ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 10, 2014

Mahiza akubali yaishe, gari la wagonjwa larudi Kibiti


Mkuu wa Mkoa wa Pwani  Mwantumu Mahiza akizungumza na Wakazi wa Vijiji viwili vya Chamakweza na Pingo  mkoani Pwani kwa ajili ya kusuruhisha mgogoro kati ya wakulima na wafugaji. Picha na Sanjito Msafiri 
Kwa ufupi
Akizungumza kwa njia ya simu, mganga mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Utete, Michael Mollel alisema madai ya kuhamishwa kwa gari hilo na kisha kurudishwa yalikuwa mambo ya wanasiasa, akisema ndiye aliyeongoza jopo la wataalamu kwenda kuomba gari hilo kwa ajili ya Kituo cha Afya Kibiti.

Rufiji. Hatimaye gari la wagonjwa la Kituo cha Afya cha Kibiti mkoani Pwani lililokuwa limehamishiwa Zahanati ya Nyamisati kwa agizo la mkuu wa mkoa limerudishwa.
Diwani wa Kata ya Kibiti, Hamidu Ungando alithibitisha kurudishwa kwa gari hilo Alhamisi iliyopita na kulishukuru gazeti la Mwananchi kwa kuripoti malalamiko yake kwa mara ya kwanza yaliyosababisha wahisani na viongozi mbalimbali kubaini upungufu katika kulihamisha gari hilo la kubebea wagonjwa.
Awali, Mkuu wa Mkoa Mwantunu Mahiza na mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Rashid Salum walisisitiza kwamba gari hilo lazima lipelekwe Nyamisati kwa kuzingatia ukubwa wa tatizo la eneo hilo na kuongeza kuwa ilikuwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete.
Hata hivyo, meneja mradi wa Access uliotoa gari hilo Mei mwaka huu, Dk Ahmed Hingora alipinga maelezo ya viongozi hao na kusema Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI) ambayo mradi wake ndio uliotoa gari hilo kwa Kituo cha Afya Kibiti na zahanati nyingine, alieleza kushangazwa na kitendo cha kuhamishwa kwa gari hilo.
Alipoulizwa kuhusu kurejeshwa kwa gari hilo Kibiti, Mahiza alijibu: “Nimewaachia wananchi wa Rufiji waamue wenyewe… naogopa kuchafuliwa kwenye mitandao, watu wenyewe wa Rufiji wataamua hatima ya gari hilo.”
Awali, Mahiza alimshtaki Ungando kwa Kamati ya Siasa ya CCM mkoani Pwani baada ya diwani huyo kudai kuwa gari la wagonjwa lililokabidhiwa Kituo cha Afya cha Kibiti limepelekwa Nyamisati.
Jitihada za kumpata Salum zilikwama.
Akizungumza kwa njia ya simu, mganga mkuu wa Hospitali ya
Wilaya ya Utete, Michael Mollel alisema madai ya kuhamishwa kwa gari hilo na kisha kurudishwa yalikuwa mambo ya wanasiasa, akisema ndiye aliyeongoza jopo la wataalamu kwenda kuomba gari hilo kwa ajili ya Kituo cha Afya Kibiti.
“Baada ya kupokewa pale Kibiti, lilipelekwa kwa mkurugenzi mtendaji wa wilaya kwa ajili ya taratibu za usajili na sasa tunavyozungumza gari limerudishwa Kibiti na linaendelea kutumika kama lilivyotakiwa liwe,” alisema Dk Mollel.
Kurudishwa kwa gari hilo ni faraja kwa wananchi wa kata 12 ambazo hazina vituo vya afya na zinategemea Kituo cha Afya Kibiti ambacho kimepandishwa hadhi na kuanza kutoa huduma za upasuaji.

No comments: