Wednesday, May 21, 2014

Ukawa wang`ang`ania

  Watoa masharti ya kurudi bungeni
Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),vimetoa sharti kwamba vitakuwa tayari kurejea katika Bunge Maalum la Katiba iwapo Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba iliyokuwa na pendekezo la muundo wa Serikali tatu ndiyo itakayojadiliwa katika bunge hilo.

Msimamo huo ulitolewa kwa nyakati tofauti katika mikutano ya hadhara mjini Tarime, mkoani Mara na mjini Songea, Ruvuma ukiwa ni mfululizo wa viongozi wa Ukawa wanaotembelea katika mikoa 17 nchini kuwaelimisha wananchi umuhimu wa katiba mpya.

Mjini Tarime, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, alisema wabunge na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotoka Ukawa watakuwa tayari kurejea katika Bunge hilo kama rasimu ya Jaji Warioba yenye pendekezo la serikali tatu ndiyo itakayojadiliwa na si vinginevyo.

Dk. Slaa alisema Ukawa inasimamia maoni ya wananchi ambao walipendekeza muundo wa serikali tatu, kwa hiyo haitakuwa tayari kukubali usaliti unaotaka kufanywa na CCM wa kutaka muundo wa serikali mbili wakati muundo huo haupo kwenye rasimu ya iliyoandaliwa na Tume ya Jaji Warioba.

“Rasimu ya Katiba ni sawa na jengo, ukibomoa msingi wa jengo huwezi tena kuzungumzia suala la mabati na rangi, Rasimu ya Jaji Warioba msingi wake ni serikali tatu, ukiondoa serikali tatu katika rasimu ina maana umebomoa msingi na hivyo utakuwa umeharibu jengo,” alisema.

Dk. Slaa alisema CCM lazima watambue kuwa rasimu ya katiba mpya iliyowasilishwa na Jaji Warioba katika mkutano wa Bunge Maalum la Katiba ilikuwa na mapendekezo ya wananchi, hivyo uchakachuaji wa aina yeyote ile itakuwa ni sawa na kuwasaliti Watanzania ambao wanataka muundo wa serikali tatu.

Aliongeza kuwa Katiba ya mwaka 1977 ilitengenezwa wakati wa mfumo wa chama kimoja cha siasa na wananchi hawakushirikishwa, hivyo CCM isitake taifa lirudi katika mgogoro wa Katiba ya 1977 kwa kuleta katiba isiyokuwa shirikishi kwa wananchi.

Alisema katiba ni mkataba kati ya wananchi na serikali, lakini inashangaza kuona serikali ya CCM ndiyo iliyokubali kuanza kwa mchakato huo, leo viongozi wake wameanza kuleta unafiki na kukwamisha upatikanaji wa katiba kwa kutaka kuondoa maoni ya wananchi.

Katika mkutano wa mjini Songea, Ukawa wamesema kuwa wanashangazwa na vitendo vinavyofanywa na viongozi wa CCM wakiwamo wabunge na mawaziri vya kumdhalilisha Jaji Warioba.

Wamesema Jaji Warioba anadhalilishwa wakati Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyemteua pamoja na wajumbe wenzake ili wafanye kazi ya kukusanya maoni kwa wananchi ili yatumike kuunda katiba mpya.

Kauli hiyo ilitolewa juzi jioni na Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la Chama cha Wananchi (CUF), Joram Bashangea kuwa hata kama Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba ambao wengi wao ni wafuasi wa CCM wataendelea na vikao vyao vya Bunge hilo serikali tatu ni lazima hata kama watachakachua maoni ya wananchi.

BASHANGE:KATIBA MPYA HAIZUILIKI
Katika mkutano huo uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Matarawe na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa Manispaa ya Songea, Bashange ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba ambaye alikatisha ziara kutokana na kupata dharura na kulazimika kurejea Dar es Salaam, alisema kazi aliyoifanya Jaji Warioba na Tume yake ni nzuri kwa kuwa alichowasilisha bungeni ni maoni yaliyotolewa na wananchi na kuwekwa katika Rasimu ya Katiba na wajumbe wote wa tume.

Alisema ndani ya tume hiyo kulikuwa na makada wa CCM na watumishi mbalimbali wa serikali ambao waliungana na kufanya kazi ambayo ilileta mwelekeo mzuri wa kuipata katiba mpya.

Hata hivyo, Bashange alisema hivi sasa kuna dalili zinazoonyesha kwamba katiba mpya haiwezi kupatikana kutokana na kuwapo mizengwe mingi kwenye Bunge Maalum la Katiba ambayo imesababisha wajumbe wa Ukawa na wengine kadhaa kususia wakidai kuwa mawazo ya wananchi yamepuuzwa kutokana na mapendekezo yaTume ya Warioba kuhusu muundo wa Muungano wa serikali tatu kukataliwa na wajumbe ambao wengi wao wanatoka CCM.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Alatanga Nyagawa, alisema katiba ni lazima ipatikane hata kama kutakuwapo njama za kuikwamisha.

MCHUNGAJI: WARIOBA ASISHAMBULIWE
Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa la Assemblies of Gog (AGT) Wilaya ya Tarime, Joseph Rioba, alisema ni kosa kwa CCM kumshambulia Jaji Warioba wakati mapendekeo aliyoyaweka kwenye rasimu ya katiba ni maoni ya wananchi.

“Watanzania walipendekeza muundo wa serikali tatu sasa kuna sababu gani kwa CCM kuanza kumulaum Jaji Warioba, CCM lazima watambue kuwa walioleta serikali tatu siyo Ukawa ni Watanzania,” alisema.

Mchungaji Rioba alisema CCM lazima watambue kuwa katiba ni mali ya wananchi, hivyo hata kama itatokea Ukawa wakaingia madarakani wataifuata katiba hiyo ambayo ni ya wananchi.

WANDWI: UKAWA SIYO WALAFI
Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, Mustapha Wandwi, alisema vyama vilivyoungana na kuunda Ukawa ni vile ambavyo havina ulafi na vimefanya hivyo ili kutetea wananchi iweze kupatikana Katiba yenye maoni ya wananchi na siyo maoni ya chama kama inavyotaka kufanya CCM

JESHI LA POLISI
Dk. Slaa akizungumzia kuzuiwa maandamano ya Ukawa, alisema Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Ernest Mangu, anapaswa kuwapeleka darasani wakuu wa Polisi wa Wilaya (OCD’s) kutokana na walio wengi kutozifahamu sheria vizuri.

“IGP Mangu wawezeshe ma-OCD wako waende shule wakasomee sheria hawa ndio chanzo cha kutokea vurugu nchini, hawafahamu sheria zinaeleza vipi chama kinapotaka kufanya maandamano,” alisema.

Hatua ya Dk. Slaa kutaka ma-OCD kwenda shule ilifuatia barua ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Tarime, Issa Bukuku, ambayo aliwaandikia viongozi wa Ukawa wa wilaya hiyo wakati akijibu barua waliyoomba kufanya maandamano wakati wa kupokea viongozi wa Ukawa kutoka makao makuu.

Katiba barua hiyo ya OCD alieleza kuwa wakati wa mkutano wa viongozi wa Ukawa, viongozi wa umoja huo hawaruhusiwi kutoa lugha za matusi na kashfa kwa viongozi wa serikali na pia hawatakiwi kutoa lugha za uchochezi.

Dk. Slaa alisema majibu ya OCD huyo yanaonyesha ni jinsi gani asivyofahamu sheria kwa sababu haiwezekani kiongozi wa siasa akasimama jukwaani bila kuwasema viongozi wa serikali.

“Huyu OCD aende shule, haiwezekani Sheikh au Padre akasalisha msikitini au kanisani bila kumkema shetani, sisi vyama vya upinzani shetani wetu ni Serikali ambayo imesababisha maisha magumu kwa wananchi,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

No comments: