SERIKALI imeeleza kuwa tatizo la jokofu la kuhifadhia maiti
lililokuwa limeharibika katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda
mkoani Mara limetafutiwa ufumbuzi.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni mjini hapa jana na Naibu Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Elimu), Kassim Majaliwa, alipojibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu,
Esther Bulaya (CCM).
“Jokufu la kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Bunda
limeharibika kwa muda mrefu na hivyo kusababisha wananchi kuhifadhi
maiti Mwanza na Musoma kwa gharama kubwa, sasa nataka kujua ni lini
serikali itatatua adha hiyo kwa wakazi wa Bunda na Mwibara?” alihoji
Bulaya.
Majaliwa alikiri jokufu la kuhifadhia maiti liliwahi kuharibika na
kusababisha wananchi kuhifadhi maiti Mwanza na Musoma, lakini kwa sasa
limetengenezwa.
Alisema tatizo lilikuwa ni kuziba kwa bomba linalopitisha gesi
kutoka kwenye ‘compressor’ na kusababisha bomba hilo kupasuka na
kuruhusu gesi kutoka. Alisema kulikuwa na tatizo la umeme katika jengo
hilo la kuhifadhia maiti.
“Tatizo hilo lilisababisha jokofu hilo kushindwa kufua baridi na kwamba Aprili 20, mwaka huu lilitengenezwa,” alisema.
Alisema kuanzia Mei 5, mwaka huu hadi sasa, sehemu zote sita za kuhifadhia maiti katika hospitali hiyo zinafanya kazi.
No comments:
Post a Comment