ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 25, 2014

WATENDAJI DAR WAASWA KUSHIRIKIANA ILI KUWEKA JIJI KATIKA HALI YA USAFI

DSC_1151
Meneja Huduma Maji taka kutoka Dawasco, Mathias Mulagwande (mwenye suti ya damu ya mzee) akinyoosha kidole kumuonyesha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick (wa pili kulia) sehemu korofi za kutiririsha maji machafu barabara ya Morogoro kati kati ya jiji.
Na Damas Makangale, MOblog Tanzania
WATENDAJI wa Mamlaka za Maji Safi na Taka, Manispaa, Halmashauri, Wakala wa Barabara na Mabasi yaendayo kasi wameshauri kuwa na utaratibu wa kuwasiliana na kushirikiana kwa pamoja ili kuleta tija katika usombaji taka katika jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza na mwandishi wetu, kwenye ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mh Said Meck Sadick, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Green Waste Pro Ltd. Bw. Anthony Mark Shayo amesema kuwa tatizo la jiji la Dar es Salaam ni watendaji wa mkoa hawana mawasiliano ya kutosha katika utendaji kazi wa kila siku.
Shayo alizungumza hayo kwenye ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ya kugagua hali ya usafi katika maeneo kadhaa pamoja na kuangalia maeneo korofi katika kutitirisha maji machafu kwenye mitaro kadhaa kati kati ya jiji.
“tatizo kubwa katika jiji la Dar es Salaam ni watendaji wa jiji, manispaa, wakala wa barabara, Tanesco na mamlaka za maji safi na taka kutokuwa na utaratibu wa kuwasiliana katika utendaji kazi wa kila siku katika kuboresha usombaji wa taka kwenye jiji la Dar,” amesema Shayo
DSC_1173
Meneja Huduma Maji taka kutoka Dawasco, Mathias Mulagwande akiwaonyesha baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar, Said Meck Sadick na Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu baadhi ya mashimo (Potholes) ambayo ni hatari kwa wananchi watembea kwa miguu baada ya ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo kasi.

Shayo alilisisitiza kwamba katika utendaji kazi wa jiji kama la Dar inahitajika ushirikiano wa dhati kati ya wadau wa kusomba taka na watendaji wa manispaa pamoja na jiji ili kuweka mkoa wa Dar es Salaam katika hali safi wakati wote.
Amesema kuwa ingawaje tatizo kubwa la uchafu linasababishwa na miundombinu mibovu ya barabara na maji hasa kuelekea katika dampo kuu la mkoa sehemu ya Pugu Kinyamwezi, Gongo la Mboto.
Shayo ambaye kampuni yake inajishughulisha na usombaji wa taka ngumu na nyepesi katika mkoa wa Dar es Salaam amesema kwamba mamlaka zinazohusika kwa kushirikiana na wadau lazima watoe elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi taka.

“sehemu ya dampo la Pugu Kinyamwezi. inahitajika kampuni ya ujenzi yenye uwezo wa kuboresha miundombinu ya barabara kuelekea kwenye dampo ili kupunguza foleni ya magari ya taka na kuongeza tija ya kazi katika eneo husika,” aliongeza
DSC_1231
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mh Said Meck Sadick akiongoza msafara wa baadhi ya viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam katika kuangalia hali ya usafi na miundombinu ya maji na barabara jijini Dar.

Kwa upande wake, Minael Mshanga Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, amesema jiji limejipanga kufanya ukarabati wa miundombinu ya barabara kuelekea dampo ili kuongeza kasi ya magari yanayokwenda kumwaga taka katika dampo hilo.
“hivi tupo katika hatua za mwisho na tumempata mkandarasi wa kuja kujenga na kutengeneza miundombinu ya barabara kuelekea katika dampo pamoja na kutengeneza mataa katika eneo husika ili kazi ya kutupa taka ifanyike usiku na mchana,” amesema Mshanga
Aliongeza kwamba jiji lina mpango wa kuanza kushirikiana kwa karibu na wakandarasi wazalendo katika kuleta ufanisi wa usombaji taka ili kuzuia magonjwa ya mlipuko katika mkoa wa Dar es Salaam.
DSC_1240
Mbunge wa Ilala, Hassan Zungu akisisitiza jambo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar, Said Meck Sadick wakati wa ziara ya ghafla ya kugagua hali ya miundombinu ya maji na barabara kati kati ya jiji la Dar.
DSC_1310
Baadhi ya magari ya wakazi wa jiji yakipita kwa taabu katika madimbwi na mashimo ya maji machafu kati kati ya jiji la Dar es Salaam.
DSC_1337
Viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam wakijadili moja ya sehemu korofi kati kati ya jiji karibu na Haidery Plaza ambapo kipindi cha mvua maji taka yaliyochanganyikana na kinyesi yanatuama kwa kipindi kirefu ambapo hakuna mfereji wala mtaro wa maji machafu.
DSC_1350
Mashimo ya miaka nenda rudi yasiyopatiwa ufumbuzi lakini baada ya ziara yatarekebishwa.
DSC_1402
Mkuu wa mkoa wa Dar, Said Meck Sadick akitoa ushauri kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Jackson Midala (mwenye tai nyeusi).
DSC_0468
Kaimu Mkuu wa Idara ya Udhibiti taka kutoka jiji, Enezael Ayo (kushoto) akifafanua jinsi magari ya taka yanavyomwaga taka katika dampo kuu la Pugu Kinyamwezi jijini Dar wakati wa ziara ya Mkuu wa mkoa wa Dar.
DSC_0477
Mkurugenzi Mtendaji wa Tirima Enterprises, Robert Ngeleshi akizungumza changamoto na matatizo ya mawakala wa kusomba taka katika jiji la Dar ambao waliongozana na Mkuu wa mkoa kwenye ziara hiyo.
DSC_0514
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Green Waste Pro Ltd. Bw. Anthony Mark Shayo akielezea jambo kwa mkuu wa mkoa wakati wa kuhitimisha ziara hiyo katika maeneo ya dampo Pugu Kinyamwezi.
DSC_0531
Moja ya Bull dozer linalorekebisha barabara likiwa limeharibika kutokana na miundombinu mibovu katika dampo la Pugu Kinyamwezi.
DSC_0553
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Minael Mshanga (kulia kwa Mkuu wa Mkoa) akitoa ufafanuzi wa matatizo na changamoto za usombaji na utupaji taka katika dampo la Pugu Kinyamwezi.
DSC_0560
Mkuu wa Mkoa wa Dar, Said Meck Sadick akiagana na wakandarasi wa usombaji taka na watendaji wa jiji. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi.

No comments: