ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 21, 2014

Azam kuzibomoa Simba, Yanga

Joseph Omog,kocha wa Azam FC

Usajili wa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Azam FC utazibomoa safu za kiungo na ushambuliaji za timu za Simba, Yanga na Mbeya City, imefahamika.

Mara tu baada ya mechi yao ya mwisho waliyoshinda 1-0 dhidi ya JKT Ruvu kwenye uwanja wao wa nyumbani jijini Dar es Salaam juzi, Azam FC juzi ilitawazwa rasmi kuwa bingwa mpya wa ligi hiyo wakimaliza msimu bila kupoteza hata mechi moja huku wakiwa na pointi 62.

Joseph Omog, kocha wa Azam FC, katika mahojiano maalum na NIPASHE uwanjani hapo juzi, alisema ameona wachezaji wazuri kutoka timu hizo tatu ambao ameshauagiza uongozi wa 'waoka mikate' wa Dar es Salaam uhakikishe unawanasa ili kuimarisha timu yao itakayoiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika mwakani.

"Ligi ilikuwa ngumu sana, timu za Mbeya City, Simba na Yanga zilitupa wakati mgumu... kuna wachezaji wazuri nimewaona Simba, Yanga na Mbeya City. Nimewaambia viongozi wawasajili msimu ujao ili tuwe na timu bora zaidi.

"Ninatambua klabu za Simba na Yanga si rahisi kuachia mchezaji lakini ninaamini uongozi utawashawishi. Siwezi kukutajia majina ya wachezaji husika lakini ni viungo na washambuliaji," alisema raia huyo wa Cameroon, ambaye amekuwa akivutiwa na Amisi Tambwe wa Simba.

Aidha, kocha huyo wa zamani wa Berrekum Chelsea ya Ghana na Leopards ya Congo aliyoipa ubingwa wa Kombe la Shirikisho barani Afrika, alisema siri ya mafanikio ya Azam FC msimu wa 2013/14 ni ushirikiano uliokuwa ukitolewa na uongozi wao ukichagizwa na kujituma kwa wachezaji na benchi lake la ufundi.

Omog alianza kuinoa Azam FC katika mzunguko wa pili akirithi mikoba ya mtangulizi wake Muingereza Stewart Hall aliyepata ulaji wa kuwa mkurugenzi wa kituo cha kisasa cha michezo cha Kidongo Chekundu kinachojengwa Ilala, Dar es Salaam na klabu ya Sunderland ya Ligi Kuu ya England kwa kushirikiana na kampuni ya kufua umeme ya Symbion Power.
CHANZO: NIPASHE

No comments: