ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, July 19, 2026

MARY MWAKIBETE WA ITV, ASHINDA TUZO YA MTANGAZAJI BORA WA KIKE 2026

Mwanahabari wa ITV na Capital Radio, Mary Mwakibete.



NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Mary Prisca Mahundi, amemkabidhi tuzo ya Best Female Presenter and Journalist 2026 kwa mwakilishi wa Mwanahabari wa ITV na Capital Radio, Mary Mwakibete.

Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa Sifuni Mshana, Mwandishi wa ITV, aliyemwakilisha Mwakibete katika hafla ya Ladies Talk Tanzania Initiative Awards 2026 iliyofanyika mkoani Morogoro.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mh. Mahundi amepongeza waandaaji wa Ladies Talk Tanzania Initiative kwa kuendelea kutoa heshima na kutambua mchango wa wanawake katika sekta ya habari nchini.

"Tunapowatambua wanawake hawa tunatia moyo vizazi vijavyo. Wanawake katika vyombo vya habari wanafanya kazi kubwa ya kuelimisha jamii na kuleta mabadiliko chanya," amesema Naibu Waziri Mahundi.

Kwa upande wake, Mshana aliyepokea tuzo hiyo kwa niaba ya Mwakibete, ameshukuru uongozi wa Ladies Talk Tanzania Initiative na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uadilifu katika tasnia ya utangazaji.

Tuzo za Ladies Talk Tanzania Initiative zinalenga kutambua wanawake wabunifu na wanaofanya kazi kwa kujituma katika nyanja mbalimbali ikiwemo habari, ujasiriamali, afya na maendeleo ya jamii.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wadau wa maendeleo na wanahabari kutoka mikoa mbalimbali nchini.



No comments: