Katika mkakati wake wa kuhakikisha inakusanya kodi ipasavyo, Serikali
imependekeza kutoza kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), katika maeneo
mbalimbali, ikiwamo uuzaji wa majeneza.
Katika miaka ya karibuni, biashara ya majeneza imekuwa kwa kasi kubwa, hasa Dar es Salaam.
Pendekezo hilo limo katika Muswada wa Sheria ya VAT unaotarajiwa
kuwasilishwa bungeni kuanzia Juni 27, mwaka huu, ambao pia umependekeza
kutoza kodi hiyo katika maeneo mengine ya usindikaji maziwa, makandarasi
wazawa na sekta ya utalii.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema jana kuwa: “Ngoja
tusikilize wadau wanasemaje, lakini lengo la Serikali ni kukuza uchumi
na kukusanya mapato.”
Alisema kuondoa misamaha ya kodi si njia pekee ya kuvutia uwekezaji na
kusisitiza kuwa nchi lazima ipate fedha ili kupeleka huduma kwa
wananchi.
Juzi, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ilikutana na Kamati ya
Bunge ya Bajeti, Wizara ya Fedha pamoja na maofisa wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) kujadili muswada huo na kutoa maoni yao, huku wabunge
wengi wakiupinga na kutaka uboreshwe.
Baadhi ya wadau wa sekta binafsi walimweleza Mwenyekiti wa Kamati ya
Bajeti, Andrew Chenge kuwa licha ya muswada huo kutakiwa kufanyiwa
marekebisho, hata wao hawakushirikishwa ipasavyo kwa maelezo kuwa
waliuona Novemba mwaka jana na kupewa wiki moja tu ya kuujadili na kutoa
maoni yao.
Kwa masharti ya kutotajwa majina, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bajeti
walisema ni jambo la ajabu kwa Serikali kuanza kukusanya kodi hadi
katika uuzaji wa majeneza.
“Wameona biashara hii inafanywa na idadi kubwa ya watu sasa wanataka
kuanza kutoza kodi ya VAT, huku si kuwatendea haki Watanzania, hata kama
ni kupata mapato lakini si kwa njia hii.”
“Muswada huu umekaa kisiasa zaidi, yaani kukusanya mapato tu, bila kutazama athari zake,” alisema mmoja wa wajumbe hao.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment