ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 1, 2014

UNAKUBALIKA KWENYE JAMII YAKO?

LEO kwenye Love & Life nitazungumzia jambo muhimu sana katika maisha yetu. Kwa wiki kadhaa mfululizo nimezungumzia zaidi mapenzi, hebu leo tugusie maisha kidogo. Ni kuhusu kukubalika kwenye jamii.

Watu wanakuchukuliaje mtaani kwako? Vipi kazini kwako una marafiki? Wanaokuzunguka wanakuonaje? Unakubalika? Ndugu zangu, kukubalika na watu unaoishi nao ni chachu ya maisha yako.

Kwa maneno mengine huwezi kufanya mambo yako kwa usahihi kama umezungukwa na watu wasiokukubali.

Kuna baadhi ya watu hujikuta wameingia katika vita ya majirani au wafanyakazi wenzake kwa mambo ambayo hayaeleweki hasa chanzo chake. Mwingine anafikia hatua anadhani amelogwa au anachukiwa na watu bila sababu.

Ndugu zangu, hakuna kitu kinachotokea pasipo kuwa na sababu. Kukubalika kutakufanya uishi kwa amani, ukijiamini na kuwa mwepesi wa kufiria na kufanya mambo ya maendeleo kwa haraka zaidi kwa vile huna shaka na jamii ya watu wanaokuzunguka.

KWANINI UTAFUTE KUKUBALIKA?

Kama nilivyosema awali, kukubalika ni muhimu. Unapokubalika unaishi ukiwa na uhakika wa kufanya mambo mengi na watu wakakuunga mkono. Mathalani, huwezi kuwa kiongozi kama watu hawakukubali. Kila unapopita watu wanakunyooshea vidole.

Taswira ya maisha yako, haiwezi kuwa sawa kama utakuwa si wa kukubalika katika jamii inayokuzunguka. Kwa maneno mengine, naweza kusema kwamba, ili uweze kuwa bora katika kila ukifanyacho katika jamii inayokuzunguka, kukubalika ni nguzo kubwa na muhimu.

KUNA HASARA GANI USIPOKUBALIKA?
Watu watakuogopa; Kwa kuwa watu wanakuogopa, unaweza kupitwa na mambo mengi. Hutapata marafiki na utatengwa katika jamii yako. Hapa hatari kubwa ni kwamba, utajihisi mpweke na pengine unaweza kufikiria labda huvutii au unakera watu.

Hata kama mwenzi wako ana tabia fulani mbaya, itakuwa vigumu watu kukuambia kwa sababu wanakuogopa. Ni vizuri sana kukubalika.

Utakosa faraja; Wakati mwingine unaweza kupata matatizo ya kawaida katika jamii, lakini watu wa kukufariji ukakosa kwa kuwa hawakukubali. Pengine unauguliwa, kuugua mwenyewe au matatizo mengine ya kibinadamu.

Utakosa misaada; Inawezekana ukapatwa na matatizo ya hapa na pale, pengine yakahusisha fedha, lakini kwa sababu hukubaliki, watu wakashindwa kukukopesha. Utabaki na shida zako mwenyewe, ukinung’unika na kuumia ndani kwa ndani lakini tatizo linabaki kuwa moja tu; kutokubalika.

Itaendelea wiki ijayo.

GPL

No comments: