Dodoma. Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB), Freeman Mbowe amemtunishia misuli, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisema hawatishwi na kusudio alilotoa la kubadili kanuni ili kudhibiti tabia ya kambi hiyo kususia vikao vya Bunge kila wanapopinga hoja.
Mbowe alisema jana mjini hapa kwamba, wako tayari kwenda jela na hata ikibidi kufa kwa kupambana na ufisadi ndani ya Serikali.
Pinda alitoa pendekezo hilo baada ya wabunge wa upinzani ambao pia ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kususia Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini na kutoka bungeni.
Baada ya kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo, Pinda alipendekeza kubadilishwa kwa kanuni ili kuwadhibiti wabunge wa upinzani kutoka nje ya Bunge mara kwa mara.
“Inawezekana kanuni zinaruhusu... lakini haiwezekani kila mnaposhindwa hoja muone njia rahisi ni kutoka nje, nasema hivi, Watanzania hawawezi kukubaliana na hili,” alisema Pinda Ijumaa iliyopita na kuongeza:
“Tabia hii inayoendelea kujengeka siyo nzuri. Tuombe kanuni za Bunge zirekebishwe kwa sababu Bunge linaonekana halina watu wakati hao waliotoka hawana sababu za msingi.”
Akizungumzia pendekezo hilo, Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema alisema wabunge wa kambi hiyo wako tayari kupokea adhabu yoyote itakayotokana na kubadilishwa kwa kanuni za kudumu za Bunge hilo.
“Katika kutafuta haki, ustawi na heri ya taifa letu na ya vizazi vijavyo vya nchi yetu, tuko tayari siyo tu kukabili adhabu zitakazotokana na kubadilishwa kwa kanuni, bali hata kwenda jela na kufa.
“Ni heri kufa umesimama kwenye haki kuliko kuishi ukiwa umesimama kwenye ubatili.
Tunafahamu gharama na mateso tunayopitia kwa ajili ya kupinga ufisadi na ubadhirifu. Tumeamua kupambana mpaka mwisho hatimaye haki na ukweli vitatuweka huru.”
Baada ya kususia Bunge Ijumaa iliyopita, Mbowe alikutana na waandishi wa habari na kudai kuwa kulikuwa mkakati mahususi wa kuwazomea na kuwatukana.
“Tulitambua kwamba kuna mkakati mkubwa ulioandaliwa baina ya Serikali, uongozi wa Bunge na wabunge wa CCM kujaribu kufukia ufisadi mkubwa ambao unaikumba ya Wizara ya Nishati na Madini,” alisema Mbowe.
Alisema wabunge wa upinzani walipojaribu kuanika uozo huo, kiti cha Spika kilitumia nguvu za ziada kuwataka watoe ushahidi papo hapo.
Alisema badala ya kujadili hoja za msingi kama kashfa ya Akaunti ya Escrow inayofikia Sh200 bilioni, wabunge wa CCM waliamua kuungana na Serikali ili kufifisha hoja za wabunge wa upinzani.
Mbowe alisema yapo maazimio mbalimbali ya Bunge ambayo hayajatekelezwa kikamilifu na kutaja sakata la Katibu Mkuu wa zamani wa Nishati na Madini, David Jairo na kashfa ya Richmond mambo ambayo alisema hadi leo, Bunge limeshindwa kudai utekelezwaji wake.
1 comment:
Watanzania wote na mlioko ughaibuni huo ndio ukweli kwamba Serikali na bunge la CCM linajaribu kuua sana hoja nzito na za ukweli. Spika naye anakuwa namba moja kuua hoja ambazo zinatakiwa kuzungumzwa na kuondoa au kuwafichua uozo. Isitoshe wahusika wanatakiw kuwa wanajuizulu badala ya kuwabadili nafasi. Waziri mkuu usiendeleze ufisadi viongozi hawawajibiki ngo..
Post a Comment