Advertisements

Thursday, April 17, 2014

MKURUGEZI WA HALMASHAURI AACHISHWA KAZI HABARI KAMILI HII HAPA

by nasanyo fortnine
Katibu Mkuu, Jumanne Sagini.
 
Serikali imemwondoa madarakani Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Hilda Lauwo, na sasa anakwenda kuwa mshauri wa masuala ya kijamii katika ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) zilizothibitishwa na Katibu Mkuu, Jumanne Sagini, Lauwo anahamishwa kwenda ofisi ya RAS na nafasi yake inachukuliwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, Trasias Kagenzi.

Lauwo mwenyewe alithibitisha kwa njia ya simu jana kuwa alipewa barua ya kwenda kuripoti kituo chake cha kazi na alikuwa safarini kwenda Shinyanga.

Sagini alisema: "Lauwo amekuwa akiandamwa na tuhuma mbalimbali na nyingi zimekuwa zikiandikwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini na tulipofanya uchunguzi wa kina tulibaini tuhuma zilizo nyingi ni za kweli, hata naibu waziri wa Tamisemi, Aggrey Mwanri alipofanya ziara mkoani Simiyu alipofika Maswa alijionea baadhi ya tuhuma hizo."

Alisema kuwa Lauwo anahamishiwa kwa RAS Shinyanga kuwa chini ya Idara ya Mipango ambako atakuwa mshauri wa maendeleo ya jamii.

"Amehamishiwa kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na sasa atafanya kazi chini ya RAS Shinyanga na Mkuu wake wa kitengo atakuwa Ofisa Mipango katika Sekretarieti ya Mkuu wa Mkoa na Lauwo atakuwa Mshauri wa maendeleo ya jamii," alisema.

Lauwo amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji katika halmashauri za wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro kabla ya kuhamishwa baada ya kutokea mzozo na madiwani kisha akahamashiwa Halmashauri ya Namtumbo mkoa wa Ruvuma ambako pia hakudumu kwani ulitokea tena mzozo na madiwani, akapelekwa Halmashauri ya Wilaya Ludewa, Mkoa wa Njombe, ambako inadaiwa pia mambo hayakuwa shwari kisha akahamishiwa Halmashauri ya wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu, ambako pia amekuwa na mizozo na madiwani.

Tuhuma mbalimbali ambazo Lauwo amekuwa akielekezwa ambazo nyingine amezikana ni pamoja na matumizi mabaya ya fedha na madaraka.

Wakati Mwanri alipofanya ziara Maswa, wananchi walilalamika juu ya mwenendo wa Lauwo na kuomba ahamishwe.

Katika hatua nyingine, baadhi ya wananchi wilayani Maswa waliozungumza na wameipongeza serikali kwa uamuzi wa kumwondoa Lauwo Maswa.

Walisema kuwa adhabu aliyopata Lauwo ni ya haki na kuitaka kuendelea kuchukua hatua kwa watumishi wengine wa serikali wasiozingatia maadili ya kazi zao.

"Hii ilikuwa ni vita yetu sote wapenda maendeleo wa Maswa na Tanzania kwa ujumla na tumeishinda na tuendelee kushikamana kwa wote wanaolewa madaraka na kushindwa kuwatumikia wananchi," alisema Pius John, mkazi wa Maswa.

No comments: