Eva Kleruu na Amani Mwamwindi baada ya kukutana
Eva na Amani
SIMANZI na machozi yalibubujika wakati familia mbili za Dk Wilbert Kleruu na Said Mwamwindi zilipokutana juzi mjini Iringa kwa ajili ya maridhiano yaliyoondoa tofauti zao.
Dk Kleruu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliuawa kwa kupigwa risasi ya kichwa Desemba 25, 1971 na Mamwindi aliyekuwa mkulimaa maarufu wa mahindi katika kijiji cha Isimani, wilayani Iringa.
Tangu kifo cha mkuu wa mkoa huo kitokee miaka 43 iliyopita, kabla ya kukutana juzi, familia hizo mbili hazikuwahi kukutana.
Watoto wa kwanza wa familia hizo, Eva Kleruu (56) na Amani Mwamwindi (63) ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa kwa niaba ya familia zao walikutana na kufanya maridhiano hayo.
Maridhiano hayo yalifanyika katika ofisi ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, mjini Iringa juzi.
Mtoto wa kwanza wa Dk Kleruu, Eva alisema; “tumekuwa tukikumbuka historia ya maisha yetu na jinsi marehemu baba yetu alivyouawa.”
Huku akitetemeka na kuongea huku akitokwa na machozi, Eva alisema tukio hilo lilikuwa likiifaanya familia ya Dk Kleruu iogope kuja Iringa.
“Pamoja na hofu hiyo niliweka nadhiri kwamba ipo siku nitafika Iringa na kutembelea sehemu ambayo marehemu baba yangu aliuawa katika shamba la Mwamwindi,” alisema.
Alisema baada ya kutembelea eneo hilo alipanga kukutana na watoto wa Said Mwamwindi ili kuweka maridhiano yatakayofanya watumie tukio lile la mauaji ya Dk Kleruu kuwaunganisha.
Kwa kupitia Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga, Eva alisema waliweza kukutana na kufanikisha azma yaao hiyo.
“Ile siku imefika na leo nimekutana na mtoto wa kwanza wa Said Mwamwindi, Meya Amani Mwamwindi na kumaliza tofauti zao zilizosababishwa na mauaji hayo,” alisema.
Eva alisema baada ya kukutana na Mwamwindi na kuziweka kando tofauti za kihistoriaa baina ya familia zao anajihisi ni sehemu ya maendeleo ya mkoa a Iringa.
Alisema kwa kupitia kampuni yao ya Power Supply Cooperation wako tayari kuhakikisha kwamba miradi midogo ya uzalishaji umeme inajengwa katika maeneo mbalimbali mkoani Iringa ili kufikisha nishati hiyo kwa watu wengi zaidi.
Katika kikao chao hicho kilichomtoa machozi pia Amani Mwamwindi, walikubaliana kukutana na familia zao na kutoa taarifa ya maridhiano hayo.
Kwa upande wake Mwamwindi aliyekuwa akiongea kwa hisia inayoashiria uchungu fulani alisema; “nimefurahishwa kukutana na dada yangu huyu na kuondoa tofauti zetu za kihistoria.”
Mwamwindi alisema; “kabla na baada ya tukio tukio hilo litokee miaka 43 iliyopita familia zetu zilikuwa hazijuani vizuri. Na sisi tulikuwa watoto, leo tunakutana tukiwa watu wazima, ni jambo la kushukuru mwenyezi Mungu.”
Alisema baada ya kikao chao hicho watapanga siku nyingine ambayo kwa pamoja familia hizo mbili zitakutana zikiwa na wawakilishi wengi zaidi.
frankleonard.blogspot
No comments:
Post a Comment