Tuesday, May 20, 2014

KIGOGO WA POLISI ALIYEANGUSHA GARI SASA NI BALAA TUPU


Kamanda wa polisi Mkoa wa Geita Kamishina msaidizi wa polisi Joseph Konyo.


Siku chache baada ya mkuu wa polisi wilaya ya Geita Mrakibu mwandamizi wa polisi Sadock Busee Bwire kuangusha gari la polisi PT 1998 alilokuwa analiendesha,na kuamriwa na Kamanda wa polisi Mkoa wa Geita Kamishina msaidizi wa polisi Joseph Konyo alitengeneze kwa pesa zake kwa madai  kuwa kwa cheo chake hatakiwi kuendesha gari la polisi.

OCD Bwire ameanza kutembeza bakuli kwa wakuu wa vituo vya nje wilayani Geita akiwataka kila mkuu wa kituo kuchangia fedha kiasi cha Tsh.150,000/= kwa ajili ya matengenezo ya gari hilo ambalo inasemekana imeharibika engine yake

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakuu wa vituo  vya Butundwe,Katoro,Mgusu,Nyarugusu,Kasamwa,Lwamgasa,Nyamboge,Nzera,na Nyakagwe wamelalamikia hatua hiyo ya Ocd kuwaamuru kuchangia gharama za matengenezo ya gari hilo

“huyu ocd wetu simuelewi anatuambia tuchangie hela sisi tunapata wapi?au ndio kusema anatuagiza tuwaonee wananchi ili tupate hela ya kumpa? Alihoji mmoja wa wakuu wa vituo


Awali akizungumzia ajali hiyo Kamanda Konyo alisema Ajali hiyo ilitokea Mei 7 mwaka huu usiku saa 2 katika kijiji cha Bufunda tarafa ya Busanda ikiwa imebeba watuhumiwa wa makosa mbalimbali  huku baadhi ya watuhumiwa wakitoroka,chanzo cha ajali hiyo licha ya kufichwa imeelezwa kuwa ni mwendo kasi wa dereva wa gari hiyo.

Aliwataja watuhumiwa waliotoroka kuwa ni William Michael,Charles Julius,Mussa Mashiri,Joseph John,Nelson Raphael,na Sued Omary wote wakazi wa Nyarugusu.

Aidha Kamanda Konyo alisema kuwa kwa mujibu wa kanuni na sheria za polisi “Police General Order” mkuu wa polisi wa wilaya ana dereva wake haruhusiwi kuendesha gari la polisi isipokuwa la kwake binafsi.

Aliongeza kuwa askari mmoja kati ya watatu aliyejulikana kwa jina la Konstebo Linus wa kituo cha polisi Nyarugusu alijeruhiwa baada ya meno yake mawili kung’oka na kulazwa katika hospitali ya wilaya kwa matibabu.

Kaimu mganga mkuu wa hospitali ya wilaya Dk.Adam Sijaona alikiri kulazwa kwa askari huyo na kudai hali yake inaendelea vizuri.

Aidha askari polisi wa kituo kikuu cha Geita wamekuwa wakimtuhumu mkuu wa polisi huyo wa wilaya kwa madai kuwa anashirikiana na wafanyabiashara wa magendo hasa wa mkaa,na pombe kali aina ya viroba zinazoingizwa kinyume nchini kutoka nchini Uganda.

Wamedai kuwa baada ya kuwakamata wafanyabiashara hao ambao ni maswahiba wa Ocd wakisafirisha magendo na kuwafikisha mahakamani,Ocd huyo ameamua kuwachongea uhamisho na kupelekwa wilaya za Nyang’wale Chato na Mbogwe,uhamisho ambao wameuita ni wa fitina wala sio wa haki.

Wameeleza kuwa licha ya gari ya polisi kuangushwa na kuharibiwa hakuna jalada lililofunguliwa kituoni hapo na haikukaguliwa na mkaguzi wa magari kama taratibu zinavyoelekeza na badala yake ilifichwa kwenye gereji bubu ili kuficha ukweli,hali ambayo imezua hofu kwa askari aliyeumia kuwa atakosa haki zake .

Jitihada za kumpata mkuu wa polisi wa wilaya Sadock Busse Bwire  kujibu tuhuma zinazomkabili hazikuzaa matunda,baada ya simu yake kuita kwa muda mrefu bila kupokelewa,na alipotumiwa ujumbe wa maneno hakujibu.

Kamanda wa polisi mkoa wa Geita  Kamishina msaidizi wa polisi Joseph Konyo alipoulizwa hatua ya wakuu wa vituo kuamriwa kuchangia gharama za matengenezo ya gari hiyo,alidai hawalazimishwi na wala hakuna sheria inayowabana  wasipochangia,alidai kuwa analifuatilia  suala hilo na baada ya hapo atalitolea ufafanuzi.

Na Valence Robert wa Malunde1 Blog- Geita

No comments: