MAMLAKA ya Mawasiliano (TCRA), kupitia Mfumo wa Anuani Mpya za Kimataifa na Postikodi, inatarajia kutoa anuani kwa kaya zote ili kila Mtanzania awe na anuani yake.
Akizungumza na waandishi wa habari katika warsha ya Wahariri wa Habari kuhusu Siku ya Kimataifa ya Mawasiliano jana, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Mkomwa, alisema mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa anuani kwa kila mtu.
Mpaka sasa hivi kuna anuani za posta 173,000 tu katika nchi yenye watu zaidi ya milioni 43, kwa mfumo huu ambao uko tayari kisheria, tutafanikiwa kumpa kila Mtanzania anuani, alisema Profesa Mkomwa.
Alifafanua kuwa mfumo huo ambao hata kanuni za utekelezaji wake ziko tayari, kilichobakia ni kutoa namba ya nyumba na barabara kwa kila nyumba na kuziweka katika mfumo wa taarifa wa kompyuta na kumrahisishia kila Mtanzania kutambulika kwa anuani ya nyumba na barabara anayoishi.
Manufaa mengine ya mfumo huo baada ya kuboreshwa na kuwa katika mfumo wa intaneti, Profesa Mkomwa alisema msafiri anayekwenda sehemu yoyote ya mji, ataelekezwa na programu ya kompyuta iwe ya simu au ya gari njia rahisi na za kumuepusha foleni mpaka afike anakotarajia.
Katika warsha hiyo inayofanyika katika siku ya kwanza ya wiki ya Mawasiliano yenye kauli mbiu ya ‘Namna ya kushirikisha wanawake na wasichana katika teknolojia ya mawasiliano, mmoja wa watoa mada kutoka Kenya, Betty Nzioka, alielezea namna teknolojia ya mawasiliano na vyombo vyake vya kielektroniki, vinavyoathiri mazingira.
Nzioka alielezea umuhimu wa wazalishaji wa vifaa vya ICT, kuwekeza katika kulinda mazingira yanayochafuliwa na mabaki ya vifaa hivyo ikiwemo hewa chafu na taka ngumu yanayoathiri mazingira.
Katika hili alieleza namna Kenya ilivyojipanga kisheria kuwabana wazalishaji wa vifaa hivyo pamoja na wadau wake kupeleka teknolojia inayofaa na inayodumu nchini huko pamoja na kuwekeza katika viwanda vya kutumia mabaki ya vifaa vya teknolojia hiyo badala ya kuyaacha kuharibu mazingira.
No comments:
Post a Comment