Wanafunzi wa vyuo vikuu nchini
Kenya wamezua vurugu wakipinga mpango wa serikali kutaka kuongeza karo
katika vyuo vikuu vyote vya umma.
Polisi walipambana na wanafunzi hao kwa kutumia gesi ya kutoa machozi kutawanya wanafunzi hao ambao walizua vurugu mjini na kuwapora abiria huku wakiharibu magari ya umma na yale ya abiria katika barabara kuu ya Uhuru katikakati ya jiji la Nairobi.
Wachuuzi walilazimika kuondoka mjini huku polisi wakipambana na wanafunzi hao ambao waliungana kutoka vyuo vikuu mbali mbali kote nchini Kenya.
Awali maandamano yao yalikuwa salama ingawa baadaye wanafunzi hao walioanza kuandamana tangu saa nne asubuhi walianza kuzua rabsha na kulazimisha polisi kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya.
Wanafunzi hao wanaandamana kupinga mapendekezo ya serikali kuongeza karo ya vyo vikuu , ingawa waziri wa elimu ya juu Profesa Jacob Kaimenyi amesema kuwa serikali bado haijatoa tamko rasmi ikiwa wanafunzi wa vyuo vikuu watalazimika kuongeza karo.
Alisema kuwa ripoti kuwa karo itaongezwa sio sawa na ni za kupotosha akisisitiza kuwa ikiwa jambo kama hilo litafanyika litahitajika kutangazwa na baraza la vyuo vikuu nchini humo baada ya makubaliano kufikiwa.
Wanafunzi hao wanapinga mpango wa serikali wakisema kuwa kuambatana na mfumuko wa bei, karo yao haipaswi kuongezwa na kwamba serikali inapaswa kushauriana nao kabla ya kufikia hatua zozote za kuongeza karo.
Wanafunzi watano wameripotiwa kujeruhiwa katika vurugu hizo.
BBC
No comments:
Post a Comment