
Rais wa Awamu ya kwanza Tanzania, Hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa na Rais wa sasa, Jakaya Kikwete kwenye moja ya mikutano yake aliyowahi kuifanya. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Wakati mjadala wa Katiba Mpya hususani muundo wa Muungano ukipamba moto, imebainika kuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kupendekeza kuanzishwa Serikali ya Tanganyika, kama sharti la kuingia kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki.
Maelezo hayo ya Mwalimu Nyerere yapo kwenye kitabu chake cha Uongozi Wetu Na Hatima ya Tanzania kilichoandikwa mwaka 1994 na kutolewa 1995.
“Wakati Mwalimu anaandika kitabu hiki mwaka 1994 taifa letu lilikuwa linakabiliwa na changamoto kadhaa za kihistoria ambazo ndizo zilimfanya kuingilia kati na kuandika kijitabu hiki ambacho kilikuwa kama nasaha, onyo, na usia kwa Watanzania,” inasema sehemu ya utangulizi wa kitabu hicho.
Katika sura ya nne ya kitabu hicho, pamoja na mambo mengine Mwalimu Nyerere alizungumzia suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo alieleza sababu zilizofanya muungano wa serikali mbili ukaanzishwa.
“Labda ni vizuri kukumbuka kwamba shabaha ya baadhi yetu ilikuwa ni kuziunganisha nchi za Afrika Mashariki ziwe nchi moja,” alisema katika kitabu chake hicho.
Alieleza kuwa, wakati Zanzibar na Tanganyika zinaungana, Kenya, Uganda na Tanganyika zilikuwa katika mazungumzo ya kutafuta uwezekano wa kuungana.
“Kama jambo hilo lingetokea, nina hakika kabisa kwamba mfumo wa nchi mpya ambayo ingezaliwa ungekuwa ni wa shirikisho; ama shirikisho la nchi tatu zenye serikali nne, au shirikisho la nchi nne zenye serikali tano.
“Kwa kweli hata kesho nchi za Afrika Mashariki zikiamua kuungana na Tanzania ikawa ni mshiriki, naamini kuwa ni rahisi zaidi kushirikisha Tanzania yenye serikali mbili ya Zanzibar na ya Tanganyika kuliko Tanzania yenye serikali mbili, ya Tanzania na Zanzibar,” alisema.
Alisema kwa kufanya hivyo, wapendao Utanganyika watakuwa wazalendo zaidi, badala ya kuwa wasaliti, wakiazimia Afrika ya Mashariki iliyoungana kuwa nchi moja, kuliko Tanzania iliyotengana ikawa nchi mbili.
Baadhi ya wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakizungumzia suala hilo, walisema kuwa ni vyema kuangalia zaidi matakwa ya wananchi kuliko kujali tu mfumo.
Mmoja wa wahadhiri hao, Faraja Christoms alisema wakati Mwalimu Nyerere akiandika kitabu cha Uongozi Wetu Na Hatima ya Tanzania, alikuwa na hofu ya kumeguka kwa muungano.
“Wakati ule kulikuwa na wale wabunge wa G55 jina walilobatizwa na Profesa Issa Shivji, hawa wabunge walikuwa wanaona kama Zanzibar inapendelewa sana, walikuwa wanaona kama wanalalamika tu kama watoto.
Alisema kuwa, kwa mtazamo wake serikali mbili ni bora zaidi ili baadaye iwepo moja lakini kama suala hilo limeshindikana ni bora kuwepo na mfumo wa serikali tatu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Emanuel Muya alisema mazingira yaliyomfanya Mwalimu Nyerere kuandika kitabu cha Uongozi Wetu Na Hatima ya Tanzania, ni tofauti na haya yaliyopo leo.
“Pamoja na yote bado kuna umuhimu wa kuungana Tanganyika na Zanzibar, hakuna anayetaka kuuvunja muungano, hata mwalimu alikuwa anataka muungano imara, alivyoondoka muungano ulikuwa imara.
“Uwe unakubalika pande zote, kwa sasa una matatizo pande zote, lazima tukubali kupata mazingira aliyokuwa akiyataka Mwalimu,” alisema.
Mwananchi
2 comments:
Utawala wa Mwalimu ulishamalizika miaka mingi jamani huu ni uhuni wa kisiasa.
Kwa mtu mwenye akili timamu kwa mazingira ya ulimwengu wa sasa swala la serikali tatu ni sahihi, kwani mtazamo na makusudio ya Mwl.Nyerere wakati huo ilikuwa serikali mbili(ya Muungano na Zanzibar) kupelekea serikali moja( Tanzania). Zanzibar ilitegemewa ife, lakini hiyo imeshindikana. Hivyo basi kudumisha umoja na mshikamano, serikali tatu ni jibu muafaka na kuwarudishia haki watanganyika walioipoteza hapo 1964 ( after Nyerere sacrificing their sovereinity). Hivyo basi demokrasia na haki ya wengi izingatiwe. Mawazo yasiyo na msingi kinyume na hapo ni uwendawazimu na hayakubaliki. Soma "Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania".
Post a Comment