ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 12, 2012

Mume amkata kwa panga mkewe ukweni

MAMA wa watoto wanne, Grace Senga (36) wa kitongoji cha Katusa mjini hapa amecharangwa kwa panga mwili mzima na mumewe kwa kilichoelezwa ni wivu wa mapenzi. 

Inadaiwa mumewe huyo, Florence Katembe (45), alimshambulia kwa panga na kusababisha majeraha na pia kutumia panga hilo kumkata vidole vinne vya mkono nyumbani kwa wakweze katika kijiji cha Mtimbwe mjini hapa huku watoto wao wakishuhudia. 

Mama huyo ambaye amepoteza fahamu kutokana na kupoteza damu nyingi alielezwa akiwa katika chumba maalumu cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) katika hospitali ya mkoa wa Rukwa mjini hapa. 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Isuto Mantage, jana alithibitisha tukio hilo na kusema mtuhumiwa anatafutwa na Polisi baada ya kutokomea kusikojulikana baada ya kumtendea mkewe unyama huo. 

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, muuguzi wa zamu katika hospitali hiyo, Deodatha Kayumba alisema mama huyo alifikishwa hospitalini hapo saa 10 alfajiri, akiwa na majeraha makubwa huku akiwpoteza fahamu kutokana na kuvuja damu nyingi. 


“Kwa kweli huwezi hata kumwona alivyojeruhiwa … amefanyiwa unyama wa kutisha, mkono mmoja ana majeraha zaidi ya 10, mkono mwingine vidole vinne vimekatwa, kichwani usiseme ana majeraha makubwa sana. 

“Yu mahututi … amepoteza fahamu kwani amevuja damu nyingi sana,“ alisema Kayumba. 
Kwa mujibu wa baadhi ya ndugu wa mama huyo ambao hawakuwa tayari kutajwa gazetini, wiki mbili zilizopita mumewe alimuaga mkewe kuwa anakwenda kijiji cha Singiwe, Mpanda mkoani Katavi kukata miti ya mbao. 

Inadaiwa kuwa aliporejea nyumbani alipewa taarifa na majirani kuwa mkewe aliamua kuhamia nyumbani kwa wazazi wake kijijini Mtimbwe na watoto wake wote baada ya kukosa fedha za kujikimu akihofia kufa kwa njaa kama angeendelea kuishi nyumbani kwake, kwani kwa wiki zote mbili, mumewe hakumtumia fedha za kujikimu kama alivyomwahidi. 

“Shemeji ghafla alifika nyumbani kwa wakeze na kukuta mkewe na watoto hali iliyomkasirisha na akadai kuwa mkewe alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtu mwingine kijijini hapo, lakini mkewe aliapa kutokuwa na mwanamume mwingine,“ alisema mmoja wa ndugu za Grace. 

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa alisubiri hadi usiku wa manane, akamvamia mkewe na kumcharanga kwa panga huku akionya watoto wake, kuwa angewaua kama wangepiga kelele, inadaiwa watoto hao walishuhudia baba yao akimfanyia akimshambulia mama yao. Kwa mujibu wa Mantage, mtuhumiwa ametoroka.


Habari Leo

1 comment:

Anonymous said...

Wewe baba ulaaniwe!!! Ufe kifo cha maumivu makali!! How dare are you? I hope justice will prevail. Kwa kweli wanawake wanaonewa sana especially vijijini.I hope there are some advocates out there who will make sure this man stay in jail for the rest of his life. And the poor kids will need some psychological help for what they witnessed.