Tuesday, May 20, 2014

Ban Ki Moon AIPONGEZA TANZANIA KWA ULIPAJI WA MICHANGO YAKE

Na  Mwandishi Maalum
Katibu  Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki  Moon, ametoa shukrani  na pongezi za pekee kwa nchi 29 kati ya 193  ambazo   hadi kufikia  Mei Sita mwaka huu,  zilikuwa  zimelipia kwa ukamilifu  na kwa wakati michango yake katika Umoja wa Mataifa.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya nchi hizi ambazo katibu Mkuu amezipongeza.
Tanzania  imelipa zaidi  ya  dola za kimarekani 450,000 kama sehemu ya michango   yake kwa Chombo hicho cha Kimataifa. Na kwa miaka mitano mfulululizo  imekuwa ikilipa kwa wakati na kwa ukamilifu.

Kwa Tanzania  kulipitia michango   siyo tu  kwamba,  ni kielelezo cha uwajibikaji kama nchi mwanachama,   lakini pia   ni utekelezaji wa utawala bora na ni heshma kwa taifa mbele ya   Jumuiya ya Kimataifa.
Pongezi za  Ban ki Moon kwa nchi hizo zimo katika taarifa yake kuhusu hali Fedha katika Umoja wa Mataifa. Taarifa  hiyo iliyowasilishwa na kisha kujadiliwa na Wajumbe wa Kamati ya Tano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya Utawala na Bajeti ya  Umoja wa Mataifa.
Katibu Mkuu amezitaka  nchi nyingine  kuiga  mfano wa nchi  hizo kwa kile alichosema   hali nzuri ya fedha ya  Taasisi hiyo ya Kimataifa pamoja na uendeshaji wa shughuli zake,  unategemea sana michango ya wanachama wake, michango inayotakiwa kutolewa kwa wakati na kwa ukamilifu.
Kila nchi mwanachama hutakiwa kulipa kiasi cha michango katika bajeti za Umoja wa Mataifa kutokana na uwiano wa uchumi wake katika dunia kama ilivyoainishwa katika Katiba  ya Umoja wa Mataifa.
Bajeti za Umoja wa Mataifa kwa mwaka ni zaidi ya bilioni 10 zikijumuisha bajeti ya Kawaida, bajeti za misheni za kulinda Amani na  mahakama za kimataifa za makosa ya Jinai. Pia kuna bajeti za miradi maalum kama ukarabati wa  Jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kiasi cha dola 2 bilioni kwa mradi wote.
Nchi nyingine ambazo  zimekwisha kulipia michango yake ni    Australia,  Austria,  Brunei Darussalam  Canada, Denmark, Equatorial Guinea, Finland, Hungary, Germany,  Iceland, Israel,  Japan, Latvia,  Liechtenstein  na  Netherlands

Nyingine ni  New Zealand, Norway,  Samoa, Senegal, Singapore,  Sweden, Switzerland, Timor-Lester, Turkmenistan, , Georgia, Kenya na Jamhuri ya Korea.

No comments: