ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 11, 2014

MBUNGE MKOANI DODOMA ATANGAZA KUNG'ATUKA MADARAKANI 2015


MBUNGE wa Chilonwa, Hezekiah Chibulunje (CCM), ametangaza kutogombea tena ubunge wa jimbo hilo mwakani baada ya kulitumikia kwa miaka 20 mfululizo.
Chibulunje alisema jana kuwa anastaafu ubunge ili kupisha vijana nao waongoze jimbo hilo alilosema limepiga hatua kubwa kimaendeleo.
Alisema amekuwa mbunge kwa vipindi vinne mfululizo na kwamba katika miaka hiyo 20, miaka kumi alikuwa Naibu Waziri ikiwemo katika Wizara ya Ushirika na Masoko mwaka 2000 hadi 2005.
Alibainisha kuwa, kuanzia mwaka 2006 hadi 2010, alikuwa Naibu Waziri katika wizara kadhaa alizozitaja kuwa ni Kilimo, Chakula na Ushirika; Viwanda na Biashara; Kazi; na Miundombinu.
“Katika nafasi zote hizi, za ubunge na unaibu waziri, sijawahi kupata misukosuko,” alisema Chibulunje na kutaja mafanikio katika jimbo hilo kuwa kupitika kwa barabara zote zikiwemo za tarafa ya Itiso, tofauti na alipoingia madarakani mwaka 1995
Pia, alisema kwa sasa asilimia 86 ya wakazi wa jimbo lake wanapata majisafi na kwamba, vijiji vitatu tu ambavyo vina shida ya maji, ambavyo ni Mlimwa kata ya Membe, Azimio kata ya Manyemba na Majengo kata ya Chiwondo.
Kwa upande wa umeme, alisema asilimia 90 ya vijiji vya jimbo hilo, vitakuwa na umeme ifikapo mwakani. Umeme huo unasambazwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA).
Kuhusu elimu ya sekondari, Chibulunje alisema alisema alipoingia madarakani mwaka 1995, jimbo hilo lilikuwa na sekondari moja ya Chamwino, lakini sasa kata zote 13 zina sekondari.
CHANZO:HABARILEO

No comments: