ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 30, 2014

Kingunge aikejeli CCM

  Asema haileti mabadiliko ya kiuchumi
  Ainanga kwa kung'ang'ania madarakani
  Kinana aelezwa agizo la JK linavyopuuzwa
Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngomale-Mwiru amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama ilivyo kwa vyama vingine vya siasa nchini, hakina malengo ya kuleta ukombozi wa kiuchumi, badala yake kinapigania kubaki madarakani.

Amesema, wakati CCM ikiwa katika kupigania kubaki madarakani, wapinzani kwa upande wao wanaendeleza zaidi nia ya kutaka kuingia Ikulu badala ya kushughulikia uchumi wa nchi.

Kingunge, alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, alipozindua kitabu cha mwongozo kwa vyama vya siasa katika ngazi za msingi wakati wa mkutano uliandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania(TCD).Alisema, vyama hivyo vinaendekeza malumbano yanayovifanya visahau mambo ya msingi ya kitaifa.

Kingunge, alisema katika hatua za awali za kuanzishwa kwake, CCM ilijua hitaji la msingi kwa umma lakini hivi sasa, kinang`ang`ania zaidi kupambana kwa lengo la kubaki madarakani na kusahau
majukumu yake kwa taifa.

“Mimi nasema kizazi cha sasa ni tofauti na kizazi chetu, CCM ya zamani na sasa ni tofauti,” alisema.

“Kwa namna hii, nchi haiwezi kupiga hatua ya kimaendeleo. Sisi wa zamani tulikuwa tunajua nini tunakifanya kwa sababu tulikuwa tunapigania kwa hali na mali masuala ya kuwaletea maendeleo wananchi wetu tofauti na ilivyo sasa,” alisema.

Kingunge, alitoa mfano wa kuwapo nchi nyingine zinazopiga hatua kiuchumi, kwa kuwa demokrasia zao zimelenga kupigania maslahi ya wananchi.

Alisema kwa hali hiyo, vyama vya siasa katika nchi hizo (hakuzitaja) vimekuwa vikiendesha siasa zao zikiwa zinatambua nini zinafanya.

Kadhalika, alisema nchi hii bado inahitaji ukombozi wa kiuchumi hivyo ni vema viongozi wa siasa wakalenga kujadili namna wanavyoweza kuwakomboa wananchi na wimbi la umaskini badala ya kuendelea kulumbana na kupigania Ikulu.

Alikitaka kila chama kukaa na kutafakari namna bora ya kuwakomboa wananchi, ikiwa ni pamoja na kubadili mfumo wa siasa na hoja za msingi kwa maslahi ya umma.

AGIZO LA JK LINAVYOPUUZWA
Wakati huo huo; Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrhaman Kinana ametaka nyumba sita za madaktari wa serikali zilizouzwa, zirejeshwe kama Rais Jakaya Kikwete alivyoagiza mwaka 2011.

Kinana alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Mbulu mkoa wa Manyara na kusisitiza kuwa haikuwa sahihi nyumba hizo kuuzwa.

Kauli ya Kinana ilitokana na taarifa iliyotolewa na uongozi wa hospitali ya wilaya ya Mbulu, kuwa pamoja na kuuzwa kwa nyumba hizo ambazo idadi yake haikutolewa, bado wanunuzi walijiongezea ‘kinyemela’ ukubwa wa eneo kutoka ekari moja kufikia tano.

Uongozi huo ulisema hali hiyo ilisababisha hospitali kutokuwa na ardhi kwa ajili ya kujenga majengo ya huduma za afya.

"Kuna watu wameuziwa nyumba za madaktari ki-makosa kisha wakajiongezea ukubwa wa maeneo, huo ni wizi haiwezekani mali ya serikali ichezewe na wachache, lazima ardhi hii irudishwe," alisema Kinana.

Alisema kazi ya CCM ni kujikosoa pale kilipokosea na siyo kujisifia peke yake na kwamba hakuna sababu ya kusema ilikuwa sera wakati Watanzania wanakosa huduma bora za afya.

"Lazima upungufu wetu tuuseme tulikosea, tukubali yapo mambo ya ovyo kama haya ya nyumba za umma kuuzwa. Matokeo yake hospitali ya Mbulu wanataka kuongeza majengo hakuna ardhi, nyumba zilizopo za madaktari zimeuzwa, hapa lazima tukubali tulikosea,"alisisitiza Kinana.

Sambamba na hilo Kinana alisema namefurahishwa na utekelezwaji wa ahadi za Rais Jakaya Kikwete kwa hospitali ya Hydom kuifanya kuwa ya Rufaa.

Alisema serikali inatoa dawa na vifaa tiba na kuajiri sehemu ya watumishi, ambazo zote zilikuwa ahadi za Rais Kikwete, sasa zimetekelezwa huku akiweka wazi kuwa uongozi wa hospitali hiyo umeomba serikali kuajiri watumishi wengi zaidi.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: