
Mhe. Bernard Membe
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe.
Bernard K. Membe (Mb) atafanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini Uturuki
kuanzia tarehe 07 – 09 Mei, 2014 kufuatia mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi
hiyo, Mhe. Ahmet Davutoglo. Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza na kuimarisha
ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki ambao umedumu kwa kipindi kirefu sasa.
Aidha, katika ziara hiyo
Mhe. Membe na mwenyeji wake watajadili umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati
ya Tanzania na Uturuki hususan, katika maeneo ya vipaumbele yaliyoainishwa
katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Afrika na Uturuki uliofanyika mwaka 2008.
Maeneo hayo ni pamoja na biashara, uwekezaji, kilimo, mawasiliano, afya, elimu pamoja
na amani na usalama.
Katika ziara hiyo, Mhe.
Waziri ataonana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Uturuki akiwemo
mwenyeji wake, Mhe. Davutoglo; Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Emrullah Isler; Waziri
wa Uchukuzi, Usafiri wa Majini na Mawasiliano, Mhe. Lutfi Elvan; Waziri wa
Nishati na Maliasili, Mhe. Tarrer Yildiz pamoja na kuongea na wafanyabiashara
wa Uturuki.
Katika ziara hiyo, Mhe.
Waziri atafuatana na viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa; Wizara ya Viwanda na Biashara; Wizara ya Kilimo,
Chakula na Ushirika; Mamlaka ya Majengo Tanzania na Mamlaka ya Ukanda Maalum wa
Uwekezaji (EPZA).
Imetolewa
na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es salaam.
6 Mei 2014.
No comments:
Post a Comment