Advertisements

Saturday, April 5, 2014

Rais Kikwete aagiza shamba la Efatha Ministry lirejeshwe kwa Wananchi

Taarifa ya maandishi via HabariLeo, Taarifa ya video via Ahmad Michuzi/MMG  -- Rais Jakaya Kikwete ameagiza kurejeshwa kwa shamba la ekari takribani 12,000 kwa wananchi ambalo liliuzwa kwa taasisi ya Efatha Ministry inayoongozwa na Nabii Josephat Mwingira.
Agizo hilo la Rais Kikwete limetolewa jana kupitia Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana wakati akiwahutubia wakazi wa Kata ya Moro katika Kijiji cha Mawenzusi.

Wakati akiwasili kijijini hapo Kinana alipokewa na mabango yenye ujumbe unaozungumzia kilio cha wananchi kudhulumiwa shamba hilo.

Wananchi hao wakiongozwa na Mbunge wao wa Sumbawanga Mjini, Hilal Aeshi pamoja na Diwani wa Kata hiyo ya Moro, Festo Mwananjela, waliwasilisha kilio chao kuhusu unyang'anyi wa shamba hilo na taasisi hiyo ya Efatha, hali
ambayo imewaacha wakazi wa eneo hilo bila kuwa na eneo lolote la kufanyia shughuli za kilimo.

Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara, Mwananjela alisema shamba hilo kabla ya kutaifishwa na Serikali lilikuwa ni maeneo ya kilimo ya wakazi wa eneo hilo, lakini baadae lilichukuliwa na Serikali kwa ajili ya kuendelezwa, hata hivyo Serikali ilishindwa kuliendeleza na kuliuza kwa taasisi hiyo.

"Cha kushangaza ni muda mrefu tangu shamba hilo kuuzwa kwa
taasisi hiyo, lakini hakuna shughuli zozote zinazoendelea kwenye mashamba hayo huku wananchi wa maeneo hayo wakinyanyaswa na kupigwa pindi wanapotumia njia zilizomo ndani ya shamba hilo ambazo walikuwa wakitumia tangu awali," alisema.

Naye Mbunge Aeshi alimuonesha Kinana, kijana Nuru Togwa aliyekatwa masikio yote mawili na walinzi waliowekwa kwenye shamba hilo wakati akipita akitoka kijijini kwake kuelekea Sumbawanga Mjini.

Kinana akizungumzia sakata hilo alisema, wananchi hao kutokurejeshewa shamba hilo na Serikali ni dhuluma na haikupaswa kuliuza shamba hilo bila kushirikisha wananchi hao.

"Serikali ilitakiwa iombe radhi wananchi baada ya kuona imeshindwa kuliendesha shamba hili, ingelirejesha kwao na si kuliuza kwa mwekezaji mmoja na kuacha watu 16,000 wakiwa hawana sehemu yoyote ya kufanyia shughuli zao kilimo, hii si haki," alisema.

Aidha, alionya juu ya watu wanaojiita wawekezaji ambao wanakuja nchini na kuchukua maeneo makubwa ya ardhi ya wananchi kwa madai ya kuwekeza na badala yake wamekuwa wakitumia mashamba hayo kukopea na kujinufaisha wenyewe na si kufanya shughuli iliyokusudiwa.

Alisema kuna watu wengi wanaojiita wawekezaji wako maeneo mengi na si mkoani Rukwa peke yake, ambao wamejichukulia maeneo hayo kwa kigezo cha jina la uwekezaji na matokeo yake nchi imekuwa na maeneo makubwa yasiyoendelezwa huku wananchi wa maeneo husika wakitaabika kwa kukosa ardhi.

"Serikali inayaona haya lakini imekaa kimya, hii ni dhambi inayohitaji kusahihishwa haiwezekani sehemu kubwa ya mashamba asilimia 70 nchini yaliyokabidhiwa kwa wawekezaji iwe haifanyiwi lolote, kwani kama wangefanya inavyokusudiwa kwa kuendeleza shughuli za kilimo Tanzania isingekuwa na njaa," alisema.

Kinana aliwahakikishia wakazi hao kwamba Tume ya Mkoa iliyoundwa kwa ajili ya kufuatilia suala hilo mapendekezo yake ambayo ni kutaka kurejeshwa kwa shamba hilo mikononi mwa wananchi na mwekezaji huyo kupatiwa sehemu kidogo yanafanyiwa kazi.

Kabla ya kuondoka mkutanoni hapo Kinana aliwatangazia wakazi hao kwamba tayari amezungumza na Rais Kikwete ambaye ameridhia shamba hilo lirejeshwa mikononi mwa wananchi ili waendelee na shughuli zao za kilimo.

1 comment:

Anonymous said...

Rais aagize kwani yeye ni mahakama? Acheni propaganda...