MKUU wa mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga, ameipa siku Saba Hospitali ya
Serikali ya mkoa huo kushusha gharama ya matibabu kutokana na wananchi
kushindwa kumudu gharama hizo, zilizopandishwa baada ya Hospitali hiyo
kupandishwa hadhi na kuwa ya Hospitali ya rufaa
Aidha, kupandishwa hadhi kwa hospitali hiyo ni agizo la Rais, Jakaya
Kikwete, alilolitoa hivi karibuni kwa kuzitaka hospitali zote za mikoa
nchini kupandishwa hadhi na kuwa za rufaa.
Rufunga, alisema
Juni 6, 2014 kuwa kutokana na kupandishwa kwa gharama katika hospitali
hiyo, imebainika kuwa asilimia kubwa ya wakazi wa mkoa huo wameshindwa
kuzimudu na wengi wao kulazimika kurudi katika tiba za asili, hali
ambayo imeleta hofu kwa kuweza kuongezeka vifo ikiwemo vya mama na mtoto
mkoani humo.
Hata hivyo, Bwana Rufunga ametaja baadhi ya huduma ambazo gharama zake
zimeongezeka kuwa ni pamoja na kumuona daktari ambayo awali ilikuwa ni
bure na sasa itakuwa shilingi elfu tano, huduma za kujifungua zimepanda
na kuwa elfu Sabini kwa watoto wa kike na shilingi elfu themanini kwa
mtoto wa kiume.
Wizi wa dawa wakithiri
Amesema wimbi la upungufu wa dawa katika Zahanati na Vituo vya Afya
katika mkoa huo, linatokana na wizi unaofanywa na baadhi ya watumishi wa
sekta hiyo wasio waaminifu na kukwamisha zoezi la serikali kutimiza
malengo yake.
Amesema katika mikakati ya kupunguza vifo vya Mama na Mtoto
vinavyotokana na uzazi katika mkoa mkoa huo, wanashirikiana na wananchi
kuibua wimbi la wizi wa dawa katika vituo hivyo unaofanywa na baadhi ya
watumishi wasio waaminifu na kusababisha kukosekana kwa dawa na watu
kupoteza maisha.
“Hatuna tatizo la uhaba wa dawa, kinachotusumbua ni huu wizi wa madawa,
tumebaini wizi huu na hatutakubali kwani hata ukifanya utafiti unakuta
dawa za serikali zinauzwa mtaani kwenye maduka ya dawa ya watu binafsi
na sasa TAKUKURU wanatakiwa kutusaidia”alisema Rufunga.
Awataka watumishi wa afya kuwajibika
Aidha, amewataka watendaji na watumishi wa sekta ya afya kuwajibika
ipasavyo katika kukabiliana na vifo vya mama na mtoto vinavyotokana na
uzazi, kwa kuboresha miundombinu katika vituo vya afya pamoja na
kuhamasisha akina mama wajawazito kujifungulia katika vituo vya afya
pamoja na kuwaelimisha wananchi wajiunge na mfuko wa afya ya jamii.
Vifo vyaongezeka
Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dkt. Ntuli Kapologwe, amesema miongoni mwa
mikoa inayokabiliwa na changamoto ya vifo vya mama na mtoto ni pamoja na
mkoa huo, hivyo kuitaka jamii wakiwemo akina Baba kuwa mstari wa mbele
katika kupiga vita vifo hivyo kwa kuwahamasisha akina mama kuhudhuria
kliniki mara kwa mara na kujifungulia kwenye vituo vya afya.
“Tunajitahidi kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. Jakaya Kikwete, kwa kuanzisha kampeni ya kupiga vita vifo vya mama
na mtoto vinavyokana na uzazi pia na sisi tunasikitishwa na vitendo vya
baadhi ya watumishi katika sekta hii wanaotukana wagonjwa na kuficha
dawa muhimu” Dkt. Kapologwe alisema.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa wakati Serikali ikijipanga kuhakikisha
upatikanaji wa dawa unakuwa wa uhakika katika hosipitali zote za umma
hapa nchini, wapo baadhi ya watumishi wasio waaminifu ambao wamekuwa
wakijinufaisha kwa manufaa yao binafsi kwa kuuza dawa hizo katika maduka
ya sawa baridi.
Mapema mwaka 2013, Bohari Kuu ya Madawa (MSD) ilitangaza kuanza
mchakato wa kuweka nembo maalum katika dawa zote zinazomilikiwa na
serikali kwa lengo la kukomesha hujuma dhidi ya dawa hizo, licha ya
tatizo la wananchi wengi kutoitambua nembo ambayo inatumiwa hivi sasa na
(MSD) pamoja na dawa zinazomilikiwa na serikali.
Chanzo: Fikrapevu
No comments:
Post a Comment