ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 11, 2014

NJIA RAHISI ZA KUFIKISHA HISIA KWA UMPENDAYE!-2


NI wakati mwingine mzuri kwa ajili yako msomaji mpendwa kujifunza mambo mbalimbali kuhusu uhusiano. Naamini unapata unachotarajia. Leo tunaendelea na somo letu lililoanza wiki iliyopita.

Ukweli uko wazi kuwa inapotokea mwanamke akampenda mwanaume huwa kuna ugumu wa kufikisha hisia zake. Ni suala la mfumo na tamaduni zetu. Haikubaliki. Lakini katika nyakati hizi za digitali, mambo yamebadilika.

Mwanamke anapohisi kumpenda mwanaume, wapo wanaoamua kusema tu kuwa wanawapenda. Ni hisia za ndani na za kweli lakini vipi kuhusu mapokeo? Habari mbaya ni kwamba, wanaume wengi wakiambiwa na wanawake kuwa wanapendwa, hukubali si kwa sababu nao wanawapenda ila kwa kuwaridhisha tu!

Kuna mambo mawili; kuwa nao kwa ajili ya kuwatumia na kuwaacha au kuwakubali ili wasionekane goigoi. Hili haliwezi kufutika vichwani mwa wanaume wengi kwa sababu ndiyo mfumo na kanuni za maisha yetu sisi Waafrika.

Kwa sababu hiyo sasa, ndiyo maana nikaandika makala haya ambayo kama mwanamke atatumia vizuri vipengele vilivyopo ataweza kumvuta mwanaume husika bila kujiingiza kwenye tatizo la kutumika na kuachwa baada ya muda mfupi. Inawezekana kabisa.

Katika toleo la wiki iliyopita nilieleza maana na namna ya mwanamke kujiweka katika mwonekano wa kuvutia. Hiyo ilikuwa hatua ya kwanza kabisa. Mwanamke anapaswa kuwa katika mwonekano nadhifu wakati wote. Tuendelee na vipengele vingine.

KUMVUTIA MWANAUME
Hapa ni tofauti kidogo na kipengele kilichopita. Kwanza ni lazima uvutie, lakini sasa hapa tunakwenda mbele zaidi. Umeshamwona mwanaume ambaye ni chaguo lako na kwa bahati mbaya haonekani kufikiria hilo. Je, uteseke moyoni? Hapana!

Vipo vitu ambavyo ukivifuata, utamsogeza mwanaume huyo na mwisho atakuwa wako. Huna sababu ya kubaki na jakamoyo.

MFUATILIE
Kitu cha kwanza kabisa ni kumjua vizuri huyo mwanaume. Anaishi wapi? Anafanya wapi kazi nk. Inawezekana ikawa vigumu kidogo kujua kila kitu kwa wakati mmoja lakini angalau ukijua kimojawapo itakuwa sawa, usipojua itakuwa imekula kwako!

Mathalani mnafanya naye kazi au huwa anakuja ofisini kwako, mnakutana kwenye mikutano au mnaishi mtaa mmoja nk. Hayo ni mambo ya muhimu kuyajua ili uweze kumweka katika mtego wako.

MVUTE KWAKO
Ninaposema hivyo, sina maana kuwa unatakiwa kumwambia moja kwa moja, la hasha! Vitendo vyako vinatosha kufikisha ujumbe. Vaa mavazi mazuri (naomba kusisitiza hapa mavazi ya heshima) ambayo hayatakutafsirisha kama mwanamke asiye na staha.

Wanaume wengi wanapenda kuwa na wanawake wenye staha na wanaotambua heshima yao. Ukijidanganya na kuvaa mavazi ya kujiachia mwili wako, maana yake atakuchukulia kama mwanamke ambaye hujatulia tu.
Atakuona kama mwanamke wa kutuliza haja zake, kisha anaendelea na maisha.

CHUNGUZA VITU AVIPENDAVYO
Wakati unajaribu kumvutia kwako pia chunguza vitu anavyopenda. Utaweza kujua kwa kumfuatilia hata kwa kidogo tu. Ukigundua angalau mtindo mmoja anaoupenda, mtege nao.

Tafuta mbunifu ambaye atakuweka katika mtindo ambao anavutika nao. Kumbuka ni sumu kumfuata mwanaume na kumwambia kuwa unampenda. Kamwe usianzishe uhusiano wewe.
Mwache afunguke mwenyewe. Inawezekana kabisa rafiki zangu. Wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!

GPL

No comments: