ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 28, 2014

MVUTANO: Werema, Maswi, Kafulila ngoma nzito

Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu (kushoto) akijaribu kuwasuluhisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema (kulia) na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila katika Viwanja vya Bunge Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dodoma. Vita kati ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila imeingia katika sura mpya baada ya mbunge huyo, kuwaeleza wapigakura wake kuwa endapo litatokea jambo lolote baya kwake, mhusika namba moja ni mwanasheria huyo.
Wakati Kafulila akisema hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi amemtaka mbunge huyo  kuonyesha uanaume wake kwa kuzungumza tuhuma zake akiwa nje ya Bunge.
Maswi aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam kwenye semina ya wizara hiyo na waandishi wa habari huku akisisitiza kwamba yeye ni msafi na yupo tayari kuchunguzwa na yeyote. “Nina usongo naye,” aliongeza Maswi.
“Mimi sichukui rushwa, sasa mtu anaokota vikaratasi vya kufungia vitumbua, anakwenda kutoa tuhuma zake…Alipomaliza kutoa tuhuma zake ndani ya Bunge nilimpigia simu nikamwambia kama yeye ni mwanaume, azungumze akiwa nje ya Bunge na siyo kutegemea kinga ya Bunge.
“Na akisema nje ya Bunge nampeleka mahakamani akathibitishe madai yake…Kwanza yuko mkononi, mwenzake (jina linahifadhiwa) hachangii tena hoja kwenye Wizara ya Nishati, nina tuhuma zake za kuhongwa,” alisema Maswi.
Maswi alikuwa akizungumzia tuhuma zilizoibuliwa bungeni na Kafulila akiwahusisha mawaziri wawili na Sh200 bilioni zilizochotwa kwenye akaunti ya Escrow, iliyokuwa inamilikiwa kwa pamoja kati ya Tanesco na Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL.
Akiomba mwongozo wa Spika bungeni jana, alisema wakati akichangia katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, Spika Anne Makinda alielekeza kuwa apeleleke ushahidi wa ufisadi huo mezani kwake ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Alisema waliwasilisha ushahidi huo yeye na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika,  mezani kwa Spika lakini hadi leo hawajui aliupeleka wapi zaidi ya kuambiwa kwamba Waziri (hakumtaja) anautumia kukosoa.
“Mwenendo wa jambo hili tangu ulipoanza na wakati wa hotuba ya Waziri Mkuu na baadaye Wizara ya Nishati na Madini linaleta shaka kuhusu dhamira ya kiti kulishughulikia na limekuwa likihatarisha maisha yangu na wengine,” alisema.
 Alisema juzi akiwa bungeni Werema alionyesha kusudio la kutaka kumpiga na baadaye nje ya Bunge alitangaza kukitoa kichwa chake.
 “Nasimama hapa kuwaeleza wananchi wa jimbo langu, kitakapotokea kitu chochote kwangu muhusika wa kwanza atakuwa yeye kwasababu ya kauli hiyo ya kusema kuwa atachukua kichwa changu,” alisema.
Kafulila alitaka kufahamu Spika Makinda analitolea uamuzi gani ili kusudi liweze kufikia mwisho.
Akijibu Spika Makinda, alisema alimwandikia barua lakini kabla ya kuiona, akalisikia jambo hilo katika vyombo vya habari, “Hizo ni adabu hizo? Siyo adabu.”
Alisema suala hilo limeshatolewa uamuzi kamili kwasababu limeshapelekwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Ma-document (nyaraka  zako zote zinakwenda huko, ulitegemea sisi tufanye hukumu hapa? Ndivyo tunavyofanya? Hata ulipoleta (suala hilo) juzi mimi nilikushangaa sana,” alisema.
Alisema Kafulia wapo naye katika Umoja wa Mabunge Duniani (IPU)  na kumsifia kuwa ni mmoja wa vijana hodari lakini kwa jambo hilo ameona (Spika) hajalishughulikia vyema.
“Sasa tunaanza kupata mashaka ni suala la kawaida ama siyo la kawaida? Nataka kukwambia kuwa suala hili liko kwa CAG na Takukuru sasa hivi,” alisema na kumtaka kuendelea kupeleka nyaraka za ushahidi hukohuko.
Kuhusu usalama, Makinda alisema: “Wewe umemchokoza na yeye akachokozeka, mnapotumia lugha mbaya mjue kuwa kila mtu ni binadamu. Tulieni suala la IPTL  lina utaratibu wake.”
 Alisema hakuna namna nyingine zaidi ya kupeleka nyaraka hizo kwa CAG na Takukuru.
“Sasa mnakaa mnatusambazia makaratasi haya sisi tufanye nini. Jambo ambalo mtu anajua lina tatizo anakuwa na utulivu. Kama unajiamini unakuwa na utulivu. Kama hujiamini unakuwa hauna utulivu,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu kauli ya Maswi, Kafulila alisema ameshazungumza jambo hilo nje ya bunge na kwamba hana hofu yoyote kwa kuwa anauhakika taarifa anazozisema ni sahihi.
Kuhusu yeye kutumiwa na Mbunge wa Musoma Vijijini kuwatuhumu Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake Maswi, alisema hakuna jambo hilo siyo la kweli.
“Juzi tulikutana na waandishi na nilitaka akaunti ya Kampuni ya Uwakili ya Mkono (Mkono & Co. Advocates) ichunguzwe. Itakuwaje mtu huyo huyo anipe documents (nyaraka)?” alihoji Kafulila.

Alisema kinafanyika sasa ni dalili zinazoonyesha kuwa viongozi hao wameanza kutapataka kwa kuwa wanafahamu malipo hayo hayakufanywa kwa njia halali.
“Huko ni kutapatapa hoja hapa ni Sh200 bilioni zilizochukuliwa. Naamini watachukuliwa hatua,” aliongeza.
Katika tuhuma zake Kafulila, alimuunganisha pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na vigogo wengine, wakiwamo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na  Serikali, wote akiwataja tu kwa vyeo bila majina.
Mawaziri waliotajwa ni Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Fedha na Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).  Ingawa Kafulila hakutaja kwa majina, Waziri wa Nishati ni Profesa Sospeter Muhongo, wa Fedha ni Saada Mkuya, Katibu Mkuu wa wizara hiyo (Nishati) ni Eliakim Maswi na AG ni Frederick Werema.
Kafulila alitoa tuhuma hizo bungeni alipokuwa akichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2014/15.
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Huyo Mwanasheria mkuu ni Mtetezi wa Mafisadi(wezi)kwa sababu anakula nao sahani mmoja. That make him MWIZI.Mheshimiwa Kafulila yupo sawa.