ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 1, 2014

Mfanyakazi afariki kiwanjani kwenye maadhimisho Mei Mosi, Dar

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa kashikana mikono na viongozi wa serikali na wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) huku wakiimba wimbo wa wafanyakazi katika kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani (MEI MOSI) leo Mei 1, 2014 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. (picha: IKULU)


  • Rais Kikwete aongoza maadhimisho ya Mei Mosi 
  • Aahidi mishahara kupanda, P.A.Y.E kushuka
  • Mfanyakazi wa Ikulu apoteza uhai kiwanjani

Habari kwa mujibu wa Lukwangule blog zinasema kuwa Rais Jakaya Kikwete, amewaahidi wafanyakazi nchini kuwa mambo mazuri yakiwemo ya kupanda kwa mishahara na kupunguzwa kwa kodi ya mishahara maarufu kama P.A.Y.E.

Akihutubia kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Dar es Salaam leo, Rais Kikwete amesema:
“Najua hiki ndio kilio chenu na wote mnasubiria kwa hamu Serikali inasema nini? Nawaahidi kuwa katika hotuba ya Bajeti Waziri wa Kazi na Ajira, itabainisha wazi, kiwango cha mshahara ambacho Serikali imekiongeza katika mishahara ya wafanyakazi,” alisema Rais Kikwete.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipungia mkono waandamanaji aliowapokea katika kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani (MEI MOSI) leo Mei 1, 2014 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akiwa mwingi wa furaha, Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea waandamanaji katika kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani (MEI MOSI) leo Mei 1, 2014 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. (picha: IKULU)

Hata hivyo, alisema Serikali haitoweza kupandisha mishahara hiyo na kufikia ombi la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA),  la Sh 750,000.

Pamoja na hayo, Rais Kikwete alionyesha kutoridhishwa na namna sehemu kubwa ya sekta binafsi, isivyozingatia viwango vya mishahara vinavyopangwa na Serikali, hali inayochangia kuibuka kwa migogoro ya mara kwa mara baina ya waajiri na waajiriwa.

Akizungumzia suala la Kodi ya Mapato (P.A.Y.E), Rais Kikwete, alisema ombi hilo nalo kama ilivyo nyongeza ya mishahara ni la muda mrefu, na kuwaahidi wafanyakazi hao kuwa nalo linafanyiwa kazi ili kupunguza kutoka asilimia 13 inayotozwa kwa sasa na kufikia tarakimu moja.

Naye Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, alimpongeza Rais Kikwete kwa kupatiwa tuzo ya utawala bora Afrika, na kuwataka waajiri nchini kutumia fursa hiyo kumuenzi kiongozi hiyo kwa kuhakikisha wanafuata nyayo na kusimamia utawala bora, ili kupunguza migogoro ya kazi.

Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya, akiwasilisha risala ya wafanyakazi katika maadhimisho hayo, aliiomba Serikali ishughulikie matatizo yanayowakabili wafanyakazi ya uboreshaji wa mishahara, kupunguzwa kwa kodi ya P.A.Y.E na kuboreshewe pensheni.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipungia mkono maandamano ya magari aliyoyapokea katika kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani (MEI MOSI) leo Mei 1, 2014 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. (picha: IKULU)

Wafanyakazi Bora kutoka idara na taasisi mbalimbali wakimsikiliza Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia katika kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani (MEI MOSI) leo Mei 1, 2014 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. (picha: IKULU)

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia katika kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani (MEI MOSI) leo Mei 1, 2014 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. (picha: IKULU)

Taarifa kwa mujibu wa Mwandishi wa TheHabari inasema kuwa maadhimisho hayo maarufu kama Mei Mosi yameingia dosari baada ya mmoja wa wafanyakazi kufariki dunia uwanjani kwa ghafla akiwa katika maadhimisho hayo jijini Dar es Salaam.

Mfanyakazi huyo anayedaiwa kufanya kazi Ikulu alizidiwa ghafla akiwa katika maandamano na kupatiwa huduma za kwanza lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya na hatimaye kudaiwa kupoteza maisha wakati akipatiwa huduma na madaktari na wahudumu kutoka kikosi cha msalaba mwekundu waliyokuwa katika maadhimisho hayo.

Thehabari.com ilishuhudia mfanyakazi huyo akiletwa katika kambi ya watu wa huduma ya kwanza iliyokuwa katikati ya uwanja wa Uhuru, kisha kupatiwa huduma ya kwanza bila mafanikio na baadaye alifariki dunia. Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika kundi ambalo lilimleta mfanyakazi huyo baada ya kuzidiwa ghafla lilimtaja kuwa jina lake ni Rashid John Chilwangwa.

Baadhi ya jamaa aliyoambatana nao wakimwangalia mara baada ya kufikishwa chumba cha huduma ya kwanza. (picha: The Habari)

Mmoja wa wafanyakazi waliyokuwa wameandamana na mfanyakazi huyo ambaye hakupenda kutaja jina lake kwa kuwa yeye si msemaji akisimulia tukio hilo, alisema John Chilwangwa (45) walikuwa naye katika sherehe za maadhimisho na hali yake ilibadilika kabla ya kuingia uwanjani na aliomba aende kujisaidia haja ndogo baada ya hapo alianza kuishiwa nguvu.

“…Si tulishangaa alikaa muda kidogo akijisaidia baada ya kumfuata tulimkuta ametoka ndani ya choo na kuja nje na kisha kukaa kwenye tofali huku akisema anajisikia kuishiwa nguvu na hali ilibadilika ndo tukamleta hapa,” alisema shuhuda huyo.

Alipoulizwa hali yake kwa sasa ambapo alikuwa ameingizwa kwenye hema la huduma ya kwanza kwa wahudumu kutoka kikosi cha msalaba na madaktari alisema wamejaribu kumuhudumia lakini bahati mbaya amefariki dunia tayari. 
“…Tumeambiwa na madaktari kuwa ameshafariki tayari,” alisema shuhuda huyo ambaye alikuja na mgonjwa huyo.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia madaktari wakijaribu kumtundikia dripu huku wakijaribu kurudisha mapigo ya moyo kwa kushtua mara kadhaa lakini juhudi ambazo hazikuzaa matunda. Baada ya kubaini amefariki dunia walisita kumwekea dripu ambayo ilikuwa inaandaliwa na badaye walimfunika kwa shuka nyeupe na kuita gari la wagonjwa tayari kwa kumpeleka hospitali kwa uchunguzi zaidi. Hata hivyo hakupatikana mara moja daktari kuzungumzia kilichomsibu Chilwangwa.

2 comments:

Anonymous said...

Ni aibu katika sherehe kubwa namna hii, mtu aanguke asipate huduma ya kwanza inayotakiwa hadi kufikishwa hospitalini amefariki muda mrefu!! Kwani wahudumu wa msalaba mwekundu au kikundi cha uokoaji kimepata utaalamu wa huduma ya kwanza akiwa anawahishwa hospitalini! Tuepusheni majanga kama haya kuendelea kutokea..

Anonymous said...

majanga yataendelea kuwepo kama bado mnawachagua hawa mafisadi wa ccm changueni vyama vya upinzani kila siku kweli wewe unakula wali mweupe kwa nini usibadilishe mapishi kula leo pilau kesho wali wa vegetable na kuku wakuchoma au samaki wa kupaka na kesho kutwa chapati nyama kavu kavu ,mchuzi wa bilinganya wa chuku chuku unaonaje badilisheni mapishi

ccm msiwachague wanakudhalilisheni hata huduma ya kwanza hawana kazi kunufaisha matumbo yao na family zao