Friday, May 30, 2014

HIVI UNAMNYIMA NINI, UMEBADILIKAJE MPAKA AKUSALITI?


Kesi za wapenzi na wanandoa kusalitiana zimekuwa zikiongezeka kila kukicha. Uaminifu umekosekana baina ya wale wanaodai wanapendana kiasi kwamba hakuna anayeweza kusimama na kusema kuwa, hasalitiwi.

Utafiti unaonesha kwamba, hata wale ambao wanajiaminisha kuwa wapenzi wao ni watulivu wasio na mawazo ya kuchepuka, wamekuwa wakizungukwa bila wao kujua.
Si hivyo tu, wapo ambao wanajua wazi kwamba wapenzi wao hawajatulia lakini ili kutojipa presha za bure wanaziba masikio.

Kinachonishangaza zaidi ni kwamba, wapo wanawake ambao wanajinadi kwamba, wanajitahidi kuwapa waume zao kila kitu ili kuwabana wasitoke nje lakini mwisho wa siku wanasalitiwa. Hapo ndipo baadhi wanapochanganyikiwa na kugundua kuwa, kusaliti ni hulka ya mtu.

Hii inamaanisha kwamba, hata mwanamke ajitahidi vipi, kama mume ni kiwembe atatembea na wanawake wengine tena baadhi yao wakiwa hawana hata hadhi yake.

Jiulize ni wanawake wangapi wamewafumania waume zao na machangudoa wachafu ambao kujiuza imekuwa ndiyo maisha yao ya kila siku? Ni wake za watu wangapi ambao wamewafumania wenza wao na mahausigeli?

Matukio hayo yamekuwa yakitokea sana kwenye jamii yetu. Swali ambalo mwanamke anatakiwa kujiuliza ni kwamba, je, kuna kitu chochote mume anaweza kuwa anakikosa ndani ya ndoa mpaka afikie hatua ya kuchepuka?

Mimi leo nitawalaumu baadhi ya wanawake kwa kuwashawishi waume zao kutoka nje ya ndoa. Amini usiamini wapo wanawake ambao kwa kujua ama kutojua wamekuwa wakifanya mambo ya wazi ambayo huwafanya waume zao kuangalia mwanamke mwingine wa kumpa raha.

Najua wapo wanaume wakorofi, wasioridhika na mapenzi wanayopewa na wake zao, wenye tamaa za kijinga, wasioona aibu kutembea hata na vibinti vidogo. Ukibahatika kuingia kwenye maisha ya ndoa na mwanaume wa sampuli hii, hata ufanyeje, huwezi kuepuka kusalitiwa. Kwa maana hiyo utaamua aidha kuvumilia ama kuachana na mtu huyo.

Lakini tatizo lipo kwa baadhi ya wanawake ambao wanashindwa kuzilinda ndoa zao. Wao hawajali, wanaishi ilimradi siku zinakwenda na wala hawafikirii namna ya kuboresha ndoa zao.

Wapo wanawake ambao ni wababe na mbaya zaidi ubabe wao wanauonesha hadi kwa waume zao. Mke anakuwa si msikivu, haoni hatari kujibishana na mumewe. Huyu hawezi kumshika mumewe, anakuwa ni sawa na kuku anayemsukumia mwanaye kwa kipanga.

Mwanamke asiyejua majukumu yake kama mke ni tatizo pia. Mume anastahili kupatilizwa katika haki zake za kindoa na kubwa zaidi ni pale kwenye faragha.
Ukifuatilia sana utabaini kuwa, wanaume wengi wanaochepuka sana kuna kitu wanachokikosa kwa wake zao ikiwa ni pamoja na penzi la dhati.

Kwa mfano unaweza kukuta mke hajui kabisa ‘mambo’ yetu yalee, ni mchafu asiyemvutia mumewe lakini pia ni mtu asiyependa kujifunza na kubadilika.
Niwakumbushe tu wanawake kwamba, ulimwengu wa sasa umebadilika sana. Wapo wasichana huko mtaani ambao ni kama fisi wanaosubiria mizoga. Yaani wao wanadili na waume za watu wasiopatilizwa na wake zao.

Wakigundua wamemnasa mwanaume ambaye hapatilizwi na mkewe basi watatoa mahaba yaliyoshiba na matokeo yake ndiyo unasikia mume katelekeza familia, kahamia kwa nyumba ndogo.
Mimi nadhani mwanamke aliyekamilika ni yule ambaye kila wakati anaifanyia tathmini ndoa yake. Analinganisha mapenzi ya zamani na ya sasa. Anaangalia mwenendo wa ndoa na kipi akikifanya atazidi kufurahia maisha.

Kwa maana hiyo kama utahisi au kugundua kuwa unasalitiwa, ni vyema ukajiangalia na kujiuliza sababu za mumeo kuanza kuchepuka. Je, kuna sehemu unakosea? Kuna kitu zamani ulikuwa unamfanyia sasa hivi unamnyima? Ni vizuri ukapata majibu ya maswali haya.

Ifike wakati uumize akili yako ya kutafuta anachokikosa kwako mpaka aamue kukusaliti. Ukigundua kuwa unampatia kila anachostahili kwa ukamilifu lakini yeye anachepuka, basi huyo ni wale wanaume malimbukeni wasiotosheka hivyo anakuwa hana vigezo vya kuendelea kuwa mumeo.

GPL

No comments: