Wakuu wa Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wakizindua kitabu rasmi cha Muongozo wa Majaji wa Jumuiya hiyo kwenye Mkutano wa 12 wa siku moja wa Jumuiya hiyo uliofanyika ukumbi wa Kimataifa wa Arusha { AICC }.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa niaba yaRais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Sheni akipokea kitabu wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mkoani Arusha.
Baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania waliohudhuria Mkutano wa 12 wa Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki huko Arusha. Wa mwanzo kutoka kushoto ni Waziri wa Ardhi wa SMZ Mh. Ramadhan Abdulla Shaaban, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Mh. Benard Membe na Waziri wa Afrika Mashariki Mh. Joh Samuel Sitta.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Uhuru Kenyeta wa Kenya akihutubia Mkutano wa 12 wa Jumuiya hiyo Mkoani Arusha.
Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakisaini baadhi ya hati za makubaliano ya Jumuiya hiyo. Kutoka kulia ni Rais Wa Uganda Yoweri Museveni, Rais wa Kenya ambae ndie Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Rais Uhuru Kenyata, Rais wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Burundi Bwana Bazombaza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Wakuu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wakiimba wimbo Maalum wa Jumuiya hiyo kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 12 wa Jumuiya hiyo uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha { AICC }.
Majaji wapya walioapishwa kushika nyadhifa mbali mbali kwenye Mkutano wa 12 wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mkoani Arusha. Kutoka Kushoto ni Jaji Edward Mtakangwa, Dr. Anon Regerwa na Jaji Fakih Jundu.
Viongozi wa Mtaifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakilizindua Mnara wa kumbumbuku ya mauaji ya Rwanda yaliyotokea karibu miaka ishirini iliyopita hapo Makao Makuu ya Jumuiya hiyo Arusha Tanzania.vKutoka kushoto ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Burundi Bwana Bazombaza, Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, Rais wa Kenya mabae pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Rais Uhuru Kenyata, Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Waziri Mkuu wa Rwanda Bwana PierreDamieni Habumuryemi.
Wakuu waJumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 12 wa Jumuiya hiyo Mkoani Arusha Tanzania.Kutoka Kushoto waliokaa vitini ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Burundi Bwana Bazombaza, Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Rais wa Kenya Uhuru Kenyata, Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Waziri Mkuu wa Rwanda Bwana Pierre Damieni Habumuryemi.
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete akiwapongeza Majaji wapya wa Mahkama ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki waliokula kiapo kwenye Mkutano wa 12 wa kuitumikia Jumuiya hiyo Mkoani Arusha. Nyuma yake ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame
Mataifa wanachama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yanapaswa kuzingatia umuhimu wa ulinzi wa pamoja wa eneo lote la Afrika ya Mashariki kwa lengo la kujaribu kudhibiti vitendo vya ugaidi vinavyoonekana kujitokeza katika baadhi ya Nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Uhuru Kenyata wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya alieleza hayo wakati akiuhutubia Mkutano wa 12 wa siku moja wa Viongozi Wakuu wa Jumuiya hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Arusha (AICC).
Rais Uhuru Kenyata alisema Mataifa ya Afrika Mashariki hasa pembe ya Bara hilo imekumbwa na wimbi la vitendo vya kigaidi kiasi kwamba huleta hali ya wasi wasi kwa wakaazi wa eneo hilo. Alisema ukosefu wa utulivu katika baadhi ya maeneo ndani ya ukanda wa Bara la Afrika umekuwa ukiipa wakati mgumu jumuiya hiyo kiasi kwamba Mataifa wanachama yanalazimika kufanya kazi kwa pamoja ili kukabiliana na tatizo hilo.
“Ukanda wa Afrika Mashariki umekuwa ukikumbwa na vitendo vya kiharamia pamoja na ugaidi jambo ambalo halileti sura nzuri kiasi kwamba huchangia hali ya wasi wasi kwa wana Jumuiya wote “. Alifafanua Rais Uhuru Kenyata.
Akizungumzia suala la kuwa na Ushuru wa Forodha na Soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya hiyo Rais Kenyata alisema upo muelekeo mzuri wa suala hilo ambalo linaonekana kupewa Baraka na Viongozi wa Mataifa wanachama.
Rais Uhuru Kenyata alifahamisha kwamba taratibu na mikakati ya kisheria imekuwa ikiendelea kuchukuliwa na watendaji pamoja na Wataalamu wa Jumuiya hiyo ili kuona suala hilo linafikia muwafaka.
Alieleza kuwa juhudi za kuwa na ushuru wa forodha na soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki zilizoanza harakati zake kati ya mwaka 2005, 2010 na 2013 zimelenga kustawisha hali ya uchumi ya wananchi wa mataifa shirika wa Jumuiya.
Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki { EAC } aliipongeza Tanzania kwa kuadhimisha miaka 50 ya Muungano ulioasisiwa na Mataifa mawili huru ya Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.
Rais Kenyata alisema kwamba Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa kielelezo cha kihistoria ndani ya Bara la Afrika pamoja na Mabara mengine Duniani. Alieleza kwamba Afrika Mashariki na Bara zima la Afrika limepata heshima kubwa katika Nyanja za kisiasa kutokana na Muungano wa Tanzania uliofikia nusu karne sasa tofauti na ile miungano mengine iliyoshindwa kumudu hata kwa miezi michache.
Mapema Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Balozi Dr. Richard Sezibera ameishukuru Tanzania chini ya Rais wake Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kwa ukarimu wa Wananchi wake. Balozi Dr. Richard Sezibera ukarimu huo unaoendelea kuviwezesha vikao mbali mbali vya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanyika kazi zake za kila siku Ndani ya ardhi ya Tanzania.
Katika Mkutano huo wa 12 wa Viongozi Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Majaji Watatu waliapishwa kushika nyadhifa mbali mbali katika baraza la Majaji la Jumuiya hiyo.
Majaji hao ni pamoja na Mh. Edward Mtakangwa, Dr. Aron Regerwa, Jaji Fakih Jundu akiwemo pia Dr. Enos Bukuku aliyeongezewa muda wa kuendelea kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki.
Halkadhalika Viongozi hao Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa pamoja pia walizindua Mnara wa kumbumbuku ya mauaji ya Rwanda yaliyotokea karibu miaka ishirini iliyopita.
Mkutano huo wa 12 wa Viongozi wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umehudhuriwa na Rais Uhuru Kenyata wa Kenya ambae ndie Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni pamoja na Mwenyeji wa Mkutano huo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete.
Wengine ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Burundi Bwana Bazombasa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyemuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohd Sheni pamoja na Waziri Mkuu wa Rwanda Bwana Pierre Damieni Habumuryemi.
No comments:
Post a Comment