Alitoka asubuhi kwenda kujumuika na wanawake wa mjini na alirejea nyumbani alfajiri akiwa amelewa na siku nyingine hakurudi kabisa.
Gaudensia alivumilia, wakati mwingine alijitahidi kuzungumza na mume wake ili abadilike lakini haikuwezekana. Reina alimpiga marufuku Gaudensia kutumia gari walilopewa na wazazi wake. Zaidi ya hapo akawa anachukua fedha bila utaratibu kwenye maduka yote, Gaudensia akihoji anajibiwa: “Tulia hizi mali ni zangu, nimepewa na wazazi wangu, hukutoka nazo kwenu.”
Baada ya kuona manyanyaso yamezidi, huku mali walizopewa na wazazi wa Reina zikizidi kupukutika, Gaudensia akaona isiwe tabu, akaamua kwenda chuo angalau apate shahada ya kwanza. Alikwenda Udom, hali ambayo ilimfanya awe mbali na mumewe.
Huku nyuma akawa anapata taarifa za mume wake kuingiza wanawake mpaka kwenye chumba chao cha kulala. Alivumilia kwa kuhisi kwamba pengine angeweza kubadilika baadaye. Hata hivyo mambo yalikuwa tofauti kabisa. Akiwa chuoni akasikia taarifa kuwa maduka yote yamefilisika.
Aliumia sana ila hakujua afanye nini. Alipowalalamikia wazazi wa Reina, hawakuwa na la kufanya zaidi ya kusikiliza na kukaa kimya. Maisha yalizidi kupiga hatua kwa kasi ya ajabu, kila likizo alirejea nyumbani lakini mapenzi kwa mumewe hakupata kabisa.
Reina alirejea nyumbani usiku wa manane akiwa amelewa. Kipindi hicho maduka yamefilisika na hana fedha kabisa, kwa hiyo akawa kazi yake kwenda kwa wazazi wake kupiga mizinga ndipo maisha yanakwenda. Hali ilikuwa mbaya sana.
Miezi kisha mwaka ulikatika, ukafuata wa pili baadaye wa tatu, mwisho akafanikiwa kumaliza shahada yake ya kwanza ya uhasibu. Ni kipindi ambacho Reina naye alifanikiwa kupata kazi kwenye kampuni ya Tanzania One, Arusha kama mhasibu msaidizi, mambo yake yakawa supa.
Taarifa za Reina kupata kazi, Gaudensia alizipokea kwa furaha sana, akampigia simu kumpongeza lakini alipata majibu ya kukatisha tamaa lakini hakujali sana. Maana alipompigia simu kumpongeza, Reina alijibu: “Sasa pongezi za nini na inakuhusu nini, kazi nimepata kwa ujanja wangu.”
Gaudensia aliendelea na utaratibu wake wa kila siku, kila asubuhi ilikuwa lazima ampigie simu kumsalimia, mchana kumjulia hali na usiku kumtakia usiku mwema. Reina alipogoma kupokea, yeye alimtumia SMS na mambo yalikwenda.
Baada ya kumaliza chuo na kurejea Dar es Salaam, hakumaliza siku tatu, aliunganisha Arusha kwenda kuungana na mume wake. Kule palikuwa na hali mbaya sana. Gaudensia alipoingia ndani kitu cha kwanza cha kumuumiza kilikuwa ni kukuta boksi la kondomu, na alipotazama kapu la uchafu (dustbin) chumbani, alikuta kondomu zilizotumika.
Akamuuliza mumewe kuhusu uwepo wa kondomu hizo, akajibu: “Ulitaka nitembee nao bila kinga?”
Gaudensia: “Reina hebu onesha heshima kwangu, mimi ni mkeo wa ndoa, unanijibu unavyojisikia kweli, hiyo ni tabia gani?”
Reina: “Tatizo wewe mwanamke una gubu sana, badala ya kunipongeza kwa kuwa mwangalifu, wewe unanisema kukuta kondomu. Hizi nimeziacha makusudi ili uone jinsi ninavyojilinda.”
ITAENDELEA WIKI IJAYO.
GPL
No comments:
Post a Comment