Kocha Mkuu wa Frankana, Mbrazili, Marcio Maximo.
Na Wilbert Molandi
JUMLA ya shilingi milioni 371 zinatakiwa kutumiwa na Yanga kwa ajili ya kukamilisha kumleta Kocha Mkuu wa Frankana, Mbrazili, Marcio Maximo.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji ndiye anabeba jukumu hilo la kumwaga mamilioni hayo ya fedha ili kumpata Maximo, kocha wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars.
Mbrazili huyo aliwahi kuifundisha timu ya taifa, Taifa Stars kabla ya nafasi hiyo kutua kwa Mholanzi, Jan Poulsen aliyeondolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa Yanga, kamati ya utendaji ya timu hiyo ilikutana hivi karibuni na kujadiliana masuala mbalimbali ikiwemo la usajili na suala la kocha.
Chanzo hicho kilisema, katika kikao hicho, viongozi hao wamempendekeza Maximo kuja kukinoa kikosi hicho kwenye msimu ujao wa 2014-2015.
Kilisema kuwa, kocha huyo amekubali kuja kuifundisha Yanga kwa mshahara wa dola 16,000 (sawa na shilingi milioni 25) kwa mwezi, hivyo kwa mwaka mmoja timu hiyo itamlipa Mbrazili huyo shilingi milioni 307).
Kiliongeza kuwa, pia kocha huyo anataka fedha ya uhamisho dola 40,000 (sawa na shilingi milioni 64), hivyo jumla ya fedha watakazotumia Yanga ni shilingi 371.
“Fedha hizo ndizo tumefikia hapo, lakini bado kuna majadiliano kuhusiana na kupunguza kiwango cha mshahara na fedha za kusaini. Halafu litakuwa ni suala la Maximo atakuja lini nchini,” kilieleza chanzo.
Gazeti la Championi Jumamosi ndiyo lilikuwa la kwanza kuandika kuhusiana na ujio wa Maximo nchini wiki moja iliyopita, kabla ya juzi, magazeti mengi nayo ‘kujitupia’ na kuripoti suala hilo.
Pamoja na juhudi hizo za Manji kumleta Maximo, kumeibuka mkanganyiko kuhusiana na kipa wa Yanga, Juma Kaseja ambaye alikuwa hana uelewano mzuri ma Maximo.
Wakati akiwa Stars, Maximo aliapa kutomuita Kaseja katika kikosi chake licha ya kwamba alikuwa ndiye kipa bora nchini na namba moja katika kikosi cha Simba.
Maximo alidiriki kumuita Ally Mustapha ‘Barthez’ ambaye hakuwa amedaka hata mechi moja Simba, hali iliyozua mkanganyiko na kamwe hakuwahi kusema tatizo lake na Kaseja ni lipi.
“Kweli kuna mpango wa kuanza ufumbuzi kuhusiana na suala la Kaseja. Wote wanahitajika Yanga, hivyo kutakuwa na mjadala kuhusu hilo na lengo ni kuona wanafanya kazi pamoja,” kilieleza chanzo.
“Tutamtaarifu Maximo na kumueleza hali halisi, tunaamini hakutakuwa na tatizo.”
Manji aliwaeleza jana wanachama wa Yanga kwamba kamati ya utendaji imefikia uamuzi wa kumleta kocha huyo ingawa Championi lina uhakika kuwa mazungumzo ya Manji na Maximo yamefikia asilimia 90.
“Juzi usiku tulikutana kamati ya utendaji kufikia muafaka wa kumleta Maximo, hivyo kila kitu kinakwenda sawa, vipo baadhi ya vitu tunavikamilisha,” alisema Manji wakati akizungumza na wanachama.
CREDIT:GPL
No comments:
Post a Comment