Lakini unadhani kuna kiongozi yeyote wa TFF au Serikali ambaye amejitokeza kumpongeza? Hapana.
UKITAKA kumhukumu Mtanzania usimsikilize sana. Ukimpa nafasi ya kumsikiliza atakupa maneno matamu sana. Ni kama zilivyo hotuba za viongozi wetu. Unaweza kudhani zinatoka katika mioyo yao, kumbe zinatoka katika midomo yao tu.
Mara kadhaa viongozi wetu wa Serikali na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) wamekuwa wakiyasisitizia makampuni mbalimbali yajitokeze kudhamini mchezo wa soka nchini. Umewahi kusikia?
Majuzi nikiwa hapa Brazil nilikuwa nasoma taarifa kuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Binslum Tyres Limited, Nassor Binslum ameingia mkataba na timu ya tatu ya Ligi Kuu nchini, Ndanda FC.
Mkataba wa kwanza ulikuwa dhidi ya Mbeya City na thamani yake ulikuwa ni Sh360 milioni. Mkataba wa pili ulikuwa wa Stand FC ya Shinyanga. Thamani ya pesa haijatajwa ingawa najua ni kubwa. Mkataba wa tatu ni huu wa Ndanda ambao pia thamani ya pesa haijatajwa ingawa najua nao utakuwa ni mkubwa.
Lakini unadhani kuna kiongozi yeyote wa TFF au Serikali ambaye amejitokeza kumpongeza? Hapana. Ni rahisi tu kufikiri kwamba hotuba wanazotoa wakati wa kutaka kampuni zidhamini michezo zinakuwa zimeandaliwa kitaalamu na wapambe na wala maneno wanayoyasema hayatoki kwa viongozi wao.
Nimefuatilia kwa karibu taarifa kwa vyombo vya habari kutoka kwa msemaji wa TFF, Boniface Wambura, nikiamini kwamba huenda mheshimiwa Rais wa TFF na watendaji wake wa karibu watamtuma kutoa salamu za pongezi kwa Binslum au kwa timu ambazo amezidhamini, lakini naona kimya. Wambura bado hajatumwa kufanya hivyo kwa sababu Tanzania ina mvuto zaidi katika habari zinazohusu vurugu na si pongezi.
Habari za uchaguzi wa utata wa Simba hasa kuhusu Michael Wambura kwa Tanzania ni habari muhimu kuliko udhamini wa soka. Hasa ukizingatia timu ambazo zimedhaminiwa kwa pesa nyingi ni timu za mikoani ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikiteseka na udhamini katika soka.
Ikifika wakati wa uchaguzi wa viongozi, najua kuna viongozi watakaokwenda kugombea ubunge na utasikia wanasema “Chini ya uongozi wangu nikiwa pale, mikataba ya udhamini katika soka iliongezeka ikiwamo udhamini wa Binslum katika klabu tatu za Mbeya City, Ndanda na Stand” Watanzania bwana!
Credit:wanasposi

No comments:
Post a Comment