Domayo alisaini Azam akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na wana Jangwani hao kubakiza mwezi mmoja tu hivyo kikanuni alikuwa huru kuzungumza na hata kukubaliana na timu nyingine. Kanuni zinatoa uhuru huo kwa mchezaji ambaye amebakiza chini ya miezi sita katika mkataba.
KWA mashabiki wa Yanga haikuwa taarifa nzuri. Iliwashitua mno pale waliposikia kuwa kiungo wao mashuhuri, Frank Domayo, amejiunga na mabingwa wapya wa Ligi Kuu Bara, Azam FC kwa mkataba wa miaka miwili.
Domayo alisaini Azam akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na wana Jangwani hao kubakiza mwezi mmoja tu hivyo kikanuni alikuwa huru kuzungumza na hata kukubaliana na timu nyingine. Kanuni zinatoa uhuru huo kwa mchezaji ambaye amebakiza chini ya miezi sita katika mkataba.
Kiungo huyo anayeichezea pia timu ya taifa, Taifa Stars, ameng’olewa Yanga kwa kitita cha Sh70 milioni huku na pia atakuwa akilipwa mshahara wa Sh3 milioni kwa mwezi achilia mbali posho na juisi za Bakhresa pale Chamazi.
Kwa maisha ya sasa ya Kitanzania, Sh70 milioni alizolipwa ni fedha nyingi na ni wananchi wachache wa nchi hii wanaofanikiwa hata kuzitia tu machoni fedha hizo kabla ya kurudisha roho zao kwa Muumba achilia mbali kuzimiliki.
Hivi ni baadhi tu ya vitu ambavyo unaweza kuvifanya kwa fedha za usajili wa Domayo.
1.Kununua kiwanja
Kiasi cha Sh10 milioni kutoka kwenye kitita hicho kinaweza kukupatia kiwanja cha maana cha ukubwa kati ya mita 25 kwa 25 au hata cha mita 35 kwa 35 katika maeneo tulivu ya Jiji la Dar es Salaam kama vile Tabata, Tegeta, Kimara, Goba au Mbagala.
2.Shamba la ekari 2 Mlandizi, Pwani
Ardhi ni amana kubwa kwenye ulimwengu wa sasa, ni amana ya kudumu. Hivyo ni vyema kwa mtu yeyote kuwekeza kwenye sekta hii kwa ajili ya matumizi yake na ya uzao wake wa baadaye.
Katika fedha za Domayo kwenda Azam, unaweza kutenga kiasi cha Sh 5 milioni pekee kununua kati ya ekari moja hadi mbili za shamba katika maeneo ya Mlandizi au Kigamboni.
3.Toyota Hiace
Wafanyabiashara watakwambia kuwa fedha iliyokaa si sawa na fedha iliyoko kwenye mzunguko. Kwenye fedha za usajili wa Domayo unaweza pia kuchukua milioni 16 na kununua gari aina ya Toyota Hiace kwa ajili ya biashara. Gari hizi zina uwezo wa kuingiza kati ya Sh40,000 hadi 60,000 kwa siku hivyo kuwa kati ya uwekezaji wa maana zaidi kwenye ulimwengu wa sasa unaohitaji zaidi usafiri.4.Toyota Verossa
Bado utakuwa na fedha nyingi tu iliyosalia. Unaweza kununua gari dogo la kutembelea aina ya Toyota Verossa iliyotembea kilomita elfu 40,000 tu kwa gharama ya Sh10 milioni.
Au unaweza kununua magari mengine madogo ya kutembelea kama vile Toyota Mark II, Toyota Raum, Suzuki Swift au Toyota Opa kwa gharama isiyozidi Sh10 milioni.
5.Suzuki Carry ‘Kirikuu’ mbili
Katika fedha hiyo bado unaweza kutenga kiasi cha Sh15 milioni kwa kununua gari hizo ndogo za mizigo. Gari hizi hutumika kuhamisha mizigo ndani ya jiji na maeneo mengine nchini zikiwa na uwezo wa kubeba hadi tani moja.
Kwa Dar es Salaam gari hizo zina uwezo wa kuingiza hadi Sh20,000 kwa siku kila moja.
6. Bodaboda tano
Usafiri wa Pikipiki maarufu kwa jina la ‘Bodaboda’ ndio umeshika kasi nchini kwa sasa, mijini na vijijini. Baada ya kufanya hayo mengine, pia unaweza kuwekeza kwenye sekta hiyo kwa kununua pikipiki tano aina ya Boxer ambazo kila moja inauzwa Sh2 milioni. Utatumia Sh10 milioni.
7. Laptop (Tarakilishi mpakato)
Dunia imehama kutoka Analogia kwenda Digitali hivyo si vibaya ukatenga kiasi kidogo pia kwenye mkwanja huo wa Domayo na kununua Laptop mpya itakayogharimu kiasi cha Sh2 milioni. Hapo utakuwa na fursa kuperuzi mitandao kibao ya kijamii pamoja na kujua habari za dunia kupitia Intaneti.
Utapata Laptop ya kisasa zaidi yenye RAM (Random Access Memory) 4GB, Processor Speed 4GB, Hard Disk 1 Terrabytes (GB 1000) na Touch Screen.
8.Simu Samsung Galaxy S5Bado tuko digitali na fedha bado zinaturuhusu kufanya matumizi, kwenye lile burungutu bado unaweza kuchomoa hapo kama Sh1.2 milioni ukanunua simu yako nzuri ya Samsung Galaxy S5 ukaendelea kufurahia maisha kwa kuiweka dunia kiganjani kwako.
9. Fedha ya mfukoni
Bado utakuwa umebakiwa na Sh800,000 kama fedha ya mfukoni tu itakayokufanya uwe bonge la pedeshee mjini.

No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake