Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda akimpongeza Askofu Conrad Ernest Nguvumali baada ya kuwekwa wakfu kuwa Askofu wa Kanisa la Moravian Jimbo la Rukwa ibada iliyofanyika kwenye uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga.
Sumbawanga. Mwanasiasa mkongwe nchini, Dk Chrisant Mzindakaya amekataa hadharani mbele Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ombi la Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya kumsamehe Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Aeshi Hilaly.
Tukio hilo lilitokea jana kwenye ibada ya kusimikwa Askofu wa Kanisa Moravian Jimbo la Rukwa, Cornad Nguvumali iliyofanyika kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na madhehebu ya Kikristo nchini.
Manyanya aliwaita jukwaani akitaka washikane mikono ili kuzika tofauti zao za kisiasa zilizodumu kwa muda mrefu tangu Hilaly alipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Dk Mzindakaya alisema alipoombwa na Waziri Mkuu kutoa msamaha kwa Hilaly alitoa utaratibu wa kutumika kupitia vikao vya kichama ikiwa pamoja kuitishwa vikao kwa maeneo yote ambayo mbunge huyo alifanya mikutano na kuchafua heshima yake.
“Sasa mie ni mtu mzima nafasi ya msamaha inahitaji kuandaliwa, sijaandaliwa kiroho kwa ajili ya jambo hili... tayari nilitoa utaratibu kwa wazee wa chama watuite mimi na kijana wangu, nipo tayari kumsamehe lakini hapa si mahali pake, hapa ni sehemu ya kidini, siyo kuleta siasa hapa na nikisema hapa nitakuwa juha” alisema Dk Mzindakaya.
Manyanya akiri kutowashirikisha wanasiasa hao kwenye jambo hilo akidai kutoridhishwa na jinsi wasivyoelewana kitu ambacho kinatia doa uhusiano wa kawaida wa watu hao na jinsi ambavyo hawashirikiani kwenye mambo ya msingi ya maendeleo ya Mkoa wa Rukwa.
Mkuu huyo wa Mkoa alianza kwa kumsimamisha Hilaly katika hadhara hiyo na mwanasiasa huyo alikiri kuwapo misuguano baina yake na Dk Mzindakaya kwa kipindi kirefu sasa na kuibua makundi ndani ya CCM huku akimtaka Mzindakaya amsamehe mbele ya hadhara hiyo.
“Siku zote tunatofautiana mimi na mzee wangu lakini hakuna marefu yasiyo na ncha... Mzee wangu Mzindakaya najua nilikukosea au inawezekana wewe ulinikosea lakini ya kale si ndwele tugange yajao naomba unisamehe. Mimi nimetamka hapa mbele ya Mungu na kuna viongozi wa dini,” alisema Hilaly.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa ugomvi baina ya wanasiasa hao unachagizwa na mambo kadhaa ikiwemo kile kinachoelezwa Dk Mzindakaya kutomuunga mkono Hilaly wakati wote wa kampeni za uchaguzi.
Kingine ni mbunge huyo kuhoji bungeni uhalali wa Kampuni ya Sumbawanga Agriculture and Animal Food Industries Ltd (Saafi), kupangishwa nyumba 12 na Serikali kwa gharama nafuu lakini nayo ikazipangisha kwa gharama ya juu kwa kampuni moja ya ujenzi wa barabara.
Baada ya Hilaly kuhoji, Ofisi ya Wakala wa Majengo Mkoa wa Rukwa, ilitoa notisi ya siku 30 kwa kampuni ya Saafi inayomilikiwa na Dk Mzindakaya kukabidhi nyumba zote 12 zilizoko eneo la Norad.
Pia mbunge huyo aliibana Serikali bungeni akihoji kuhusu mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kawa lililopo katika Ranchi ya Nkundi chini ya Dk Mzindakaya itoe maelezo ya kina ni kwa nini imetumia fedha zake Sh1.09bilioni kujenga mradi huo ambao umekuwa hauna manufaa kwa wananchi kwa kuwa wanakatazwa kuingia kutumia maji hayo.
Akizungumza katika ibada hiyo, Pinda ambaye hakugusia kabisa suala hilo aliwataka viongozi wa dini kuwapa uhuru waumini wao kuwa na mapenzi na vyama vya kisiasa wanavyotaka lakini wasifuate misimamo ya nyumba zao za ibada.
“Kuna viongozi wanawanyima waumini wao uhuru wa kupenda chama cha siasa anachotaka... kila muumini awe na uhuru wa kuchagua chama anachotaka, siyo kulazimishwa kufuata msimamo wa kanisa,” alisema Pinda.
MWANANCHI

No comments:
Post a Comment