Inafuatia polisi kupiga marufuku chopa kuruka kesho
NEC: Ruksa endapo hazina nembo, alama ya chama
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe
Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi, aliyasema hayo
jana wakati akizungumza na Waandishi wa habari mjini hapa kuhusu hali ya
usalama na polisi walivyojipanga kukabiliana na matukio ya vurugu
yanayotishia uvunjifu wa amani kwenye uchaguzi huo.
Alisema kuwa hakuna chama chochote cha siasa kinachoruhusiwa
kurusha helikopta angani siku ya Jumapili kwa kuwa hatua hiyo ni sehemu
ya kampeni ambazo kisheria NEC imeweka ukomo ambao ni Machi 15, saa
12:00 jioni.
Mungi alisema chama ambacho kitarusha helikopta hizo kwa kisingizio
cha kulinda kura zao ni kuvunja sheria kwa kuwa kura hizo zinalindwa na
mawakala waliotajwa kwenye sheria ya uchaguzi.
MBOWE: NIPO TAYARI KUFIA ANGANI
Mbowe, akizungumza katika mkutano wa kampeni kijiji cha Sadani,
alisema kauli ya kamanda wa polisi Iringa kuzuia chopa yao ni mkakati wa
kutaka kusababisha maafa na yupo tayari kufia angani siku ya Jumapili.
"Tutaruka kwa chopa mbili, RPC Mungi apende asipende niko tayari
kufa...Nazungumza kwa mamlaka kama kiongozi mwenye dhamana. Nchi hii
kila mtu ana haki ya kutumia usafiri wowote...Hatutaogopa kuruka kwa
chopa, mpeni salam kamanda wa polisi," alisema Mbowe.
NEC YATOA UFAFANUZI
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian
Lubuva, akizungumzia matumizi ya chopa yaliyotangazwa na Chadema,
alisema kuwa chombo chochote ambacho kilitumika katika kampeni hizo,
kikiwa na nembo au bango la chama chochote cha kisiasa hakitakiwi kwenye
uchaguzi huo, isipokuwa kama vitaondolewa vitu hivyo, vinaruhusiwa
kutumika.
"Tunachosisitiza hapa ni material (nyenzo) ambazo zilikuwa
zikitumiwa wakati wa kampeni na hatuhitaji kuona nguo, kofia wala
magwanda siku hiyo...Matumizi ya chopa sisi kama tume, hatujakataa
kutumika lakini tunasema kama itatumika kubeba abiria kutoka uwanja
fulani kwenda sehemu nyingine na si kutua kwenye kituo cha kupigia kura,
hapo ni sawa,"alisema Jaji Lubuva.
Alisema ni vigumu NEC kuijibia polisi kuhusu katazo la matumizi ya
helikopta hizo siku ya uchaguzi lakini ukweli ni kwamba kama wataweza
kutofautisha mambo waliyokuwa wakiyafanya katika kampeni zao na uchaguzi
huo, wanaweza kuitumia.
Hata hivyo, Meneja kampeni za Chadema jimbo la Kalenga, Godbless
Lema, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, alisema chopa ya
Chadema inayomilikiwa na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo,
itapasua anga kama kawaida ikiwa imembeba mgombea wao, Grace Tendega na
viongozi wengine wa chama hicho.
"Tutaitumia helikopta yetu kusambaza chakula na maji kwa mawakala
wetu katika vituo 216 vilivyotengwa. Helikopta ni usafiri kama gari
ambalo wanatumia CCM au Chadema katika kampeni hizi...CCM wana magari
yao ambayo ni Land Cruizer na Chadema tunazo Ford Ranger halafu
yameruhusiwa kutumika lakini chopa hawataki; kwani nani asiyejua lipi ni
la nani,"alihoji Lema.
Alisema Chadema itaheshimu sheria za uchaguzi kwa kuondoa nembo na
alama za kichama katika helikopta hiyo na kuitumia kufanya kazi muhimu
ikiwamo kumsaidia mgombea kuvifikia vituo vilivyopo mbali katika jimbo
hilo.
Alisema hata kama vyombo vya dola vinakazana kuzuia matumizi hayo
ya helikopta, Chadema pia imejipanga kuzuia uhalifu wowote katika jimbo
hilo lakini pia wanategemea kuongeza idadi ya vijana wengine 1,000,
watakaongeza nguvu kwenye kata zote 13.
DAFTARI LA WAPIGA KURA
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Operesheni na Oganaizesheni za
Chadema, Benson Kigaila alisema NEC inajaribu kuficha ukweli kuhusu
uboreshaji wa daftari la wapiga kura kwa sababu imeongeza kinyemela
majina ya watu zaidi ya 1,000 katika daftari la wapiga kura bila ya
kutangaza kwa umma na kuvishirikisha vyama shiriki katika uchaguzi huo.
"Kwa nini daftari hili liboreshwe Kalenga tu, halafu wasitangaze
umma ukajua au kuvishirikisha vyama vinavyoshiriki uchaguzi huu. Huku
kuna maanisha nini kama si hujuma lakini pia hadi jana kuna mawakala
zaidi ya nusu walikuwa hawajaapishwa,"Alisema Kigaila.
Alisema kufuatia ucheleweshaji huo, mawakala wao kama watakuwa
hawajaapishwa hadi Jumamosi, Chadema kinaitaka Tume ya Jaji Lubuva
kuwaapisha wakiwa kwenye vituo vyao kwa sababu hawatakubali kama chama
vituo hivyo vikabaki wazi kwa minajili ya kusubiri mihuri.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment