Zanzibar Image by Hassan Khamis |
Maeneo mbalimbali visiwani Zanzibar, yamepangwa kuwekwa kamera za CCTV, kukabili matukio ya uhalifu.
Waziri wa Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk
amesema mchakato wa utafiti wa kuweka kamera hizo, umekamilika na
kipaumbele ni eneo la Mji Mkongwe.
Mbarouk alisema hayo wakati akijibu hoja mbalimbali za wajumbe wa Baraza
la Wawakilishi, waliochangia makadirio mapato na matumizi ya bajeti ya
Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2014/2015 katika Baraza Wawakilishi.
Alisema kampuni mbili, zilipewa kazi hiyo ya kuweka kamera za CCTV
katika maeneo mbalimbali , ambapo kipaumbele ni Mji Mkongwe wa Zanzibar.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni hizo tayari zimewasilisha taarifa yake
serikalini kwa ajili ya uchambuzi wa kina na ripoti yake itatangazwa kwa
wananchi,” alisema.
Alisema uwekaji wa kamera za CCTV ni muhimu kwa ajili ya kukabili
matukio ya uhalifu vitendo vya uhalifu ambavyo huathiri maisha ya watu
na maendeleo ya sekta ya utalii.
Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu alitaka kufahamu mikakati
ya kuweka kamera za CCTV za kurekodi matukio mbalimbali , ikiwemo ya
uhalifu katika eneo la Mji Mkongwe.
Jussa alisema kama mradi huo wa kuweka kamera ungekamilika na kufanya
kazi, matukio mengi ikiwemo kumwagiwa tindikali kwa raia wawili
wanawake kutoka Uingereza, kungedhibitiwa na wahusika wangekamatwa.
Awali, Mbarouk alisisitiza suala la kuimarishwa kwa amani na utulivu
nchini na alitaka jamii kuachana na vitendo vya uhalifu ambavyo ni
tishio kwa maisha ya watu.
Alisema matukio mbalimbali ikiwemo ya hivi karibuni la kulipuliwa bomu
eneo la Darajani, kunatishia amani ya nchi pamoja na wageni kutembelea
Zanzibar.
“Sekta ya utalii inategemea sana amani na utulivu na ikivurugika tu,
basi hakuna mgeni atakayezuru Zanzibar katika mazingira ya vurugu na
fujo,” alisema.
Wakati huo huo, Mwakilishi wa Viti Maalumu, Asha Bakari Makame, alisema
kutokana na kuwepo matukio ya ugaidi, suala la watu kupekuliwa zaidi,
hususani wanawake waliovaa baibui ni jambo la kawaida.
Alisema yapo matukio ya wanawake, kutumia vibaya mavazi hayo, kutokana
na wengine kuficha sura zao kwa lengo la kufanya uhalifu huo.
“Mimi sipingi matumizi ya kivazi cha baibui...lakini kufuatia kuibuka
kwa matukio ya uhalifu na vitendo vya ugaidi, wanawake waliovaa
mabaibui wanalazimika kupekuliwa,” alisema.
Alisema mbinu za uhalifu zimeongezeka siku hizi hali ambayo pia wanaume
wanaweza kutumia vazi hilo kwa ajili ya kutekeleza uhalifu.
Vazi hilo ambalo ni maarufu kwa wakazi wa mwambao wa pwani ya Afrika ya
Afrika, hususani Zanzibar, lilizua mjadala jana kwenye Baraza la
Wawakilishi baada ya baadhi ya wajumbe wanawake, kulalamika kwamba
wanaofanya kazi kwenye vyombo vya habari vya Serikali ya Zanzibar,
wanalazimishwa kuvua mavazi hayo wanapoingia kazini.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo,
Bihindi Khamis Hamadi alisema uvaaji baibui kwa wanawake, wanapokuwa
kazini ni upendeleo na si utaratibu wa kazi.
Alisema utaratibu wa kazi na masharti yake, upo wazi kwamba vazi hilo haliruhusiwi kuvaliwa sehemu ya kazi.
“Mheshimiwa Naibu Spika yapo malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi wa
Serikali kwamba wanazuiliwa kuvaa mabaibui katika sehemu ya
kazi...ukweli unabakia kuwa, vazi la baibui kazini haliruhusiwi na
kinachofanyika ni mazoea tu kwa wanawake hao,” alisema.
Alikiri pamoja kwamba ni sehemu ya utamaduni wa wananchi wa Zanzibar,
wanawake wanapoingia kazini na mavazi hayo, hutakiwa kuyavua na
kuyahifadhi katika sehemu maalumu hadi wanapoondoka kazini.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, jana aliliambia Bunge mjini Dodoma kwamba
matukio ya uhalifu yanayotokea Zanzibar, ikiwemo kumwagia viongozi
tindikali na utumiaji wa mabomu ya kurusha kwa mkono, yalipangwa kuwa
mengi zaidi, lakini Serikali imeyadhibiti.
Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Betty Machangu (CCM).
Pinda alisema baada ya matukio hayo Zanzibar, Serikali ilijipanga
vizuri ikiwemo kutumia vyombo vya kimataifa, kujua chanzo cha matukio
hayo na katika harakati hizo, walibaini kulikuwa kutokee matukio mengi
zaidi, Serikali ikayazuia.
Katika swali lake kwenye kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo kwa
Waziri Mkuu, Machangu alitaka kauli ya Serikali kuhusu kuibuka kwa
vikundi vya kihalifu vya vijana na vingine vyenye tabia ya kigaidi.
Alitaja baadhi ya vikundi hivyo ni Panya Road, Kiboko Msheli, Komando
Yosso na Toto Tundu, na vingine vilivyotokea Mtwara ambavyo vilikuwa
vikipewa mafunzo vichakani na kwamba yako madai, baadhi walipelekwa
Somalia.
Machangu pia alitaka kufahamu kauli ya Serikali kuhusu matukio ya
Zanzibar kuhusu mauaji ya padre na kumwagiwa tindikali kwa mashekhe.
Katika ufafanuzi wake, Pinda alisema Machangu amechanganya mambo mawili
katika swali lake, moja la ugaidi na lingine la uhalifu wa kawaida.
Katika suala la uhalifu la vikundi hivyo kupora vitu na kukimbia,
Polisi imeshafanyia kazi. “Pale Dar es Salaam hali sasa ni shwari.
Naomba vijana wajiepushe na vitu vitakavyowakutanisha na mkono wa dola,”
alisema.
Pinda ametoa kauli hiyo, wakati mwishoni mwa wiki iliyopita mtu mmoja
alifariki dunia na wengine saba kujeruhiwa baada ya kurushiwa bomu na
watu wasiojulikana katika eneo la Darajani, muda mfupi baada ya
kuhudhuria mawaidha yaliyokuwa yakitolewa na Shekhe Kassim Mafuta Kassim
(38) mkazi wa Pongwe mkoani Tanga. Aliyefariki dunia kwa bomu hilo ni
Muhammed Khatib Mkombalaguha.
Tukio hilo la mlipuko ni la nne kutokea mwaka huu. Mengine ni
yaliyotokea Kanisa la Evangelist lililopo maeneo ya Fuoni Machi 2,
Kanisa la Anglikana, Mkunazini, Februari 24 na mlipuko mwingine ulitokea
kwenye hoteli ya kitalii ya Mercury ilioko Forodhani. Vilevile,
Zanzibar imeandamwa na matukio ya kumwagiwa watu tindikali pamoja na
kushambuliwa kwa risasi.
No comments:
Post a Comment