ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 22, 2014

Logarusic aitega Simba

Beki wa Simba, Nassor Masoud (kulia) akiwania mpira na mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa. Timu hizo zilitoka sare 1-1. Picha na Michael Matemanga

Dar es Salaam. Baada ya kuisaidia Simba kupata sare 1-1 na Yanga, Kocha  Zdavko Logarusic amesema hatima ya kuendelea kuifundisha timu hiyo itajulikana wiki hii.
Akizungumza na gazeti hili, Logarusic alisema anatarajia kukutana na uongozi wa Simba wiki hii ili kujadili mustakabali wake ndani ya klabu hiyo kwa vile mkataba wake wa sasa tayari umefikia tamati.
“Kimsingi mkataba wangu wa miezi sita wa kuifundisha  Simba umemalizika, lakini wiki ijayo nitakutana na uongozi na kujadiliana nao kama bado wananihitaji au niondoke,” alisema Logarusic.
Katibu mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema ni kweli wamepanga kukutana na kocha Loga wiki hii kujadiliana naye kabla hajaondoka nchini.
“Kiufundi mkataba wake unamalizika Mei 30, lakini kwa sababu sasa hatuna mechi kwa sababu ile ya jana (juzi) ilikuwa ya mwisho hivyo uongozi utakutana wiki hii na kuzungumza naye.
“Tunaamini baada ya hayo mazungumzo tutakuwa tumejua mstakabali wake kabla ya kuondoka kwake kurudi kwao wiki ijayo.
Kamwaga aliongeza  mbali ya suala la kocha huyo, pia kuna wachezaji waliomaliza mikataba pamoja na kuboresha maslahi ya nyota wengi.
“Siwezi kusema nina mkataba wake umekwisha nitakuwa kama namweka sokoni, ila tutaboresha mikataba ya Jonas Mkude, Ramadhani Singano na wengine baada ya kuonyesha kiwango cha juu msimu huu,” alisema Kamwaga.
Logarusic alipewa mkataba wa miezi sita na klabu hiyo wakiangalia mwenendo wa timu hiyo ili waamue kama wamuongezee mkataba ama la, lakini kwa jinsi Simba ilivyofanya vibaya msimu huu, kocha huyu anaonekana kuwa katika hatari ya kutimuliwa, ingawa klabu ya Hearts of Oak ya Ghana imeonyesha nia ya kuhitaji huduma yake.
Hearts of Oak inakusudia kumpa Logarusic mkataba wa miaka miwili na nusu kuanzia Juni mwaka huu kutokana na mazungumzo ya awali waliyofanya kati ya klabu hiyo na kocha huyo raia wa Croatia, ingawa pia klabu ya  FC Leopards ya Kenya inamuhitaji.
Akizungumzia mchezo wa Jumamosi iliyopita Logarusic alisema: “Niseme wazi sisi ndiyo tuliamua kuwapa Yanga sare ambayo hawakustaili kwa sababu tu ya uzembe wa mabeki kuona kama mechi imemalizika.”
Katika mchezo huo, Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao lililokwamishwa na  Haruna  Chanongo dakika ya 75 kisha Yanga kusawazisha dakika ya 86 kupitia kwa Simon Msuva.
“Ukweli ni kwamba katika soka dakika moja inatosha kubadilisha matokeo ya mchezo hivyo tulitakiwa kuwa makini muda wote wa mchezo,” alisema Loga ambaye mara baada Yanga kusawazisha alionekana kummfokea  beki wa kushoto, Issa Rashid.
Aliongeza:”Kama tungekuwa makini tungepachika mabao mengi kwa sababu tulitengeneza nafasi nyingi kuliko Yanga. Kifupi mechi tuliitawala  sisi,”.
Mwananchi

No comments: