nyalandu alisema katika kutekeleza maazimio ya Bunge na ahadi za serikali kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira, imekamilisha utaratibu wa kuzitoa bunduki zilizokuwa chini ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tangu Novemba 2012.
Bunduki hizo zilikuwa zinashikiliwa na TRA kutokana na kutolipiwa kodi na kuwa tayari wizara imetoa sh. milioni 212 kwa ajili ya kulipa kodi na ushuru.Bunduki hizo zimegharimu sh. milioni 427.
Waziri Nyalandu ambaye tangu kuchaguliwa kwake hivi karibuni amekuwa akifanya mabadiliko ya kuimarisha wizara hiyo, alisema bunduki hizo zitagawiwa kwa wapiganaji katika hifadhi za taifa za Mamlaka ya Ngorongoro, mapori yote ya akiba kwa lengo la kupambana na ujangili.
Katika hatua nyingine, Nyalandu alisema amezipandisha hadhi kanda nane zilizopo katika Pori la Akiba la Selou ili ziweze kujitegemea kiuendeshaji.
Alisema kanda hizo zitakuwa chini ya Meneja wa Poli lote la Selou, Benson Kibonde, ambaye atasaidiwa na wakuu wa kanda na kanda zao kwenye mabano: Msafiri Mashiku (Kanda ya Matambwe), Asterius Ndunguru (Msolwa), Adili Zella (Liwale), Bigilamungu Kagoma (Kingupira), William Mallya (Kalulu), Munhu Ndunguru (Miguruwe), Ramadhani Mkhofoy (Ilonga) na Msiba Kombo (Likuyu-Sekamaganga).
Mbali ya wakuu hao, Nyalandu alisea wameimarisha Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) kitakachotekeleza majukumu yake kwenye kanda nane kuu na kuwataja wakuu na kanda zao kwenye mabano kuwa ni: Paskal Mrina (Kaskazini-Arusha), Faustine Masalu (Mashariki - Dar es Salaam), John Mbwilizi (Serengeti - Bunda), Benjamin Kijija (Ziwa - Mwanza), Charles Msilanga (Magharibi - Tabora), Keneth Sanga (Kati - Manyoni), Majid Lalu (Juu Kusini - Iringa) na Abeid Mmari (Kusini- Songea).
Katika hatua nyingine, Nyalandu alisema kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa tembo na mapambano dhidi ya ujangili wamepokea magari matano aina ya Land Rover ambayo yamegawiwa kwenye kanda za Pori la Akiba la Selous za Matambawe, Msolwa, Kiwale, Kingupira na Kalulu.
Mbali na magari hayo yaliyotolewa na washirika, Mfuko wa Wanyamapori umenunua magari 14 aina ya Toyota yenye thamani ya sh. bilioni 1.6 ambayo yamegawanywa katika maeneo mbalimbali.
Mgawanyo wa magari hayo ni mawili katika Pori la Akiba la Rungwa na mengine ni moja moja katika mapori ya akiba ya Selous Kanda ya Sekamaganga, Uwanda, Lukwati - PITI, Kijereshi, Rukwa - LWAFI, Burigi-Biharamulo-Kimisi, Lukwika-Lumesule -Msanjesi, Moyowosi-Kigosi, Maswa, Mkungunero, Taasisi ya PASIANSI na Mfuko wa Kuhifadhi wanyamapori (TWPF), Mabadiliko mengine yaliyofanywa na Nyalandu ni kumteua Nurdin Chamuya kuwa msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuchuku anafasi ya Chikambi Rumisha, ambaye anarudi katika Idara ya Sera na Mipango.
Akizungumzia kuhusu mapambano dhidi ya ujangili na hatua ambazo serikali inazichukua, Nyalandu alisema vita dhidi ya majangili inahitaji ushirikiano wa watanzania wote na kwamba, serikali itaendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha maliasili za taifa zinakuwa salama.
Pia, alitumia fursa hiyo kuwaeleza watumishi na watendaji wa wizara yake kuwa wanapaswa kushiriki kikamilifu na kuwa waadilifu katika kutekeleza majukumu yao na kwamba, mabadiliko yanayoendelea kufanyika kwa sasa yanalenga kuongeza ufanisi.
''Watanzania wanatuangalia sisi watendaji tuliopewa jukumu kubwa la kulinda maliasili za taifa tunafanya nini, tunapaswa kuwa waadilifu ili kujenga imani na kuwahamasisha kuwa walinzi wa maliasili. Kama mtu tutamuona hayuko pamoja nasi tutambadili mara moja ili tuweze kusonga mbele,'' alisema Nyalandu.
Credit:Matukio na Vijana blog
No comments:
Post a Comment